Tafuta

Siku kuu ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu ilianzishwa kunako mwaka 1955 na Papa Pio wa Kumi na Mbili. Siku kuu ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu ilianzishwa kunako mwaka 1955 na Papa Pio wa Kumi na Mbili. 

Siku kuu ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu: Ufalme wa Kristo Yesu

Siku kuu ya Bikira Maria Malkia wa Mbingu, 22 Agosti, ilitangazwa na Papa Pio XII, mwaka 1955. Bikira Maria anashiriki utukufu na ufalme wa Yesu na kwamba, Mama Kanisa anapenda kumweka mbele ya macho ya waamini kama kielelezo makini na mfano wa matumaini ya Wakristo wote ambao pia wanashiriki katika: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 22 Agosti, kila Mwaka, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Bikira Maria Malkia wa mbingu, Siku kuu iliyoanzishwa na Papa Pio wa XII kunako mwaka 1955. Hii ni kumbu kumbu inayoadhimishwa na Mama Kanisa kwa heshima ya Bikira Maria, siku chache tu baada ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, hapo tarehe 15 Agosti. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, mwili na roho, Bikira Maria anawafundisha watu wa Mungu kumwadhimisha Mungu kwa sababu amewatendea mambo makuu. Bikira Maria, Malkia wa mbingu, anawaalika watu kumwadhimisha Mungu kutokana na ukuu, uzuri na wema wake katika maisha yake. Waamini wanahamasishwa katika hija ya maisha yao, kuhakikisha kwamba, wanatafuta mambo makuu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha yao; kwani Yeye peke yake, ndiye aliye mkuu vinginevyo, wanaweza kujikuta wakiwa wanazama katika mambo madogo madogo ya maisha.

Haya ni mambo ambayo wakati mwingine hayana mvuto wala mashiko! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna watu wamezama hadi kutopea huko waliko kwa kuwa na mamuzi mbele, kinyongo, wivu, uadui na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, uchu wa mali na madaraka. Haya yote yanawaonesha watu waliovaa ngozi ya Kondoo, lakini ukweli wa mambo, watu hawa ni sawa na “mbwa mwitu wakali”. Bikira Maria anashiriki utukufu na ufalme wa Kristo Yesu na kwamba, Mama Kanisa anapenda kumweka mbele ya macho ya waamini kama kielelezo makini na mfano wa matumaini ya Wakristo wote ambao pia wanashiriki katika: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Kumbu kumbu hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusimama kidete katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika msingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli.

Kanisa bado linaendelea kumwomba Bikira Maria Malkia wa amani aweze kuwaombea walimwengu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na vita, migogoro na kinzani za kijamii, ili watafute amani na kuiambata, kwani amani ni jina jipya la maendeleo na ustawi wa wengi. Bikira Maria ni Malkia wa Mbingu, yeye pia ni Malkia wa Mababu, Mitume na Mabikira kama ambavyo Kanisa linavyomwimbia katika Litania ya Bikira Maria.

Bikira Maria Malkia wa Mbingu



22 August 2019, 10:57