Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake ni dira na mwongozo wa maisha ya mkristo katika ujunzi wa mahusiano na Mungu. Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake ni dira na mwongozo wa maisha ya mkristo katika ujunzi wa mahusiano na Mungu.  (ANSA)

Papa Francisko: Sala ya Bwana: Upya wake: Mahusiano na Mungu!

Sala ya Kristo Yesu inafumbatwa kwa namna ya pekee, katika mahusiano na mafungamano ya dhati kabisa na Mwenyezi Mungu, ambaye wanaweza kuthubutu kumwita “Baba Yetu”. Huu ndio upya wa Sala ya Kikristo, kielelezo cha majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa wale wanaopendana, wanaoheshimiana na kuthaminiana kwa kusikilizana na hatimaye, kujenga mshikamano wa dhati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sala kuu ya Bwana, maarufu kama Sala ya “Baba Yetu Uliye mbinguni” ni sala inayomwonesha mwamini uso wa upendo na huruma ya Mungu. Ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake na mwongozo thabiti wa maisha ya Mkristo. Sala hii ni muhimu sana katika maisha ya mkristo kama anavyofundisha na kushuhudia Yesu mwenyewe katika maisha yake. Katika mafundisho yake makuu, Yesu anawafundisha wanafunzi wake namna ya kusali vyema zaidi, huku wakimwelekea Mwenyezi Mungu, Baba mwenye huruma na mapendo. Baba Yetu ndio ufunguo wa Sala kuu aliyofundisha Yesu, inayoweza kupenya katika moyo wa Mwenyezi Mungu. Wakristo wanasali na kumwomba Mwenyezi Mungu ambaye ni Baba yao aliye mbinguni! Mungu ni asili na chemchemi ya maisha na kwamba, binadamu wote ni watoto wake wapendwa, wanaotamani kuona Ufalme wa Mungu ukisimikwa hapa duniani na mapenzi yake yakitendeka duniani kama mbinguni.

Huu ni mwelekeo wa maisha ya kiroho unaopaswa kufuatwa na waamini wote.  Sala kuu ya Baba yetu uliye mbinguni, kimsingi ni chemchemi ya matumaini ya Kikristo. Mwinjili Luka ndiye anayefafanua kwa kina na mapana, utume wa maisha ya Kristo Yesu katika Sala. Mitume walikuwa wanashangazwa na maisha ya Yesu ambaye daima kila siku asubuhi na jioni alijitenga na shughuli nyingine zote, akatumia muda wake kwa ajili ya sala yaani kuongea na kujiaminisha mikononi mwa Baba yake wa mbinguni! Wanafunzi baada ya kuona umuhimu wa sala katika maisha na utume wao, wakamwomba Yesu ili aweze kuwafundisha.  Sala ya Baba Yetu ni sala ya kikristo inayowawezesha waamini kumwita Mwenyezi Mungu, “Baba Yetu”. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamini hawana tena hofu na hivyo, wanaweza kuthubutu kumwita Mwenyezi Mungu “Aba!” yaani “Baba”.

Hii ni sala inayohitaji ujasiri kwani kwa neema ya Mwenyezi Mungu watu wote wameunganishwa kuwa waana kama ilivyofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu anayewawezesha kumwita Mwenyezi Mungu, “Baba”. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alikwisha fafanua Sala ya Bwana wakati wa Katekesi zake, lakini, Jumapili tarehe 28 Julai 2019 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alifanya tena tafakari ya kina kuhusu Sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni. Wanafunzi wa Yesu walizoea kusali kama kawaida, lakini waliguswa na upya wa sala kama ulivyoshuhudiwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Sala yake ilikuwa ni tofauti sana na sala walizokuwa wanasali walimu wengine wa nyakati zake. Sala ya Yesu ilionesha umoja na mshikamano wa dhati kabisa na Baba yake wa mbinguni katika hali ya unyenyekevu na utii mkubwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, siku moja baada ya Kristo Yesu kuhitimisha sala yake, wanafunzi wake wakamwomba ili awafundishe kusali zaidi.

Sala hii ya Kristo Yesu inafumbatwa kwa namna ya pekee, katika mahusiano na mafungamano ya dhati kabisa na Mwenyezi Mungu, ambaye wanaweza kuthubutu kumwita “Baba Yetu”. Huu ndio upya wa Sala ya Kikristo, kielelezo cha majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa wale wanaopendana, wanaoheshimiana na kuthaminiana kwa kusikilizana kwa makini na hatimaye, kujenga mshikamano wa dhati. Haya ni majadiliano kati ya Mwana na Baba; majadiliano ya kina kati ya waana na Baba yao wa mbinguni! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Sala ya Bwana  ni kati ya zawadi adhimu ambazo Kristo Yesu amewaachia wafuasi wake baada ya kukamilisha utume wake hapa ulimwenguni. Ni katika Sala ya Baba Yetu, Kristo Yesu anawafunulia wafuasi wake Fumbo la Mwana wa Baba wa milele, linalowagusa na kuwaambata kama ndugu na hivyo kushiriki katika Ubaba wa Mwenyezi Mungu kwa njia ya majadiliano pamoja na kujiaminisha kama waana wapendwa wa Mungu.

Waamini wanamwomba Mwenyezi Mungu Ufalme wake ambao umefunuliwa na Kristo Yesu ufike hapa ulimwenguni. Jina lake litukuzwe, awape mahitaji yao ya kila siku; awasamehe makosa yao na kuwaokoa kutoka dhambini. Baba Mtakatifu anasema, siri kubwa ya Sala ya Baba Yetu ni pale waamini wanapomwomba Mwenyezi Mungu, wao pia wawe tayari kutoa. Sala hii ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu yanayowataka waamini kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu. Si rahisi kuweza kusali vyema, kwani kuna wakati waamini wanapatwa na kishawishi cha kutaka kusimama mwanzoni kabisa mwa sala kwa kusema tu “Baba Yetu”. Lakini kuna haja ya kuwa wadumifu katika maisha ya sala, wakiendeleza ule udadisi wa kutaka kujua undani wa mambo kwa kusema kwa nini imekuwa hivi?

Lengo ni kutaka kupata uhakika na usalama wa maisha yao, kwa kuvutwa na uso wa huruma na mapendo kutoka kwa Baba yao. Waamini wawe na uthubutu wa kumuuliza Mwenyezi Mungu, kwa nini imekuwa hivi? Katika mashaka na mahangaiko ya ndani mintarafu maisha ya sala, daima waamini wakimbilie ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwaunganisha na Mwanaye Kristo Yesu pamoja na Baba wa Mbinguni, ili kuishi kikamilifu Habari Njema ya Wokovu chini ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu.

Papa: sala ya Bwana
29 July 2019, 09:47