Tafuta

Papa Francisko anasema, mkutano wa Urafiki kati ya watu unaoadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake ni fursa ya kujenga na kudumisha madaraka ya kuwakutanisha watu. Papa Francisko anasema, mkutano wa Urafiki kati ya watu unaoadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake ni fursa ya kujenga na kudumisha madaraka ya kuwakutanisha watu. 

Ujumbe wa Papa Francisko kwenye Mkutano wa watu Italia, huko Rimini: Uso wa huruma & mapendo

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuuangalia Uso wa Kristo Yesu: fukara, mtii na mseja kamili, ili aweze kuwasafisha na kuwatakasa na hatimaye, kuwapatia uwezo mpya wa kuwaangalia jirani zao kwa: huruma, upendo na kuwajali jinsi walivyo. Katika mtazamo kama huu, kwa pamoja wanaweza kupiga ukulele wa shangwe na kusema, kwa hakika: Mungu ni mkuu, mwema na anawajali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini: “Meeting per l’amicizia fra i popoli” unaofanyika kila mwaka sasa umeingia katika awamu yake XL “40”. Kuanzia tarehe 18 -24 Agosti 2019, na unaongozwa na kauli mbiu “Jina lako linapata chimbuko lake kwa yale mambo msingi unayopania”. Hii ni sehemu ya utajiri unaobubujika kutoka katika mashairi yaliyowahi kutungwa na Mtakatifu Yohane Paulo II enzi ya ujana wake. Mkutano umezinduliwa, Jumapili tarehe 18 na Maria Elizabetta Alberti Casellati, Rais wa Senate ya Italia na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali mbali wa Kanisa na Serikali ya Italia na wajumbe kutoka ndani na nje ya Italia. Huu ni mwanya wa kutafakari na kupembua mambo msingi yanayorutubishwa katika maisha ya kila siku, ambayo wakati mwingine, hayapewi uzito unaostahili.

Hii inatokana na hali halisi inayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, kiasi kwamba, anaonekana kuwa na haraka kupita kiasi cha kutaka kila dakika kugeuza karatasi ya maisha yake. Kumbe, kila mwaka wajumbe wa mkutano wa urafiki wa watu wanapata nafasi ya kukaa na kutafakari mambo msingi yanayojenga na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Francesco Lambiasi wa Jimbo Katoliki la Rimini, Italia anasema, hii ni fursa ya watu kukutana na kuangaliana ili kugundua na kuonja: Ufunuo wa Sura ya huruma na upendo wa Mungu, yaani Kristo Yesu; Wito na dhamana yao katika maisha kama ilivyokuwa kwa Mathayo Mtoza ushuru na kwamba, mkutano huu uwe ni mahali pa ushuhuda wa ukarimu na ujenzi wa utambulisho wao wa Kikristo.

Baba Mtakatifu anawatakia heri na baraka wajumbe wote wanaoshiriki katika mkutano huu unaokumbukia miaka 40 tangu jitihada hizi zilipoanzishwa. Ni nafasi ya kuutafakari ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu, kama Mtakatifu Veronica alivyokirimiwa na Kristo Mwenyewe wakati wa Njia ya Msalaba, kuelekea Mlimani Kalvari. Mtumishi wa Mungu Don Luigi Giussani, muasisi wa Jumuiya hii, katika tafakari zake mbali mbali anausifia ujasiri wa Mtakatifu Veronica anayepasua umati wa watu na kuthubutu kumpangusa Kristo Yesu, Uso wake uliokuwa umetapakaa kwa damu! Tangu wakati huo, Veronica mwanamke wa kawaida sana kijijini, anainuliwa juu kutokana na ujasiri wake wa kupenda na kumthamini Kristo Yesu aliyekuwa anateseka.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni changamoto ya kuangalia na kuthubutu kuona, ujumbe unaotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa hata katika ulimwengu mamboleo. Watu watambue kwamba, Kristo Yesu anawapenda, anawathamini na anataka kuwashirikisha katika kazi ya ukombozi kama ilivyokuwa kwa Mathayo Mtoza Ushuru, ambaye Kristo Yesu, alimwangalia, akampenda, akamchagua na kumtuma kuwa ni chombo na shuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Watu wengi katika ulimengu mamboleo wameanguka na kuelemewa na changamoto na matatizo katika maisha; ni watu wanaojisikia pweke na kudhani kwamba, hakuna mtu awaye yote anayewaangalia na kuwathamini hata katika hali na mahangaiko yao. Hawa ni watu wanaokusanywa pamoja na kuangaliwa kama”namba” na kusahau kwamba, wanayo historia, utu, heshima na haki zao msingi kama inavyopaswa kuwa kwa wakimbizi na wahamiaji.

Kwa bahati mbaya watu hawa wana dhulumiwa, wanateswa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi. Wakati mwingine wanatumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Wote hawa wanao onekana kusahauliwa na Jumuiya ya Kimataifa, wanatamani kuona ufunuo wa Sura ya upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao, ili kuwa na uhakika wa usalama wa maisha yao pamoja na kuondokana na hofu na wasi wasi inayowakabili katika maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuuangalia Uso wa Kristo Yesu: fukara, mtii na mseja kamili, ili aweze kuwasafisha na kuwatakasa na hatimaye, kuwapatia uwezo mpya wa kuwaangalia jirani zao kwa: huruma, upendo pamoja na kuwajali jinsi walivyo. Katika mtazamo kama huu, kwa pamoja wanaweza kupiga ukelele wa shangwe na kusema, kwa hakika: Mungu ni mkuu, ni mwema na bado anaendelea kuwaangalia watu wake!

