Tafuta

Vatican News
Viongozi wakuu wa Makanisa sehemu mbali mbali za dunia, wanawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuunga mkono juhudi za kuzimisha moto kwenye misitu ya Amazonia. Viongozi wakuu wa Makanisa sehemu mbali mbali za dunia, wanawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuunga mkono juhudi za kuzimisha moto kwenye misitu ya Amazonia.  (AFP or licensors)

Janga la Moto Msitu wa Amazonia: Matamko ya Viongozi wa Makanisa

Tangu mwaka 2018 idadi ya matukio ya moto kwenye msitu wa Amazonia yameongezeka kwa asilia 84%, kiasi kwamba, wanaharakati pamoja na Jumuiya ya Kimataifa imeishutumu Serikali ya Brazil kwa kushindwa kudhibiti vitendo hivi na sasa moto huu umekuwa ni “Janga la Kimataifa” kwani linatishia; usalama, maisha na maendeleo ya watu wengi duniani. Mazingira ni nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Msitu wa Ukanda wa Amazonia unaoendelea kuteketea kwa moto kwa majuma kadhaa sasa una ukubwa wa kilometa za mraba milioni 5.5 na robo ya msitu huu, tayari imekwisha kuteketea vibaya kwa moto. Msitu huu unazalisha asilimia 20% ya hewa ya Oksijeni, kumbe, kuteketea kwa msitu huu ni janga la kimataifa, linalopaswa kushughulikiwa kwa njia ya umoja na mshikamano wa kimataifa. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza watu katika maafa makubwa.  Katika kipindi cha mwaka mmoja, yaani tangu mwaka 2018 idadi ya matukio ya moto kwenye msitu wa Ukanda wa Amazonia yameongezeka kwa asilia 84%, kiasi kwamba, wanaharakati pamoja na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, imeishutumu Serikali ya Brazil kwa kushindwa kudhibiti vitendo hivi na sasa moto huu umekuwa ni “Janga la Kimataifa” kwani linatishia; usalama, maisha, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi duniani.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 25 Agosti 2019, amesema, Jumuiya ya Kimataifa ina wasi wasi mkubwa kutokana na moto mkubwa unaoendelea kuteketeza Msitu wa Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushirikiana na kushikamana kwa dhati, ili kusaidia kuuzima moto huu ambao madhara yake ni makubwa. Msitu huu ni pafu la maisha ya watu katika sayari dunia. Wakati huo huo, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika tamko lake kuhusu majanga ya moto sehemu mbali mbali za dunia, anasikitika kusema kwamba, katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na wimbi kubwa la majanga ya moto sehemu mbali mbali za dunia. Jumuiya ya Kimataifa inashuhudia kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani na matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa mazingira na athari kwa maisha ya watu na mali zao.

Matukio ya majanga ya moto yanaendelea kuongezeka kila kukicha, changamoto na mwaliko kwa watu kubadili tabia. Wanasayansi na wataalam wa masuala ya mazingira wanaonya kwamba majanga ya moto yataendelea kusababisha athari kubwa kwa ekolojia ya dunia, lakini waathirika wakubwa ni nchi maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Majanga ya moto sehemu mbali mbali za dunia, yataendelea kuacha madhara makubwa hata kwa kizazi kijacho, kwa kuharibu ardhi inayotegemewa na watu wengi, miundo mbinu pamoja na maisha ya watu. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anapenda kuchukua fursa hii, kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa kupanda na kutunza miti, ili kusaidia mchakato wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi. Wajenge utamaduni wa kushinda kishawishi cha kukata miti na kuchoma misitu, ili kuchangia kudhibiti ongezeko la kiwango cha joto duniani.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, huu si wakati wa kutupiana lawama ni nani kasababisha janga la moto, lakini, ikumbukwe kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi ni jambo linalopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa pasi na mzaha. Uzalishaji wa hewa ya ukaa ni tishio kubwa kwa usalama, maisha na maendeleo ya familia ya Mungu. Majanga ya moto sehemu mbali mbali za dunia, iwe ni changamoto ya kukumbuka umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kuhakikisha kwamba, rasilimali na utajiri wa dunia unatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Binadamu anayo dhamana ya kutunza na kuendeleza utakatifu wa kazi ya uumbaji. Patriaki Bartolomeo wa kwanza ambaye ni kati ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaoendelea kujipambanua katika utunzaji bora wa nyumba ya wote anasema, tarehe 1 Septemba 2019 atazindua rasmi, Waraka wa Kichungaji Kuhusu Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote.

Hii ni tafakari ya kina kuhusu utunzaji bora wa mazingira ambayo imefanyika kwa kipindi cha miaka 30 ya maisha na utume wake kama Patriaki. Unachota amana na utajiri wake kutoka katika Mafundisho ya Kanisa la Kiorthodox katika kipindi cha karne ishirini zilizopita, kuhusu umuhimu wa utunzaji wa kazi ya uumbaji. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anapenda kuchukua fursa hii, kuwakumbuka na kuwaombea wale wote walioathirika kwa majanga ya moto sehemu mbali mbali za dunia. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina kuhusu mtindo na mfumo wa maisha yao; jinsi wanavyoishi, ulaji wao pamoja na vipaumbele vya maisha! Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil limeishauri Serikali ya Brazil kuhakikisha kwamba, inafanya kila linalowezekana ili kushiriki kudhibiti janga la moto kwenye Msitu wa Ukanda wa Amazonia. Changamoto hii inapaswa pia kuvaliwa njuga na nchi wanachama wanaounda Ukanda wa Amazonia, kuhakikisha kwamba, wanaibua mbinu mkakati utakaosaidia kudhibiti majanga ya moto yanayohatarisha ekolojia ya dunia.

Huu si wakati wa kufanya propaganda za kisiasa, bali ni wakati wa kushikamana na kushirikiana ili kuzima moto huu unaoendelea kusabisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Na habari zaidi zinabainisha kwamba, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, linapenda kuunganisha sauti yake, ili kulilia mshikamano wa dhati na wanannchi wa Amazonia, ili kwa pamoja waweze kushirikiana na kushikamana kuuzima moto huo. Mwaliko wa pekee kabisa unatolewa kwa viongozi wakuu wa Brazil, Bolivia, Marekani pamoja na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa. Watu wenye nafasi muhimu katika Jumuiya ya Kimataifa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wasaidie kusimama kidete kulinda na kutunza misitu ya Ukanda wa Amazonia unaoteketea kwa moto! Kamwe wasiruhusu uharibifu huu wa mazingira nyumba ya wote kuendelea, wala kamwe wasikubali kutaliwa na utamaduni wa kifo.

Kwa upande wake, Rais Jair Bolsonaro wa Brazil amesema, Serikali yake inaheshimu utawala wa sheria na itahakikisha kwamba, inawatafuta mpaka iwapate wale wote wanaliojihusisha na hujuma ya janga la moto kwenye Msitu wa Ukanda wa Amazonia, ili wafikishwe kwenye mkondo wa sheria. Kulinda, kutunza na kuendeleza Msitu wa Ukanda wa Amazonia ni haki na wajibu wa Serikali ya Brazil na kwamba, Serikali itaendelea pia kupambana na makampuni yanayovuna mazao ya msitu huu kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi. Serikali ya Brazil tayari imetuma vikosi vya ulinzi na usalama kusaidia zoezi la kuzima moto unaoendelea kusababisha wasi wasi mkubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Janga la Moto Amazonia

 

26 August 2019, 13:42