Tafuta

Nia za Papa Francisko kwa Mwezi Julai: Ili haki iweze kutawala duniani. Mahakimu na Majaji wafanye kazi za barabara katika ukweli na uwazi, ili kudumisha haki na amani duniani! Nia za Papa Francisko kwa Mwezi Julai: Ili haki iweze kutawala duniani. Mahakimu na Majaji wafanye kazi za barabara katika ukweli na uwazi, ili kudumisha haki na amani duniani! 

Nia za Papa Francisko mwezi Julai: Haki duniani!

Papa Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Julai 2019 anaombea haki ili iweze kutawala na kudumishwa ulimwenguni. Wale wote waliopewa dhamana na jamii ya kuhakikisha kwamba, haki inatendeka, wafanye kazi hii kwa uaminifu, uadilifu, ukweli na uwazi. Haki ni muhimu sana katika ulimwengu ambamo rushwa na ufisadi, uchu wa mali, madaraka na faida kubwa vinatawala!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya kijamii, changamoto ambayo imevaliwa njuga na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, unaoendelea kusoma alama za nyakati, ili ujumbe na nia za Baba Mtakatifu kila mwezi ziweze kuwafikia watu wengi zaidi mahali walipo! Utume wa Sala Kimataifa kwa sasa unaendelea kuchanja mbuga kwa kutumia mitandao ya kijamii, ili kuweza kuwashirikisha waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema katika sala, huku wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu Francisko.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii yanaliwezesha hata Kanisa kuweza kuvuka mipaka ya kijiografia na kuwa karibu zaidi na watu kwa njia ya mitandao ya kijamii. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 175 tangu kuanzishwa kwa Utume wa Sala Kimataifa, Baba Mtakatifu amekiri kwamba, huu ni mhimili wa maisha na utume wa Kanisa! Anawashukuru wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, Utume wa Sala Kimataifa unakita mizizi yake hata katika ulimwengu wa kidigitali. Mitandao ya kijamii, iwe ni majukwaa ya kutangaza na kushuhudia: wema, huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu na pia ilete mvuto wa kumwendea Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Julai 2019 anaombea haki ili iweze kutawala na kudumishwa ulimwenguni. Wale wote waliopewa dhamana na jamii ya kuhakikisha kwamba, haki inatendeka, wafanye kazi hii kwa uaminifu, uadilifu, ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika ulimwengu ambamo rushwa na ufisadi vinaendelea kushika kasi ya ajabu; uchu wa mali na madaraka pamoja na baadhi ya watu kutafuta faida kubwa kwa gharama ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, haki na usawa vinatendeka kwa watu wote bila ubaguzi.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Mahakimu na Majaji ni watu muhimu sana ambao maamuzi yao yanachangia kwa kiasi kikubwa katika masuala ya haki msingi za binadamu, ustawi, maisha na maendeleo ya watu. Utekelezaji wa dhamana na majukumu yao bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote kile, utawawezesha kuwa mbali na kishawishi cha upendeleo na rushwa; mambo ambayo yanaweza kuathiri hukumu wanayotarajia kutoa Mahakamani. Baba Mtakatifu anawaalika wafanyakazi wa Mahakama sehemu mbali mbali za dunia kufuata mfano wa Kristo Yesu, ambaye ametangaza na kusimamia ukweli hadi dakika ya mwisho bila kuteteleka wala kuyumbishwa

Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya video unasambazwa sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa kwa kushirikiana na kampuni ya La Machi pamoja na vyombo vya mawasiliano vya Vatican vinavyoratibu usambazaji wake. Ujumbe huu unaweza kupatikana kwa anuani ifuatayo: (www.thepopevideo.org).

Papa: Nia Julai 2019
09 July 2019, 14:09