Tafuta

Vatican News
Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani ni sehemu ya matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani pamoja na uporaji wa rasilimali na utajiri kutoka katika nchi changa zaidi duniani! Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani ni sehemu ya matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani pamoja na uporaji wa rasilimali na utajiri kutoka katika nchi changa zaidi duniani! 

Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 2019: Utu wa binadamu!

Kila kukicha katika ulimwenguni kuna ibuka wataalam wa ubaguzi na kwamba, kila siku ukatili unaongezeka duniani. Nchi changa duniani zinaendelea kupokwa rasilimali na utajiri wake kutokana na soko la wajanja wachache. Vita inaendelea kupamba moto katika baadhi ya maeneo yenye utajiri na rasilimali adhimu. Kuna wafanyabiashara wanaoendelea kujineemesha kwa biashara ya silaha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Huduma, upendo na mshikamano wa dhati kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ni kati ya mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Anaguswa na shida pamoja na mahangaiko ya wakimbizi, wahamiaji, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 itaadhimishwa Jumapili,  tarehe 29 Septemba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Si Wahamiaji peke yao”.

Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya binadamu kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa mwaka huu 2019 linaendesha kampeni inayopania kuragibisha maboresho katika shughuli kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Hili si suala la wahamiaji na wakimbizi peke yake, bali linagusa na kutikisa misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kutowatenga watu kwa sababu ya maamuzi mbele, kwani kwa kufanya hivi, ni kuendeleza ukatili dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019, kwa mwezi Julai anapenda kutoa angalisho kwa kufanya rejea katika Maandiko Matakatifu: “Angalieni msidharau mmojawapo wa wadogo hawa, kwa maana nawaambia ya kwamba malaika zao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni” ( Mt. 18:10). Baba Mtakatifu anakaza kusema si wahamiaji peke yao: bali hakuna sababu msingi ya kumtenga mtu yeyote yule.

Kila kukicha katika ulimwengu mamboleo kuna ibuka wataalam wa ubaguzi na kwamba, kila siku ukatili unaongezeka duniani kutokana na vitendo vya kibaguzi. Nchi changa duniani zinaendelea kupokwa rasilimali na utajiri wake kutokana na soko la wajanja wachache. Vita inaendelea kupamba moto katika baadhi ya maeneo yenye utajiri na rasilimali adhimu. Kuna wafanyabiashara wanaoendelea kujineemesha na kujitajirisha kwa biashara haramu ya silaha duniani, “inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia”.

Baba Mtakatifu anasema, jambo la kushangaza ni kuona kwamba, pamoja na yote haya yanayotendeka, bado kuna watu wanathubutu kabisa kuwageuzia kisogo wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta, usalama, hifadhi na maisha bora zaidi! Kamwe hawataki kuwaona na wala kuwasaidia na kusahau kwamba, hawa ni matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani pamoja na ukwapuaji wa rasilimali na utajiri kutoka katika Nchi changa zaidi duniani. Mara nyingi watu ni “mabingwa wa kuzungumzia amani duniani”, lakini hao hao, kwa upande mwingine ndio wauzaji wakuu wa silaha zinazoendelea kusababisha majanga makubwa kwa maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia!

Huu ni unafiki mkubwa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, waathirika wakuu ni watoto, wazee, maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanaoachwa kuambulia “makombo yanayoanguka kutoka meza za wakubwa” kama ilivyo kwenye Maandiko Matakatifu katika ule mfano wa mtu tajiri na Lazaro maskini! Kanisa linaitwa kutoka na hivyo linathubutu kuchukua hatua ya kwanza bila woga wala makunyanzi, ili kwenda kukutana; kuwatafuta wale walio mbali, ili kuwakusanya njia panda na hatimaye, kuwakaribisha wale wote wanaotengwa na kunyanyaswa. Hawa ni wale ambao jamii yenyewe inawatenga.

Sera na mikakati ya uchumi wa kibaguzi ni kuendelea kuwanufaisha matajiri kwa kuwa matajiri zaidi na maskini kwa kuendelea kutopea katika umaskini, kiasi hata cha kukandamizwa na “kugeuzwa kuwa kama soli ya kiatu”. Maendeleo ya kweli yanafumbatwa katika sera na mikakati fungamani inayowashirikisha watu wote katika: kuamua, kupanga na kutekeleza. Hizi ni sera zinazosaidia ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja kutupia jicho kwa mahitaji msingi ya kizazi kijacho. Baba Mtakatifu anasema kwa msisitizo kwamba, maendeleo ya kweli ni fungamani, yanasaidia uzalishaji na kuonesha sera, dira na mwelekeo kwa siku za mbeleni.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusaidia kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa mintarafu huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji duniani.  Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu na fungamani itaendelea kuragibisha huduma ya upendo kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, ili kuwasaidia waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kupata uelewa mpana zaidi wa tema zinazochaguliwa na Baba Mtakatifu.

Papa: Wakimbizi

 

02 July 2019, 15:25