Tafuta

Vatican News
Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzisha kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM: Ari na mwamko wa kimisionari, umoja na mshikamano! Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzisha kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM: Ari na mwamko wa kimisionari, umoja na mshikamano! 

Jubilei ya Miaka 50 ya SECAM: Papa Paulo VI na Mchango wake!

SECAM ilizinduliwa rasmi tarehe 31 Julai 1969 huko Uganda wakati wa hija ya kitume ya Mtakatifu Paulo VI. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na mafanikio makubwa na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Ari na moyo wa kimisionari, miundo mbinu ya uongozi imeendelea kuimarika! Sasa ni wakati wa kulitegemeza Kanisa la Afrika kwa hali na mali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, Jumapili iliyopita, tarehe 21 Julai 2019 limezindua Maadhimisho Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wa SECAM Barani Afrika. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu mkuu Gabriel Mbilingi, Rais wa SECAM. Jubilei inaongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Kama kawaida ya maadhimisho ya Jubilei, hiki ni kipindi muafaka cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Lengo kuu la Jubilei hii ni kumshukuru Mungu kwa zawadi imani kwa familia ya Mungu Barani Afrika. Huu ni wakati kwa waamini kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo, hivyo wanaitwa na kutumwa kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

SECAM ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uliowahamasisha Maaskofu kutoka Barani Afrika kushikamana kwa hali na mali, ili kuweza kukoleza ari na moyo wa kimisionari, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. SECAM ikazinduliwa rasmi tarehe 31 Julai 1969 huko Uganda. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na mafanikio makubwa na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Askofu mkuu Charles Gabriel Palmer Buckle, Mweka hazina wa SECAM, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Rubaga, Jimbo kuu la Kampala, Uganda amegusia kuhusu ari na mwamko wa kimisionari kutoka Barani Afrika na kwamba, kwa sasa Bara la Afrika limekuwa ni kitalu cha miito ya kimisionari sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa Barani Afrika limeendelea kuwa ni chachu kubwa ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu hasa katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii.

Kwa upande wake, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, amelitaka Kanisa Barani Afrika kuendelea kujizatiti zaidi katika mchakato wa kujitegemea kwa rasilimali watu, fedha na vitu kama sehemu ya ukomavu wa Kanisa, linalosonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika azma ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Rais Museveni amewapongeza Maaskofu Barani Afrika na kuwataka kuimarisha tasaufi ya maisha ya kiroho inayokita mizizi yake katika Injili ya ukarimu na huduma kwa watu wa Mungu. Amelitaka Kanisa kusaidia mchakato wa maboresho ya sekta ya kilimo, ili kuwakwamua watu wengi kutoka katika umaskini wa hali na kipato, kwa kuongeza tija na uzalishaji. Bara la Afrika likiweza kuboresha sekta ya kilimo, watu wake watapata fedha ya kuboresha hali zao za maisha.

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Paulo VI alipotembelea kwa mara ya kwanza Bara la Afrika kwa kufanya hija ya kitume nchini Uganda kwanza kabisa aliitaka familia ya Mungu Barani Afrika kuwa mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake; kujenga na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia habari Njema ya Wokovu Barani Afrika. Alisema, viongozi wa kisiasa Barani Afrika wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa misingi ya haki, amani na maridhiano. Kanisa kwa kushirikiana na Serikali mbali mbali Barani Afrika zisaidie kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa: kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu, wanawake Barani Afrika wakipewa kipaumbele cha kwanza!

Alilitaka Kanisa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, afya, kilimo na huduma bora za maji safi na salama.  Katika muktadha huu, Mtakatifu Paulo VI alikazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene Barani Afrika kama njia ya kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu. Alikazia pia umuhimu wa kukuza na kuendeleza mashirika na vyama vya kitume ili kusaidia majiundo, malezi na makuzi ya imani, tayari kuchangia katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu! Mtakatifu Paulo VI, katika hija yake ya kitume, aliwataka waamini kuiga mfano bora wa Mashahidi wa Uganda walioyamimina maisha yao kama kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Akawataka wawe jasiri na thabiti katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani. Ujasiri wa imani unawawezesha waamini kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao.

