Tafuta

Altare inaonesha: Sadaka na Meza ya Bwana. Alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara inayotolewa kwa ajili ya upatanisho! Altare inaonesha: Sadaka na Meza ya Bwana. Alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara inayotolewa kwa ajili ya upatanisho! 

Papa Francisko: Maana ya Altare katika Liturujia ya Kanisa!

Altare inaonesha: sadaka na meza ya Bwana; ni alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara iliyotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kristo alijisadakaa ili kumkomboa mwanadamu kutoka dhambini. Altare ni sura ya mwili wa Kristo anasema Mtakatifu Ambrosi na kwamba, mwili wa Kristo uko juu ya Altare.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya Liturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji! Hii ndiyo tabia ya Liturujia na kwa sababu ya Sakramenti ya Ubatizo, ni haki na wajibu wa waamini ambao kimsingi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki wa Mungu. Liturujia ni chemchemi ya roho ya kweli ya kikristo. Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumtangaza  na kumshuhudia Kristo. Lengo ni umoja na mshikamano wa watoto wa Kanisa. Liturujia ni muhimu kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa kwa njia ya Kristo Yesu. Liturujia ni utekelezaji wa kazi ya Kikuhani ya Kristo Yesu.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Liturujia, Ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa Fumbo wa Kristo Yesu, yaani Kanisa. Hili ni tendo takatifu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, lengo kuu la Liturujia ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa! Ibada ya Misa Takatifu ni kumbukumbu ya sadaka ambamo hudumishwa sadaka ya Msalaba, na karamu takatifu ya umoja katika Mwili na Damu ya Bwana. Lakini adhimisho la Sadaka ya Ekaristi Takatifu huelekezwa kwenye umoja wa ndani wa waamini na Kristo kwa njia ya komunyo. Kukomunika ni kumpokea Kristo mwenyewe aliyejitoa sadaka kwa ajili ya waja wake.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafafanua kwamba, Altare, ambayo Kanisa lililounganika katika kusanyiko huizunguka katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, yanaonesha mambo mawili ya fumbo moja. Altare inaonesha: sadaka na meza ya Bwana. Altare ni alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara iliyotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kristo alijitoa kwa ajili ya ukombozi wa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Altare ni sura ya mwili wa Kristo anasema Mtakatifu Ambrosi na kwamba, mwili wa Kristo uko juu ya Altare. Kumbe, Kanisa linafundisha kuhusu umoja kamili kati ya Sadaka na Altare.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walileta mageuzi makubwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kuonesha umuhimu wa kuzunguka Altare katika maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa. Altare ni tema iliyochaguliwa tangu mwaka 2003 kuongoza kongamano la Liturujia Kitaifa nchini Italia. Maana na ufahamu wa Altare ni kati ya mambo msingi yanayoendelea kufanyiwa utafiti kama sehemu muhimu sana ya malezi na majiundo ya waamini katika Liturujia ya Kanisa. Wahandisi na wajenzi wa Makanisa mapya watambue umuhimu wa Altare katika mazingira ya Liturujia. Altare inapaswa kujengwa ikiwa imetenganishwa na ukuta, ili kutoa nafasi kwa wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa kuweza kuizunguka. Altare ijengwe mahali ambapo panaonesha ukuu na umuhimu wa Altare katika Ibada.

Kongamano la Kumi na Saba (XVII) la Liturujia Kitaifa nchini Italia limefunguliwa tarehe 30 Mei huko kwenye Monasteri ya Bose na kuhitimishwa tarehe 1 Juni 2019. Mada zilizojadiliwa ni pamoja na: mabadiliko ya Altare kutoka katika Altare zilizotengenezwa kwa mbao hadi Altare zilizochongwa kwa mawe; chimbuko la Altare ya Kikristo; historia ya mgawanyo wa nafasi katika maadhimisho ya Kiliturujia; Mapokeo na umuhimu wa kusoma alama za nyakati katika ujenzi wa Altare; pamoja na Taalimungu ya Altare. Tema nyingine ni Mimbari kwa Kiswahili, "Marufaa" kwa Kiarabu, "Ambo", kwa Lugha ya Kilatini, ni mahali pa kutangazia Neno la Mungu.

Umuhimu wa wahandisi kujadiliana na wanataalimungu katika ujenzi wa Altare, mahali pa kukaa watu wa Mungu na mahali pa kujenga Kisima cha Ubatizo! Sanaa na Liturujia ni mada ambayo pia imejadiliwa. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa, katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Fra Enzo Bianchi, Muasisi wa Monasteri ya Bose, amewatakia heri na baraka. Anasema, tafakari ya Kongamano hili isaidie kukuza na kudumisha uelewa wa Liturujia kama hatima ya maisha ya Kanisa, umoja na udugu, kwa sababu Liturujia inawafunda watu kuhusu utajiri wa Neno la Mungu.

Kongamano hili liliandaliwa kwa ushirikiano wa Monasteri ya Bose na Idara ya Miundombinu ya Kikanisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Kauli mbiu ya kongamano hili ni “Altare, Uvumbuzi wa hivi karibuni na matatizo mapya”. Mwishoni mwa ujumbe huu, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia washiriki wote baraka zake za kitume!

Papa: Altare
05 June 2019, 09:02