Tafuta

Vatican News
Katika kuelekea kilele cha miaka 80 tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia, Baba Mtakatifu Francisko anaomba kusali kwa ajili ya amani duniani! Katika kuelekea kilele cha miaka 80 tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia, Baba Mtakatifu Francisko anaomba kusali kwa ajili ya amani duniani!  (Vatican Media)

Wito wa Baba Mtakatifu Francisko kusali kwa ajili ya amani!

Katika kuelekea tukio la kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 80 tangu ilipotokea vita ya pili ya dunia,itakayofikia kilele chake tarehe Mosi Septemba,Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake,kati ya salam kwa lugha mbalimbali kwa watu wote,pia ametoa wito wa kusali kwa ajili ya amani ili pasiwepo na marudio ya majanga yanayosababishwa na chuki hadi kupelekea uharibifu tu, mateso na vifo.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake, kati ya salam kwa lugha mbalimbali kwa watu wote, pia ametoa wito wa kusali kwa ajili ya amani ili pasiwepo na marudio ya majanga yanayosabaishwa na chuki hadi kupelekea uharibifu tu, mateso na vifo. Na haya ni maneno yaliyosikika wakati wa salam kwa mahujaji wa lugha ya kipoland. Na hii ni kutokana na kuelekea katika fursa ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 80 tangu ilipotokea vita ya pili ya dunia, kumbukumbu itakayofikia kilele chake tarehe Mosi Septemba  hasa nchini Poland ambapo wanatafanya maadhimisho katika makambi ya wanazi. Katika kumbukumbu hiyo, miji mingi itafanya maadhimisho na hata ushiriki wa wakuu wa mataifa mbalimbali duniani. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu Francisko anatoa mwaliko wa nguvu kusali katika fursa hiyo ili amani iweze kutawala ndani ya mioyo ya watu.

Kumbukumbu ya Mtakatifu Agostino

Aidha Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwasalimia kwa namna ya pekee mahujaji karibia 500 wa Kanisa la kigiriki katoliki nchini Ukraine wakiwa na Askofu Mkuu Sviatoslav. Akiangazia siku ya kumbukumbu ya Mtakatifu Agostino, Askofu na mwalimu wa Kanisa, amewashauri waige mfano wake wa kuweza kugundua maisha ya undani ambayo yanapeleka kwa Mungu na jirani mwenye kuhitaji. Kila tarehe 28 Agosti Kanisa linaadhimisha sikukuu ya Mtakatifu Agostino,  Mwalimu wa Kanisa. Mtakatifu Agostino wa Hippo alizaliwa huko Thagaste, leo mji huo unaitwa Souk Ahras nchini Algeria, kunako tarehe 13 Novemba mwaka 354  na mauti yakamfikia kunako tarehe  28 Agosti, 430. Yeye alikuwa mtawa, mtaalimungu, padri na hatimaye askofu mkuu wa Hippo.

Ujana wa Mtakatifu Agostino haukuwa mzuri kufuatia na anasa 

Wakati wote wa ujana alifuata anasa na uzushi, bila kujali machozi ya mama yake. Alipata elimu yake nzuri ya lugha na ya ufasaha wa kuhubiri huko Thagaste, Madaura na hata katika Chuo Kikuu cha Karthago (karibu na Tunis) ingawa hakuwa daima mwanafunzi mzuri, mbali ya kuwa na akili ya pekee. Alimudu kikamilifu Kilatini, lakini si sana Kigiriki. Akiwa huko Karthago, mwaka 373 alisoma kitabu cha maadili cha Sisero ambacho kilibadilisha hisia zake hivi kwa maana hiyo anasema,“matumaini yote ya bure yakawa hayana maana kwangu, nikatamani hekima isiyokufa kwa ari isiyosemeka moyoni mwangu”. Lakini kwa kuamini ukweli haupatikani pasipo Yesu, ambaye hatajwi katika kitabu hicho, alianza kusoma Biblia, ila hakupenda tafsiri ya Kilatini wala yaliyomo, akiyaona tofauti na mtindo wa falsafa inayotafuta ukweli. Hivyo alisogea mbali na dini iliyoonekana kutotia maanani hoja za akili ambayo pamoja na imani ndizo “nguvu mbili zinazotuongoza kwenye ujuzi”. Haya yanaonekana katika mandiko yake ya baada ya uongofu wake huku  akitoa pia kauli mbili za msingi kuhusu kulenga ukweli: “Usadiki ili uelewe”, halafu “uelewe ili usadiki”.

Uongofu wa Mtakatifu Agostino

Uongofu wake ulitimia kunako tarehe 15 Agosti 386, akiwa na umri wa miaka 32, aliacha kufundisha na hata kuishi na mama mtoto, akaenda kwa muda Cassiciaco karibu na ziwa la Como nchini Italia , akiwa na Monika, Adeodatus na marafiki wachache, akarudi Milano alipobatizwa na Ambrosi pamoja na mwanae na rafiki yake Alipio usiku wa Pasaka ya mwaka 387. Baada ya kubatizwa hatimaye na kunuia akaishi kitawa Thagaste, alirudi Afrika; lakini akiwa njiani, huko Ostia, bandari ya Roma, mama yake Monika akafa. Ndoto yake ilikuwa kujitosa katika maisha ya sala na masomo pamoja na marafiki wake. Lakini hiyo ilidumu miaka mitatu tu.

Mtakatifu Agostino anafundisha sana kuhusu neema na dhambi

Katika suala la neema na dhambi ni Agostino aliyefundisha kwamba ubinadamu umerithi dhambi ya asili kutoka kwa Adamu. Uhuru wa asili umepotezwa na dhambi hiyo, na hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwao. Alisisitiza kwamba si binadamu anayemtafuta Mungu, bali Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mwenye dhambi. Utakaso unaopatikana kwa imani unasababisha ondoleo kamili la dhambi zote kabisa. Halafu mwamini anazidi kufanywa mpya kwa mchakato utakaokamilishwa na ufufuko wa siku ya mwisho. Mchakato huo wote ni kazi ya neema ya Mungu: bila hiyo, binadamu hawezi kuongoka, kukwepa dhambi na kufikia utimilifu wa wokovu. Hayo yote ni zawadi tu ya Mungu, kama vilivyo pia udumifu na stahili za mtu. Msisitizo huo  kwamba neema ni dezo, ulimwongoza  Mtakatifu Augustino kufundisha juu ya uteule, neema ambayo hakuna anayeweza kuikataa na ambayo inafikisha kwa hakika mbinguni. Kwa nini Mungu hawapi wote neema hiyo ni fumbo ambalo tuliinamie tu, kwa sababu hatuwezi kabisa kulielewa. Kwa vyovyote haiwezekani kumlaumu Mungu kwa ajili hiyo, eti si haki. Mawazo hayo yalikuja kukaziwa zaidi tena na watu kama Martin Luther, Yohane Kalvini na Janseni, namna iliyokataliwa na Kanisa Katoliki. Ni mengi ambayo tunaendelea kujifunza kutoka kwa Mtakatifu huyo aliyeongokea Mungu kwa nguvu ya roho Mtakatifu, lakini pia sala nyingi na machozi mengi ya mama yake Mtakatifu Monika!

28 August 2019, 13:28