Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, changamoto za majadiliano ya kiekumene zisiwe ni kikwazo cha kusonga mbele: Mambo msingi: Wongofu, Uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na sadaka ta maisha. Papa Francisko asema, changamoto za majadiliano ya kiekumene zisiwe ni kikwazo cha kusonga mbele: Mambo msingi: Wongofu, Uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na sadaka ta maisha. 

Papa Francisko & Patriaki Bartolomeo I: Masalia ya Mt. Petro

Papa: Jambo la msingi ni hija ya wongofu wa maisha ya kiroho, uaminifu uliopyaishwa pamoja na majitoleo kamili, yanayowataka kusonga mbele kwa ujasiri mkuu. Masalia ya Mitume hawa wawili yawakumbushe na kuwaimarisha katika hija ili kwa pamoja waweze kutangaza na kushuhudia utume wa uinjilishaji na huduma kwa familia ya Mungu inayotoa kipaumbele cha uwepo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, ili kumfafanulia kuhusu zawadi aliyomtumia hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani. Kama kawaida, Sherehe hizi zilihudhuria na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo, mwendelezo wa mapokeo kwa Makanisa haya mawili kufanya hija ya pamoja. Hii ni changamoto ya kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kuweza  hatimaye, kufikia umoja kamili katika ngazi zote. Kwa sababu, wote wakiwa wamepatanishwa na Mwenyezi Mungu na kusamehewa dhambi zao; wanaitwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao yenye mvuto na mashiko! Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kuhusu Mapokeo ya Kanisa Katoliki juu ya kifodini cha Mtakatifu Petro kilichotokea wakati wa madhulunu ya Mfalme Nero na kwamba, alizikwa kwenye Kilima ambacho leo hii, ndiko kulikojengwa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro.

Kutokana na ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, Kaburi la Mtakatifu Petro tangu mwanzo likapata umaarufu sana na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wakatembelea mahali hapa. Papa Pio XII mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa, Juni 1939 aliruhusu utafiti ufanyike chini ya Altare ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na huko wakagundua ukuta uliojengwa kunako mwaka 150 BK, ukiwa na maneno yaliyoandikwa kwa lugha ya Kigiriki “πέτρα”. Ndani mwake kulikuwa na masalia ambayo yanasadikiwa kuwa ni masalia ya Mtakatifu Petro, Mtume na kwa sasa yanahifadhiwa chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. “Ex ossibus quae in Archbasilicae Vaticanae hypogeo inventa Beati Petri apostoli esse putantur” yaani “Mifupa iliyopatikana chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro inasadikiwa kuwa ni masalia ya mifupa ya Mtakatifu Petro”. Mtakatifu Paulo VI alichukua baadhi ya mifupa na kuiweka kwenye Kikanisa binafsi katika makazi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu Francisko alitamani kutoa zawadi kwa ajili ya Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol ili yaweze kuheshimiwa hata huko. Baba Mtakatifu anasema, hii ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili siku moja kuweza kufikia umoja kamili, kama ilivyo kwa watakatifu hawa huko mbinguni. Hii ni kumbu kumbu endelevu ya hija ya kitume iliyofanywa na Mtakatifu Paulo VI mjini Yerusalemu takribani miaka 50 iliyopita, akazawadiwa Picha ya Mtakatifu Andrea, ikiwa inawaunganisha wote katika imani na mapendo kwa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko wa kuongeza jitihada za majadiliano ya kiekumene ili kufikia umoja kamili na amani ambayo inabubujika kutoka katika sala. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Masalia ya Mtakatifu Petro yawekwa karibu na Masalia ya Mtakatifu Andrea anayeheshimiwa sana kwenye Kanisa la Costantinopol.

Itakumbukwa kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika mchakato kuelekea umoja kamili wa Kanisa, kama inavyoonesha katika ile Sala ya Kristo, ili wote wawe wamoja. Zawadi hii anasema Baba Mtakatifu inapania kuwa ni kielelezo cha hija ya majadiliano ya kiekumene ambayo kuna nyakati yanapambana na ugumu, ili daima yasindikizwe kwa alama wazi na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Matatizo, changamoto na hali ya kutoweza kufikia muafaka kwa sasa na kwa siku za usoni kisiwe ni kikwazo cha kushindwa kuwajibika kama Wakristo na zaidi kama viongozi wa Kanisa. Jambo la msingi ni hija ya wongofu wa maisha ya kiroho, uaminifu uliopyaishwa pamoja na majitoleo kamili, yanayowataka kusonga mbele kwa ujasiri mkuu. Masalia ya Mitume hawa wawili yawakumbushe na kuwaimarisha katika hija ili kwa pamoja waweze kutangaza na kushuhudia utume wa uinjilishaji na huduma kwa familia ya Mungu inayotoa kipaumbele cha uwepo wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, amepata faraja kubwa moyoni mwake, kuweza kumshirikisha mawazo haya. Ni matumaini yake kwamba, wataweza kuonana mubashara hivi karibuni.

Masalia Mt. Petro
13 September 2019, 15:43