Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kusimama kidete kutangaza na kushuhudia furaha ya ukweli unaobububujika kutoka kwa Kristo Mfufuka! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kusimama kidete kutangaza na kushuhudia furaha ya ukweli unaobububujika kutoka kwa Kristo Mfufuka!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Waamini iweni mashuhuda wa furaha ya ukweli!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Katiba ya Kitume: “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” ni mwongozo unaovihusu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayowagusa na kuwaambata watu wa Mungu, katika mwelekeo mzima wa utekelezaji wa utume wa uinjilishaji mpya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 21 Juni 2019 anashiriki katika kongamano la kitaalimungu, huko Napoli, baada ya kuchapishwa kwa Katiba ya Kitume: “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” iliyohidhinishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Desemba 2017, na kuchapishwa rasmi tarehe 29 Januari 2018. Kongamano hili limeandaliwa na Kitivo cha Taalimungu, Chuo Kikuu cha Kusini mwa Italia, Kitengo cha San Luigi. Kati ya mada zinazochambuliwa ni pamoja na: Umuhimu wa kusoma alama za nyakati; changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; mwingiliano wa tamaduni; muktadha wa majadiliano kwenye Ukanda wa Bahari ya Mediterrania!

Mada nyingine ni Taalimungu; sanaa kama mahali pa tamaduni kukutana na kujadiliana; majadiliano ya kidini; mang’amuzi kama mbinu mkakati wa kukabiliana na kinzani za kale; shuhuda na mapendekezo. Baba Mtakatifu Francisko, atahitimisha kongamano hili kwa kudadavua “Taalimungu baada ya Katiba ya Kitume: “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” kadiri ya Mazingira ya Mediterrania. Katiba ya Kitume: “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” ni mwongozo makini unaovihusu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayowagusa na kuwaambata watu wa Mungu, katika mwelekeo mzima wa utekelezaji wa utume wa uinjilishaji mpya.

Hii ni dhamana inayojikita katika mang’amuzi, wongofu na mageuzi ya dhati yanayopania kupyaisha mfumo mzima wa elimu inayotolewa na Mama Kanisa, katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu. Katiba hii ni mwongozo na mbinu mkakati katika mageuzi ya elimu inayopania kumpatia mwanadamu furaha ya ukweli katika maisha yake. Hii ni “Furaha ya ukweli” unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu ambaye ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu; ni njia, ukweli na uzima. Ni kiungo muhimu cha umoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na umoja kati ya watoto wa Mungu, kwani Roho Mtakatifu ni: Roho wa ukweli na upendo; uhuru, haki na umoja.

Uinjilishaji na utamadunisho ni chanda na pete katika maisha na utume wa Kanisa unaojikita pia katika majadiliano na tamaduni mbali mbali kwa kusoma alama za nyakati, ili kuliwezesha Kanisa kujipyaisha zaidi kama walivyokazia Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao wa “Optatam totius” yaani “Mwongozo wa Malezi ya Kipadre” kwa kuzingatia uhamasishaji wa miito na majiundo makini ya Mapadre, ili kuwawezesha kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa, kwa kumfuasa Kristo Mchungaji mwema anayewapatia: utambulisho, tasaufi na utume wanaopaswa kuutekeleza katika mwanga wa “Furaha ya ukweli”.

Papa: Furaha ya Ukweli
20 June 2019, 11:53