Tafuta

Papa Francisko: Kumbu kumbu ya kuporomoka kwa Daraja la Morandi: Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwanadamu: Imani, matumaini na mapendo ni muhimu sana! Papa Francisko: Kumbu kumbu ya kuporomoka kwa Daraja la Morandi: Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwanadamu: Imani, matumaini na mapendo ni muhimu sana! 

Daraja la Morandi: Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwanadamu: Imani na Matumaini

Baba Mtakatifu Francisko katika kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Daraja la Morandi liporomoke na kuanguka chini, amemwandikia barua Mhariri mkuu wa Gazeti la “Il Secolo XIX”, kama sehemu ya kumbu kumbu hii iliyotokea hapo tarehe 14 Agosti 2018 na kupelekea watu 43 kupoteza maisha yao, wengine wengi kupata majeraha na vilema vya kudumu. Fumbo la Msalaba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umegota mwaka mmoja tangu Daraja la Morandi “Ponte Morandi” lililoko mjini Genova, Kaskazini mwa Italia, liliporomoka na kuanguka chini na hivyo kusababisha watu 43 kupoteza maisha. Wengi wao ni watu waliokuwa wanatoka kuvinjari maisha; wengine ni wale waliokuwa kazini kama kawaida. Mji wa Genova ukagawanyika mara mbili kutokana na ajali hii. Watu wengi wameathirika kwa sababu makazi ya watu na miundo mbinu ya shughuli za huduma na uzalishaji iliharibika vibaya sana. Serikali ya Italia inaendelea kufanya uchunguzi juu ya tukio hili kwa kuwa na watuhumiwa 70 na ukikamilika, wahusika watafikishwa kwenye mkondo wa sheria. Inakadiriwa kwamba, kuanguka kwa Daraja la Morandi kumesababisha hasara ya zaidi ya milioni 80 za Euro na kwamba, wafanyabiashara na makampuni mbali mbali yamepoteza kiasi cha milioni 400. Msongamano wa magari mjini Genova imekuwa ni changamoto kubwa sana. Familia 566 hazina makazi baada ya kuanguka kwa Daraja la Morandi. Tarehe 28 Juni 2019 Magofu ya Daraja la Morandi yakabomolewa, ili kuanza ujenzi wa Daraja jipya la Morandi unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2020.

Baba Mtakatifu Francisko katika kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Daraja la Morandi liporomoke na kuanguka chini, amemwandikia barua Mhariri mkuu wa Gazeti la “Il Secolo XIX”, kama sehemu ya kumbu kumbu hii iliyotokea hapo tarehe 14 Agosti 2018 na kupelekea watu 43 kupoteza maisha yao, wengine wengi kupata majeraha na vilema vya kudumu. Baadhi yao wakajikuta hawana tena makazi na hivyo kulazimika kuishi kwenye makazi ya muda. Baba Mtakatifu anapenda kuwakumbusha watu wa Mungu mjini Genova kwamba, bado anawakumbuka katika sala na sadaka yake. Kwa matukio kama haya, si rahisi sana kuweza kusahau. Uchungu unazidi kwa kutambua kwamba, maafa haya yangeweza kuzuilika, ikiwa kama wadau mbali mbali wangelitekeleza dhamana na wajibu wao barabara na kwa wakati. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hana majibu ya mkato, kwani wakati mwingine katika muktadha wa namna hii, maneno ya binadamu hayawezi kusadifu hata kidogo. Mtu akiangalia madhara yaliyojitokeza, kamwe hawezi kuacha kububujikwa na machozi, kushikwa na bumbuwazi na kuzama katika tafakari ya kina, kuhusu kazi ya mwanadamu.

Lakini, Baba Mtakatifu anasema, ndani ya moyo wake, kunaibuka hisia za sala zaidi, ambazo anapenda kuwashirikisha ndugu zake katika Kristo Yesu! Kamwe wasiruhusu matukio kama haya yavuruge umoja, upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Isiwe ni sababu ya kufutilia mbali kumbu kumbu pamoja na matukio muhimu yaliyojitokeza katika maisha yao. Baba Mtakatifu anasema, anayo kumbu kumbu kwani Genova ni mahali walipotoka wazazi wake na kuhamia Argentina. Anatambua sadaka na majitoleo ya wananchi wa Genova, kwani hawa ni wachapa kazi na mfano bora wa kuigwa; ni watu wenye matumaini na kamwe hawawezi kukatishwa tamaa na mambo mpito! Katika shida na mahangaiko yao ya ndani, watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anafanya hija ya maisha, akiwa anaandamana nao kwa njia ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Katika hali na mazingira kama haya, wajitahidi kuona na kuguswa na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu. Pale juu Msalabani, Kristo Yesu, ametundika mateso na mahangaiko ya binadamu wote.

