Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya wakimbizi na wahamiaji nchini Libya asema, kamwe Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuvumilia vitendo kama hivi! Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya wakimbizi na wahamiaji nchini Libya asema, kamwe Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuvumilia vitendo kama hivi!  (AFP or licensors)

Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya wakimbizi nchini Libya!

Papa Francisko ameonesha masikitiko yake kutokana na shambulio la hivi karibuni dhidi ya Kituo cha Kizuizi cha Wakimbizi kilichoko huko Tripoli nchini Libya na kusababisha watu zaidi ya 100 kufariki dunia na watu wengine zaidi ya 130 kujeruhiwa vibaya na majengo kubomolewa. Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kukubaliana na vitendo vya kinyama kama hivi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 7 Julai 2019, ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na shambulio la hivi karibuni dhidi ya Kituo cha Kizuizi cha Wakimbizi kilichoko huko Tajoura nje kidogo ya mji wa Tripoli nchini Libya na kusababisha watu zaidi ya 100  kufariki dunia na watu wengine zaidi ya 130 kujeruhiwa vibaya na majengo kubomolewa. Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kukubaliana na vitendo vya kinyama kama hivi. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji waliopoteza maisha yao katika shambulio hili ambalo Umoja wa Mataifa umelitaja kuwa ni uhalifu wa kivita.

Baba Mtakatifu anawaombea majeruhi ili waweze kupata faraja na kupona haraka. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaweka sera na mikakati itakayoratibu wahamiaji wenye shida zaidi kupata hifadhi katika nchi mbali mbali. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia kuwakumbuka na kuwaombea watu waliopoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika huko Afghanistan, Mali, Burkina Faso na Niger. Baba Mtakatifu amewaongoza waamini na watu wote wenye mapenzi mema waliokuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kusali katika ukimya, ili kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji.

Kuna wakimbizi zaidi ya 3, 500 wanaopewa hifadhi kwenye vizuizi vya wakimbizi na wahamiaji nchini Libya. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antònio Guterres amezitaka pande zinazosigana nchini Libya kuhakikisha kwamba, zinalinda na kudumisha haki msingi za binadamu, kwa kuepuka mauaji ya raia pamoja na mashambulizi kwenye miundo mbinu. Wachunguzi wa mambo wanasema, kwa sasa Jumuiya ya Kimataifa imegawanyika kiasi hata cha kushindwa kuchukua maamuzi magumu ili kuokoa maisha ya raia wanaoendelea kushambuliwa kila kukicha. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anazitaka pande zinazoendelea kukinzana nchini Lybia kurejea tena kwenye meza ya majadiliano ya kisiasa.

Kumekuwepo na shutuma kwamba, Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Waziri mkuu Fayez Al-Sarajj imekuwa ikiwatumia wakimbizi na wahamiaji kulinda maghala ya silaha, kiasi cha kubeza uhai, haki, utu na heshima ya wakimbizi na wahamiaji hawa! Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeuomba Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi wa kina utakaobainisha wale waliohusika katika shambulio hili ambalo limelaaniwa na Jumuiya ya Kimataifa. Habari zaidi kutoka Tripoli, Lybia zinasema kwamba, wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanahifadhiwa kwenye Vituo vya Vizuizi vya Kambi za wakimbizi huko Tripoli wamehamishiwa sehemu nyingine, lakini bado kuna hofu kwamba, Tripoli inaweza tena kushambuliwa wakati wowote ule!

Papa: Libya

 

 

08 July 2019, 11:14