Tafuta

Papa Francisko asema, huruma na upendo ni kipimo makini cha ujirani mwema: amana na utajiri kutoka katika Injili ya Luka! Mfano wa Msamaria mwema! Papa Francisko asema, huruma na upendo ni kipimo makini cha ujirani mwema: amana na utajiri kutoka katika Injili ya Luka! Mfano wa Msamaria mwema! 

Baba Mtakatifu Francisko: Huruma & Upendo: Kipimo cha ujirani mwema

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya huruma na upendo, na kwa njia ya Fumbo la Umwilisho ameamua kuwa karibu sana na binadamu, katika shida na mahangaiko yake ili aweze kumkomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni kwa njia hii, Amri ya Upendo kwa Mungu na Jirani inakuwa ni sheria msingi katika maisha ya kila mwamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Upendo kwa Mungu na jirani unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni kielelezo makini cha imani katika matendo. Na hii ni sehemu ya mchakato wa kuufikia utimilifu wa upendo ambao ni Mungu mwenyewe. Mfano wa Msamaria mwema ni kielelezo cha upendo unaojipambanua katika huduma ya kidugu, kielelezo cha Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu! Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, Injili inamwonesha Mwanasheria anayemuuliza Kristo Yesu jinsi ya kuurithi Ufalme wa Mungu na Yesu anamwongoza kwa kumwambia kwamba, majibu yote yanapatikana kutoka katika Maandiko Matakatifu. Yaani, huu ni  mwaliko kumpenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.

Hii ni tafsiri makini iliyotolewa na Kristo Yesu, ili kuzima kiu ya Mwanasheria, kwani kulikuwepo na tafsiri nyingi kuhusu jirani! Ndiyo maana Mwanasheria anachukua fursa tena kumuuliza Yesu, Je, jirani yangu ni nani? Na hapo Kristo Yesu anatumia fursa hii kufafanua kwa kina maana ya jirani, urithi na amana kubwa kutoka kwa Mwinjili Luka, ambayo kamwe haitafutika katika historia ya Kanisa, udugu wa kibindamu na utendaji wa Mkristo! Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 14 Julai 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mhusika mkuu katika tukio hili ni Msamaria ambaye katika kusafiri kwake alikutana na mtu mmoja aliyekuwa ameangukia kati ya wanyang’anyi, wakamvua nguo, wakamtia jeraha wakaenda zao.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Wayahudi walikuwa wanawadharau na kuwabeza sana Wasamaria, kiasi cha kujenga uadui kati yao. Wasamaria walihesabika kuwa ni “watu wa kuja tu” ambapo kamwe hawakuwa ni sehemu ya taifa teule la Mungu na wala wasingeweza “kupikika chungu kimoja” na Wayahudi. Kristo Yesu anaamua kumchukua Msamaria kuwa ni mfano bora wa kuigwa na anataka kuvunjilia mbali maamuzi mbele, ili kudhihirisha kwamba hata mgeni, yaani “Mtu wa kuja”, au “Kyasaka” au Mnyamahanga au hata yule anayedhaniwa kuwa ni Mpagani asiyefahamu hata mahali ambapo mlango wa Kanisa ulipo, anaweza kutenda mema na kuwa ni mfano bora wa kuigwa: kwa kusukumwa na dhamiri nyofu, huruma na upendo wa dhati unaomwilishwa katika huduma ya kidugu, na hivyo kuweza kutumia rasilimali mbali mbali zilizopo kadiri ya uwezo wake.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika njia ile ile kabla ya Msamaria kupitia mahali pale, alitangulia kupita Kuhani, na alipomwona alipitia kando. Hali kadhalika alipitia hapo Mlawi naye akapitia kando. Wote hawa walikuwa ni watu wa Ibada, wote walimwona, lakini hawakuthubutu kusimama na kumsaidia, pengine kwa kuogopa kunajisiwa kabla ya Ibada. Hii ilikuwa ni tafsiri ya sheria ya kibinadamu iliyokuwa imeambatanishwa na Amri kuu ya upendo, ambamo Mwenyezi Mungu anakazia kwanza kabisa huruma! Kristo Yesu anatoa mfano wa Msamaria mwema kama kielelezo makini cha upendo kwa Mungu na jirani, na wakati huo huo bado mwamini akaendelea kuwa kweli ni mchamungu akionesha utimilifu wa utu wake kama binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata leo hii, Kristo Yesu anaendelea kuwaswalisha wafuasi wake, Je, jirani yako ni nani?

Yesu katika jibu hili, analeta mwelekeo mpya kabisa kwa kukazia huruma inayomwilishwa katika upendo kama kigezo msingi cha kumtambua jirani. Huu ndio ufunguo makini wa kuweza kumtambua jirani yako kuwa ni nani? Angalisho kwa wale watu ambao hawana tena huruma na upendo katika nyoyo zao, hawataweza kugundua kuwa jirani zao ni nani? Watu wa namna hii, kimsingi wanaelemewa na ubinafsi pamoja na uchoyo. Huruma na upendo ni nguzo msingi wa mafundisho ya Kristo Yesu kwa waja wake kwani Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele kwa binadamu. Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na mahangaiko ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii! Hawa ndio kimsingi jirani zao! Waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, si wao wanaopaswa kuonesha vigezo vya ujirani, bali hali halisi ya mhitaji ndicho kigezo kikuu. Huruma ni ufunuo wa uso wa upendo wa kweli katika maisha ya mwanadamu.

Kwa njia hii, Wakristo watakuwa wafuasi wa kweli wa Yesu, ikiwa kama watakuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Waamini wanakumbushwa kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya huruma na upendo, na kwa njia ya Fumbo la Umwilisho ameamua kuwa karibu sana na binadamu, katika shida na mahangaiko yake ili aweze kumkomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni kwa njia hii, Amri ya Upendo kwa Mungu na Jirani inakuwa ni sheria msingi katika maisha ya kila mwamini. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumkimbilia Bikira Maria, ili aweze kuwasaidia kupata, kukua na kukomaa katika huruma na upendo, ambao unapaswa kumwilisha kwa Mungu na jirani. Haya ni mambo ambayo ni sawa na chanda na pete, kwani hayawezi kutenganishwa, bali yanategemeana na kukamilishana kama sehemu ya maisha ya mwanadamu!

Papa: Msamaria Mwema
14 July 2019, 09:42