Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka madaktari kuwa ni vyombo vya huruma na matumaini kwa wagonjwa na wala kifo laini si kielelezo cha uhuru wa mtu binafsi hata kidogo! Papa Francisko anawataka madaktari kuwa ni vyombo vya huruma na matumaini kwa wagonjwa na wala kifo laini si kielelezo cha uhuru wa mtu binafsi hata kidogo!  (ANSA)

Papa Francisko: Madaktari iweni vyombo vya huruma & matumaini!

Madaktari wawe ni mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa wagonjwa waliokata tamaa; kwa kusaidia kuzuia magonjwa; kwa kufanya uchunguzi wa kina pamoja na kuwaheshimu wagonjwa wenyewe. Changamoto za maisha kwenye miji mikuu imepelekea watu wengi kutumbukia katika msongo wa mawazo pamoja uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote! Utu wa binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maisha ya binadamu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayotishiwa na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za kifolaini na utoaji mimba. Hakuna uhuru wa kuchagua kifolaini, bali huu ni utamaduni wa kifo. Ni maneno mazito yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 2 Septemba 2019 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Chama cha Madaktari wa Saratani nchini Italia, “AIOM, yaani “Associazione Italiana di Oncologia Medica” kilichoanzishwa kunako mwaka 1973. Chama hiki kimekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma makini katika sekta ya afya; kwa kujikita zaidi katika tafiti za kisayansi; mchakato wa kuzuia nagonjwa ya Saratani; maboresho ya uchunguzi na tiba ya Saratani.

Juhudi hizi zinakwenda sanjari na majiundo endelevu ya madatari ili hatimaye, kuweza kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa Saratani. Chama cha “AIOM” ni daraja linalowaunganisha madaktari na mabingwa katika ulimwengu wa sayansi ili kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uhusiano wa dhati na wagonjwa wa Saratani ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kwani hiki ni kielelezo cha mshikamano na udugu unaopaswa kupyaishwa na kuboreshwa kila wakati. Mkutano mkuu wa Chama cha Madaktari wa Saratani Nchini Italia, unaotarajiwa kuadhimishwa hivi karibuni, iwe ni fursa ya kuboresha tiba na huduma kwa kila mgonjwa.

Mgonjwa anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa hasa kutokana na ukali wa mateso anayokabiliana nayo. Kila huduma ya matibabu inayotolewa kwa mgonjwa iwe ni chemchemi ya huruma na upendo kwa wagonjwa wanaoteseka. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya afya ya mwanadamu yanapaswa kuwa kweli ni chombo cha huduma kwa wagonjwa na wala si vinginevyo. Kamwe mgonjwa asionekane kuwa ni mgizo mzito, kiasi cha kuanza kuhalalisha kisheria mchakato wa kifolaini. Kwa haraka haraka anasema Baba Mtakatifu Francisko jambo hili linaweza kuonekana kuwa kama sehemu ya uhuru wa mtu binafsi; lakini ndani mwake, uhuru huu unafumbata ubinafsi unao thubutu kupima utu wa mtu kutokana na umuhimu wake. Kifolaini hakimsaidii mtu kupungumza maumivu.

Kumbe, ni dhamana na wajibu wa madaktari kuhakikisha kwamba, wanawasaidia wagonjwa kupata nafuu katika mahangaiko yao; kwa kujenga na kudumisha utamaduni unaothamini utu, heshima na haki msingi za binadamu; chemchemi ya matumaini katika maisha ya mwanadamu! Madaktari wawe ni mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa wagonjwa waliokata tamaa; kwa kusaidia kuzuia magonjwa; kwa kufanya uchunguzi wa kina pamoja na kuwaheshimu wagonjwa wenyewe kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Changamoto za maisha kwenye miji mikuu imepelekea watu wengi kutumbukia katika msongo wa mawazo pamoja uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Saratani sehemu mbali mbali za dunia hayana budi kujielekeza zaidi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; hii ni sehemu ya utu wa mwanadamu na maendeleo yake kijamii.

Baba Mtakatifu anakitaka Chama cha Madaktari wa Saratani Nchini Italia kuendeleza utume wake kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa wa Saratani, kwa kusaidia maboresho katika sekta ya afya na jamii katika ujumla wake; ili kuinua utu wa binadamu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu. Yeye mwenyewe awe ni nguvu na mwanga katika huduma; awasaidie kujenga na kudumisha: urafiki, mahusiano na mafungamano na wagonjwa pamoja na Mwenyezi Mungu. Kristo Yesu ni mganga aliyetumwa na Baba wa milele ili kumkomboa mwanadamu. Madaktari wanahamasishwa daima kuangalia: ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao; wawe wakarimu, daima wakijielekeza katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika upendo na mshikamano hasa kwa maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Madaktari wawe ni majirani wema kwa wagonjwa; daima waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa wagonjwa. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka madaktari wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwasimamia wao pamoja na wagonjwa wanaowahudumia.

Papa: Saratani

 

03 September 2019, 15:33