Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, Vatican itaendelea kushirikiana na FAO katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini duniani! Papa Francisko asema, Vatican itaendelea kushirikiana na FAO katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini duniani! 

Vatican na FAO kushirikiana kupiga vita njaa & Umaskini duniani!

Mapambano dhidi ya baa la njaa na ukosefu wa maji safi na salama hayana budi kuzama zaidi ili kubainisha chanzo kikuu cha matatizo haya ambacho kimsingi ni ukosefu wa huruma na kutoguswa na mahangaiko ya watu pamoja na wanasiasa kutoheshimu, kuzingatia na kutekeleza mikataba iliyotiwa sahihi kimataifa! Vatican na FAO wataendelea kushirikiana dhidi ya njaa na umaskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 27 Juni 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano wa 41 wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO na kumshukuru kwa namna ya pekee Profesa Josè Graziano da Silva ambaye anamaliza muda wake kama Mkurugenzi mkuu wa FAO na kumkaribisha Bwana Qu Dongyu, kutoka China ambaye amechaguliwa hivi karibuni kuwa Mkurugenzi mpya wa FAO. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Vatican na FAO wataendelea kushirikiana ili kutokomeza umaskini duniani pamoja na kukomesha baa la njaa na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani, ifikapo mwaka 2030.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mchakato wa kukomesha baa la njaa kwa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani ni changamoto pevu, ingawa kumekuwepo na  mafanikio makubwa katika miaka ya hivi karibuni. Mapambano dhidi ya baa la njaa na ukosefu wa maji safi na salama hayana budi kuzama ndani kabisa ili kubainisha chanzo kikuu cha matatizo haya ambacho kimsingi ni ukosefu wa huruma na kutoguswa na mahangaiko ya watu pamoja na wanasiasa kutoheshimu, kuzingatia na kutekeleza mikataba iliyotiwa sahihi kimataifa! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula pamoja na ukosefu wa maji safi na salama ni tatizo na changamoto ya watu wote wa Mungu, inayopaswa kuchukuliwa kama sehemu ya uwajibikaji wa jumla.

Lengo ni kuwakomboa watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa na ukosefu wa maji safi na salama duniani! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, kwa kuendelea kuishi na kuona kwamba, haki zao msingi zinaheshimiwa na kuthaminiwa na wote! Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na matumizi bora zaidi ya chakula na maji, kwa kuondokana na utupaji ovyo wa chakula pamoja na uchafuzi wa maji sehemu mbali mbali za dunia. Uwajibikaji wa kijamii ni mchakato mkubwa wa uwekezaji katika kipindi cha muda mfupi na mrefu. Ushuhuda wa urithi huu utaendelezwa na vijana wa kizazi kipya na kwamba,  uharibifu wa mazingira ni maafa ambayo kamwe hayawezi kukubalika tena!

Baba Mtakatifu anasema, kuna uhusiano mkubwa kati ya athari za mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usalama wa chakula duniani pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Haya ni matatizo yanayoathiri familia ya binadamu katika ujumla wake. Ni kutokana na muktadha huu,  maendeleo ya sekta ya kilimo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee, kwa kuimarisha sera na mikakati ya kilimo bora sanjari na utunzaji wa ardhi. Maboresho haya hayana budi kwenda sanjari na maendeleo ya teknolojia pamoja na sera na mikakati inayofumbatwa katika mshikamano. FAO na Mashirika ya Kimataifa ni watendaji wakuu wanaopaswa kuchukua hatua madhubuti ili maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanapata mahitaji yao msingi!

Mashirika ya Kimataifa hayana budi kuungwa mkono na serikali pamoja na wadau mbali mbali, ili kufikia Malengo yaliyobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa, pamoja na kukuza uwajibikaji wa watu katika nchi, jumuiya na hatimaye, katika maisha. Vatican itaendelea kuunga mkono juhudi za FAO katika mapambano dhidi ya  baala njaa duniani, ili kuhakikisha kwamba, watu wanakuwa na maisha bora zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni!

Papa: FAO
27 June 2019, 16:06