Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika mkutano wake na vijana na familia amekazia umuhimu wa kulinda na kudumisha haki msingi za watoto; vijana wajenge utamaduni wa wa kukutana na wengine! Papa Francisko katika mkutano wake na vijana na familia amekazia umuhimu wa kulinda na kudumisha haki msingi za watoto; vijana wajenge utamaduni wa wa kukutana na wengine!  (Vatican Media)

Hija ya Kitume Romania: Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia

Baba Mtakatifu Francisko katika mkutano wake na vijana na familia amekazia: Umuhimu wa watoto kupewa haki zao msingi na kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi. Pentekoste mpya iwawezeshe kutembea kwa pamoja katika huduma na sala. Waamini watambue:Iimani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha ushuhuda wa maisha ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 1 Juni 2019 amekutana na kuzungumza na vijana pamoja na familia kutoka Ias, huko Romania, akasikiliza kwa makini shuhuda zao na hatimaye, akatoa tafakari yake iliyokita mizizi katika mambo makuu yafuatayo: Umuhimu wa watoto kupewa haki zao msingi na kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi. Pentekoste mpya iwawezeshe kutembea kwa pamoja katika huduma na sala. Waamini watambue kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha ushuhuda wa maisha ya Kikristo!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuimarisha mizizi na utambulisho wao wa Kikristo bila kuyumbishwa hata kidogo! Vijana wathubutu kujenga utamaduni wa kukutana na kushirikishana ndoto zao za maisha na kwamba, Wakristo wote wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia! Baba Mtakatifu amewapongeza watoto waliohudhuria kwa wingi katika mkutano huu na kuwataka waamini kusali na kuwaombea ili Bikira Maria aweze kuwalinda na kuwapatia tunza yake ya kimama. Watoto hawa wapewe haki zao msingi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanakuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi.

Mkutano huu umekuwa ni kielelezo cha Uso wa familia ya Mungu unaoundwa na watoto, vijana na wazee kutoka katika mataifa mbali mbali; watu wenye lugha, tamaduni, mapokeo na imani tofauti, kwa pamoja wamekutanika ili kugundua ule uzuri wa kutembea pamoja kama ndugu, kama ile furaha walionesha Bikira Maria na Elizabeti walipokutana. Inafurahisha sana kuona wazazi wakiwa wameungana na kuambatana na watoto wao katika sala na maadhimisho mbali mbali ya mafumbo ya Kanisa! Hili ni jambo la kufurahisha na kumshukuru Mungu, mfano bora wa kuigwa na waamini sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu amesema kwamba, mkutano huu ni kielelezo cha Pentekoste mpya, inayowakirimia waamini nguvu ya kugundua karama na mapaji ya Roho Mtakatifu ndani mwao, tayari kuyatolea ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, kwa kutembea kwa pamoja.

Waamini wawe ni wajenzi na vyombo vya umoja na mshikamano; waendelee kutembea kwa pamoja wakihudumia na kusali; wakiota na kutekeleza ndoto zao katika uhalisia wa maisha yanayokita mizizi yake katika amana na urithi wa maisha ya kiroho na kiutu! Watoto na vijana wakuze na kudumisha tunu msingi walizojifunza kutoka katika familia zao; waimarishe na kushuhudia amana na urithi wa imani waliorithishwa ndani ya familia; wawe na ujasiri na ukarimu wa kuweza kuwashukuru wazazi wao waliowarithisha imani, ili hata wao waweze kuchangia katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Waamini wakumbuke kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kumwilishwa katika matendo kama ushuhuda wa huruma na upendo wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake.

Waamini watambue na kudumisha: historia na utambulisho wao unaowaunganisha na kuwawezesha kuwa wamoja katika Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Vijana wajenge mtandao wa udugu wa upendo, ili waweze kung’aa kama nyota za usiku, daima wakitambua tunu msingi za maisha ya familia, urithi unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa na wote! Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwisho wa dunia ni pale ambapo, upendo wa Kikristo utatoweka kama ndoto ya mchana na Mwenyezi Mungu kusukumiziwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hapa wazee watashindwa kuwa na ndoto na vijana watakosa utabiri, mambo msingi katika malezi, makuzi na ukomavu wa vijana wa kizazi kipya! Ikumbukwe kwamba, Mungu ni upendo!

Baba Mtakatifu anatambua fika changamoto na matatizo ya maisha ya Kijumuiya, lakini kisiwe ni kisingizio cha kutaka kujenga utamaduni wa uchoyo, ubinafsi na hali ya kutaka kujitafuta wenyewe. Mwenyezi Mungu amemkirimia kila mtu wito na karama zinazopaswa kutumiwa kwa uhuru kamili, ili kuvunjilia mbali kuta za utengano, ili kutengeneza njia inayojenga na kudumisha utambulisho wa wana wa Mungu unaofumbatwa katika udugu wa kibinadamu! Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza vijana kutoka ndani na nje ya Romania na hasa kwa namna ya pekee katika mji huu wa Ias ambao unajulikana kama Makao makuu ya vijana wa Romania.

Huu ni mji unaosimikwa katika ukarimu kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, tayari kutembea kwa pamoja, ili kutekeleza ile ndoto ya wahenga na unabii wa vijana, ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi. Vijana ni mahujaji wa karne ya ishirini na moja, wenye uwezo wa kujenga mshikamano na mafungamano ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani katika matendo; kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza, ili kudumisha amani na maridhiano kati ya watu! Wawe ni wajenzi na mashuhuda wa umoja na mafungamano ya kijamii; amani ipewe kipaumbele cha kwanza; ukweli usimamiwe na kudumishwa na kwamba, watu wote wajisikie kuwa ni sehemu ya familia ya Mungu.

Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Wazazi na walezi wanafurahia kuona mafanikio ya watoto wao. Mwishoni mwa tafakari yake anasema Baba Mtakatifu Francisko,  kwa hakika, Romania ni Bustani ya Bikira Maria Mama wa Mungu, hali ambayo imejidhihirisha katika mkutano kati ya Baba Mtakatifu, vijana na familia kutoka ndani na  nje ya Romania. Bikira Maria ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani, anayewalinda na kuwatunza watoto wake. Bikira Maria ni matumaini ya familia na Kanisa katika ujumla wake.

Papa: Watoto

 

02 June 2019, 15:00