Akiwa ametundikwa Msalabani, watu wengi walimdhihaki, wakamtukana na kumdhalilisha; wakamchoma mkuki ubavuni, na hatimaye, akafa kifo cha aibu pale Msalabani. Kristo Yesu katika mambo yote anasema Baba Mtakatifu Francisko alikuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi. Katika shida na mahangaiko ya binadamu, Kristo Yesu, aliweza kuhuzunika, akatoa machozi, akawa faraja na chombo cha baraka kwa wale waliokuwa wanamzunguka. Katika shida na magumu ya maisha, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, wawe wepesi kumkimbilia na kumwangalia Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, ili kujiaminisha na kujikabidhi katika ulinzi na tunza yake. Kristo Yesu ni jibu makini katika mateso na mahangaiko ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, pale mlimani Kalvari, Yesu alipokuwa ametundikwa Msalabani, chini ya Msalaba, alikuwepo Mama yake mpendwa, Bikira Maria, “Stabat mater”. Akajionea na kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya Mwanaye mpenzi. Hata katika shida na mahangaiko ya waamini, wakumbuke kwamba, huko mbinguni, wanaye Mama na Mwombezi; anayewangalia kwa jicho la huruma na mapendo; anayewaombea mbele ya Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu.

Kumbe, wasiwe na wasi wasi kukimbilia chini ya ulinzi na tunza yake ya kimama wanapokabiliwa na mateso, magumu na changamoto za maisha. Mtoto mbele ya Mama yake, anajisikia salama zaidi. Hivi ndivyo ilivyokuwa na hata kujitokeza kwa Benedetto Pareto kunako mwaka 1490, Mlimani Figonga, alipotokewa na Bikira Maria na kujitambulisha kuwa ni Mama wa Yesu, na kumwomba, wamjengee Kikanisa. Katika shida na mahangaiko yao ya ndani, wanapoona kana kwamba, wameelemewa na mazito kiasi cha kutaka kukata tamaa, wanyanyue tena nyuso zao na kumwangalia Bikira Maria, Mlinzi wao, ili kujiaminisha kwake, kwa imani na matumaini. Baba Mtakatifu anasema binadamu wana karama, mapungufu na udhaifu wao, lakini wakumbuke kwamba, wanaye Baba mwingi wa huruma na mapendo wanayeweza kumwendea wakati wowote ule! Wanaye ndugu yao ambaye ni Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, anayefanya hija ya maisha pamoja na ndugu zake bila kusahau uwepo wa Roho Mtakatifu, anayewahudumia na kuwaongoza. Wasisahau kwamba, wanaye Mama mbinguni, anayeendelea kuwalinda na kuwapatia tunza yake ya kimana na kamwe hawezi kuwatelekeza hata kidogo!

Watambue kwamba, katika shida na mahangaiko yao, bado pia kuna Jumuiya ya Wakristo, kuna Kanisa mahalia la Genova na pamoja nao, Baba Mtakatifu Francisko pia anashiriki kikamilifu katika mateso na mahangaiko yao. Pale wanapotambua ukubwa wa udhaifu wao wa kibinadamu, hapo ndipo wanapoweza pia kutambua na kuthamini mahusiano na mafungamano yao ya kibinadamu; kifungo cha upendo kinachowaunganisha kama wana familia na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, familia ya Mungu mjini Genova ni watu ambao wanajali na kuthamini sana mshikamano na mafungamano ya kijamii. Huu ni muda wa kutembea bega kwa bega bila kukata wala kukatishwa tamaa; wawe ni nguzo ya wanyonge na dhaifu ndani ya jamii. Baada ya maafa haya makubwa, familia ya Mungu mjini Genova imeweza kusimama tena, ili kuwatia shime wale waliothirika zaidi. Baba Mtakatifu mwishoni mwa ujumbe wake kwa familia ya Mungu mjini Genova, inayoadhimisha kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Daraja la Morandi lililo poromoka na kuanguka chini, anawataka kuwa ni watu wa matumaini na kamwe, wasiruhusu watu kuwapoka matumaini haya. Wanaposali na kujiombea, wamkumbuke hata yeye katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa: Ponte Morandi
13 August 2019, 15:38