Tafuta

Papa Francisko katika hija yake ya kichungaji Jimbo kuu la Camerino ameonesha wasi wasi kuhusu mvutano uliopo kwenye Ghuba ya Uajemi na kuwataka wadau kujikita haki majadiliano na amani. Papa Francisko katika hija yake ya kichungaji Jimbo kuu la Camerino ameonesha wasi wasi kuhusu mvutano uliopo kwenye Ghuba ya Uajemi na kuwataka wadau kujikita haki majadiliano na amani. 

Papa Francisko: Camerino: Wasi wasi watanda Ghuba ya Uajemi!

Baba Mtakatifu anaendelea kufuatilia kwa umakini kubwa kutokana na kuongezeka kwa mvutano huko Ghuba ya Uajemi. Papa anawaalika wahusika wote kutumia kidiplomasia, ili kufikia suluhu ya kweli katika mgogoro huu ambao unaweza kukuza vita huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano, haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumamosi tarehe 15 Juni 2019 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Edvige Carboni kuwa Mwenyeheri. Ibada hii imeadhimishwa huko Pozzomaggiore, Kisiwani Sardegna, Kusini mwa Italia. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 16 Juni 2019 huko Camerino, amemkumbuka Mwenyeheri Edvige Carboni, mwanamke mnyenyekevu, aliyekumbatia Fumbo la Msalaba na kushuhudia imani, kiasi cha kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kwa jirani zake.

Katika Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Kimataifa kwa Mwaka 2019, Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji kwa kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa mshikamano. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Jumuiya za Kanisa na kiraia, zijitahidi kuonesha ukaribu wao, kwa kusikiliza na kujibu kilio chao! Baba Mtakatifu amesema, anaendelea kufuatilia kwa umakini na hofu kubwa kutokana na kuongezeka kwa mvutano huko Ghuba ya Uajemi. Baba Mtakatifu anawaalika wahusika wote kuhakikisha kwamba, wanatumia nyenzo za kidiplomasia, ili kufikia suluhu ya kweli katika mgogoro huu ambao unaweza kukuza vita na kinzani huko Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano, haki na amani katika ukweli na uwazi! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwasilimia wale wote walioshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu hapo Camerino. Amewakumbuka na kuwasalimia wagonjwa, wazee, wafungwa na wale wote waliokuwa wanafuatilia hija hii ya kichungaji kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wote waliojisadaka ili kufanikisha hija hii ya kichungaji katika Jimbo kuu la Camerino-Sanseverino Marche. Amewasalimia watu wote wa Mungu walioathirika kutokana na tetemeko la ardhi na kwamba, akiwa angani katika maeneo yao, amewakumbuka na kuwaombea!

Papa: Ghuba Uajemi
16 June 2019, 15:58