Waamini waendelee kuboresha imani yao kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na Ibada mbali mbali, ambazo zitawasaidia kuwa kweli ni wafuasi wamisionari wa Kristo Yesu, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Imani iwasaidie kuonesha upendo kwa Mungu na jirani. Mtakatifu Paulo VI, wakati alipokuwa anazungumza na Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika, alikazia umoja na mshikamano katika urika wa Maaskofu katika kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ili kukuza na kudumisha maisha ya Kikristo Barani Afrika kwa kutambua kwamba, tangu wakati huu, waafrika wenyewe wanapaswa kuwa ni wamisionari Barani Afrika tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Dhamana hii inajikita katika ujenzi wa miundo mbinu ya Kanisa, itakayoliwezesha Kanisa kuonenana, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Kanisa kwa asili ni la kimisionari, dhamana inayopaswa kuendelezwa na kudumishwa Barani Afrika.

Ni kutokana na muktadha huu, Kanisa Barani Afrika linaendelea kuhamasishwa kujitegemea kwa rasilimali watu, yaani waamini watakaojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kanisa linawahitaji wakleri, watawa na makatekista walioandaliwa barabara ili kuweza kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika mchakato wa utamadunisho, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Kanisa Barani Afrika linaendelea kubaki kuwa ni Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume; kwa kuchota amana na utajiri wake kutoka katika Mapokeo ya Kanisa. Kanisa Barani Afrika liendelee kuboresha Liturujia ya Kanisa ili Mwenyezi Mungu aweze kupewa sifa na utukufu na mwanadamu apate kukombolewa. Kanisa Barani Afrika litambue kwamba, ni Mama na Mwalimu na liendelee kukazia umuhimu wa uaminifu, uadilifu, ukweli na uwazi; ili kukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mtakatifu Paulo VI alisema, mihimili ya Dola yaani: Bunge, Serikali na Mahakama iwe ni mahali pa kukuza na kudumisha: uhuru wa kweli, demokrasia shirikishi, haki jamii, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili. Serikali na Kanisa vishirikiane na kusaidiana katika kuwahudumia watu wa Mungu Barani Afrika, kwa kuheshimu dhamiri nyoofu, utu na heshima ya binadamu na kwamba, uongozi ukite mizizi yake katika huduma ya upendo, kanuni maadili na utu wema. Mihimili ya Dola iwe mstari wa mbele kudumisha amani, ambalo ni jina jipya la maendeleo duniani! Wanadiplomasia Barani Afrika walihamasishwa kukuza na kudumisha udugu wa ubinadamu, ili kukoleza misingi ya haki, amani na mshikamano. Kristo Yesu ni Mfalme wa kweli na uzima; utakatifu na neema; haki, amani na upendo Umoja na mshikamano ni nguzo msingi ya maendeleo, kumbe, kuna haja ya kuondokana na: ubaguzi, ukabila, udini na umajimbo usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa mustakabali wa familia ya Mungu Barani Afrika.

Mchakato wa haki, amani na upatanisho vipewe kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya maendeleo Barani Afrika. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene Barani Afrika. Vyama na mashirika ya kitume Barani Afrika yasaidie kukoleza imani na kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili. Waamini walei, wawe ni sauti ya wanyonge; waendelee kukuza na kudumisha: upendo, haki, uhuru na ukweli pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatumia kikamilifu karama na mapaji waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Ikumbukwe kwamba, wito na mwaliko wa utakatifu wa maisha ni kwa ajili ya watu wote wa Mungu pasi na ubaguzi. Mashahidi wa Uganda wawe ni mfano bora wa kuigwa! “Sanguis Martyrum semen est Christianorum” yaani “Damu ya Mashahidi wa imani ni mbegu ya Ukristo”.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa matashi mema kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anasema, anaungana nao kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wa SECAM Barani Afrika. Anawataka waendelee kujikita katika umisionari wa utume, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji, ili kweli Injili iweze kugusa medani mbali mbali za maisha ya watu!

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu katika ujumbe wake kwa SECAM anasema kwamba, kwa hakika SECAM imekuwa ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu kati ya waja wake Barani Afrika. Dhana ya Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibika Barani Afrika inapaswa kukuzwa na kuendelezwa. Huu ni wakati muafaka wa kurejea tena katika mambo msingi yaliyopewa kipaumbele na Mtakatifu Paulo VI alipotembelea kwa mara ya kwanza Barani Afrika kunako mwaka 1969. Utamadunisho wa tunu msingi za Kiinjili ni changamoto changamani inayopaswa kuvaliwa njuga Barani Afrika. Kanisa liendelee kufunda dhamiri nyoofu, kwa kuendelea pia kujipyaisha ili kuwa aminifu kwa Kristo Yesu!

SECAM Jubilei 50
23 July 2019, 13:51