Waamini watambue kwamba, wao ni sehemu ya historia ya upendo wa Mungu kwa waja wake; watu waliokuwa wanabezwa, lakini, Mwenyezi Mungu kwa huruma na upendo wake, akawaona, akawatakasa na kuwachagua kuwa ni sehemu ya urithi wake. Leo hii wanao utambulisho wao makini na wamepewa jina! Mtakatifu Yohane Paulo II anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii yanayotoa utambulisho wao kama Jumuiya ya waamini. Wito wa Mathayo mtoza ushuru, aliyebahatika kuangaliwa na Kristo Yesu kwa jicho la upendo na huruma; akakirimiwa nguvu ya kuweza kusimama na kuacha yote, tayari kumfuasa Kristo Yesu. Mathayo akapata amani, furaha na utulivu wa ndani. Ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Kristo, ulimwezesha Mathayo kuwa mtu huru kwa kuuvua utu wake wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa matumaini na maisha mapya!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini anaendelea kufafanua kwamba, huu ndio utambulisho na ushuhuda unaopaswa kutolewa na Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Wafuasi wa Kristo wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini ili kuzima kiu ya matumaini miongoni mwa watu wa Mataifa. Wakristo waakisi Uso wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili waweze kuwa ni wafuasi wamisionari wa furaha ya Injili na kwamba, majina yao yatakuwa yameandikwa mbinguni. Hii ni furaha ambayo hakuna mtu awaye yote anayeweza kuwapokonya katika maisha. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, furaha ya Injili inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, zawadi wanayopaswa kuwashirikisha wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha.

Hii ndiyo maana ya kuwa mtume mmisionari! Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini ni fursa makini ambayo inawawezesha watu kujenga madaraja ya kukutana na kuangaliana, ili kuimarisha utambulisho wao kama wafuasi wa Kristo Yesu. Hii ndiyo njia muafaka ya kukumbukia miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia. Ni nafasi ya kusonga mbele kwa ari na matumaini makubwa, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja na kati yao, ili kuwaunga mkono katika jitihada mbali mbali wanazozitekeleza katika Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Hii ni kumbukumbu ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, kwa kuwawezesha kutekeleza dhamana na shughuli mbali mbali za kitume, kama kielelezo cha kipaji cha ubunifu katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa watu wa Mungu.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, sera na mikakati kama hii, itasaidia kupyaisha maisha na kuwapatia waamini nguvu mpya ya kushuhudia imani kwa kuendelea kusoma alama za nyakati na kujibu kilio cha maskini kama kielelezo cha imani tendaji. Baba Mtakatifu anawatakia wote heri na baraka kwa kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Askofu Francesco Lambiasi wa Jimbo Katoliki la Rimini, Italia katika Ibada ya ufunguzi wa Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini: “Meeting per l’amicizia fra i popoli”, amesema, wakati huu kuna vuguvugu la upyaisho wa imani inayopaswa kumwilishwa katika matendo ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu. Kristo Yesu amekuja kutupa duniani moto wa upendo, uliowaka kiasi cha kumpandisha juu ya Msalaba, pale Mlimani Kalvari na hapo akayamimina maisha yake, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo unao okoa.

Amesema, Neno la Mungu ni sawa na upanga wenye makali kuwili; unagawanya na kutenganisha yale mema na mabaya katika jamii. Neno la Mungu linakuza utukufu na utakatifu wa Mungu na kuwapatia waamini fursa ya kuona mapungufu yao katika maisha, tayari kutubu na kumwongokea Mungu. Inasikitisha kuona kwamba, moto ambao wakristo wamebahatika kuupokea katika Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, unaendelea kufifia taratibu na hata pengine, kuna Wakristo ambao moto huu umezimika kabisa na kwamba, wanahitaji nguvu ya Roho Mtakatifu kuweza kupyaisha tena ari na mwamko wa maisha na utume wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kwa namna ya pekee kabisa, Mama Kanisa anawahamasisha vijana kuambata wongofu wa ndani, tayari kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Walimwengu wanataka kukutana na Wakristo ambao kwa hakika ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Mfufuka katika uhalisia wa maisha yao.

Katika kipindi cha miaka arobaini cha maisha na utume wa Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia, tema mbali mbali zimeweza kujadiliwa kwa kusoma alama za nyakati. Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; Umuhimu wa ujenzi wa madaraja ya watu mbali mbali kukutana, Utambulisho; Utu, heshima na mafao ya wengi; Wema, uzuri na utakatifu wa maisha. Ushuhuda wa imani tendaji katika ushirikiano unaoongozwa na kanuni auni ni kati mambo yanayoendelea kupewa kipaumbele cha pekee! Mkutano huu limekuwa ni Jukwaa la kubadilishana uzoefu, mang’amuzi na changamoto za maisha katika ulimwengu mamboleo. Katika mkutano huu wa Rimini, kati ya vigogo wanaoendelea kushirikisha mang’amuzi yao ni pamoja na Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Papa: Rimini 2019
19 August 2019, 10:56