Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 agosti 2019 anatarajiwa kukutana na vijana wa Chama cha Skauti kutoka Barani Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 agosti 2019 anatarajiwa kukutana na vijana wa Chama cha Skauti kutoka Barani Ulaya. 

Papa Francisko kukutana na Skauti 5000 kutoka Barani Ulaya! Moto

Chama cha Skauti Barani Ulaya kuanzia tarehe 27 Julai hadi 3 Agosti, kitawakusanya wanachama wake 5000 wenye umri kati ya miaka 16 hadi 21 kutoka katika nchi 20, ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha vijana wa kizazi kipya. Tarehe 3 Agosti 2019, watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, kumbu kumbu ya miaka 25 tangu walipokutana na Mtakatifu Yohane Paulo II.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wazazi wana waamini walezi wa Skauti kwa sababu wanatambua wema, hekima na busara ya malezi ya kiskauti yanayojikita katika tunu msingi za maisha ya binadamu; mazingira, maisha ya kiroho na imani kwa Mwenyezi Mungu. Hizi ni mbinu zinazowafunda Maskauti kuwa kweli huru na kuwajibika barabara katika matendo yao; imani hii ya wazazi inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote, bila kulisahau Kanisa na kwamba, daima wanapaswa kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya Jumuiya kubwa ya Kikristo. “Katiba ya Ujasiri” ni kielelezo cha mambo msingi wanayoyakumbatia na matarajio yaliyomo mioyoni mwa vijana wa Skauti. Haya ni masuala ya elimu, usikivu makini unaopaswa kuoneshwa na viongozi wao bila kusahau mchango wa Parokia na Kanisa katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza wanachama wa Skauti kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu; mchakato ambao unapaswa kuwa ni endelevu kama sehemu ya malezi na majiundo makini ya vijana, ili waweze kuimwilisha Injili inayowaletea mabadiliko katika maisha. Baba Mtakatifu ameyasema haya hivi karibuni alipokutana na kuzungumza na vijana wa Chama cha Skauti kutoka Italia, AGESCI.  Anasema kwamba vyama vya kitume ndani ya Kanisa Katoliki vina nafasi ya pekee kabisa katika maisha yake kwani huu ni utajiri wa Kanisa ambao ni matunda ya Roho Mtakatifu, kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji katika medani mbali mbali za maisha. Chama cha Skauti Barani Ulaya kinaweza kuwa ni chachu ya Uinjilishaji kwa kudumisha madaraja ya majadiliano na jamii.

Dhamana hii inaweza kutekelezeka ikiwa kama Skauti itaendelea kushikamana na Parokia zao pamoja na kushiriki kikamilifu katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Kanisa mahalia, kwa kushirikiana kikamilifu na viongozi wa Kanisa katika ngazi mbali mbali. Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, muasisi wa Chama cha Skauti Bwana Baden Powell anakiri kwamba, dini ni sehemu muhimu sana ya vinasaba vya wanachama wa Skauti kwani ni sehemu ya maisha yao, kwa kutambua uwepo wa Mungu na huduma. Hiki ni chama ambacho kinaendelea kuwekeza zaidi katika masuala ya maisha ya kiroho kimataifa pamoja na kuhakikisha kwamba, wanachama wake wanapewa malezi ya imani; mambo ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga, kwa ajili ya mafao ya wanachama wa Skauti.

Ni katika muktadha huu, Chama cha Skauti Barani Ulaya kuanzia tarehe 27 Julai hadi 3 Agosti, 2019 kitawakusanya wanachama wake 5000 wenye umri kati ya miaka 16 hadi 21 kutoka katika nchi 20, ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha vijana wa kizazi kipya. Tarehe 3 Agosti 2019, watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, kumbu kumbu ya miaka 25 tangu walipokutana na Mtakatifu Yohane Paulo II. Lengo ni kukuza na kudumisha urafiki na udugu wa kibinadamu, utakaowasaidia kutambua urithi, amana na utajiri wao wa kitamaduni na maisha ya kiroho, ili hatimaye, waweze kujenga ndani mwao ari na moyo wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Skauti wanatambua kwamba, Kristo Yesu ni dira na mwongo wao wa maisha!

Mkutano huu wa Skauti Barani Ulaya utaadhimishwa katika sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza ni kutembelea mkoa wa Umbria, chemchemi ya watakatifu wengi kutoka Italia. Baadaye, watakusanyika na hatimaye, kuanza kuelekea mjini Vatican, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wakati wote huu, watakuwa wanaongozwa na tafakari ya Neno la Mungu, maisha ya Kisakramenti pamoja na tafakari zitakazokuwa zinatolewa. Kwa hakika, vijana watapata muda wa kufurahia maisha ya pamoja sanjari na kuendelea kujifunza kutunza mazingira nyumba ya wote. Mkutano wa Skauti Barani Ulaya utahitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakaoongozwa na Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE.

Papa: Skauti
19 July 2019, 15:53