Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu msaidizi Antoine Hèrouard kuwa msimamizi wa kitume wa Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes: Lengo ni kuimarisha huduma ya kiroho! Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu msaidizi Antoine Hèrouard kuwa msimamizi wa kitume wa Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes: Lengo ni kuimarisha huduma ya kiroho!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Lourdes: Huduma ya kiroho kwa mahujaji ni muhimu

Uteuzi wa Askofu msaidizi Antoine Hèrouard kuwa msimamizi wa kitume: Lengo ni kuendelea kuboresha huduma ya shughuli za kichungaji na maisha ya kiroho kwa mahujaji wanaotembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes. Udhibiti wa shughuli za kiuchumi na fedha ni muhimu, lakini kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa ajili ya maisha ya kiroho, amani na urithi wa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya. Ni mahali pa kuonjeshana upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa na kuthaminiwa. Madhabahu kimsingi ni mahali pa: Sala na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayetoa machozi ya faraja kwa wale wanaoteseka; ni mwombezi wa watu waliokata tamaa na kwamba, Mama huyu anajaribu kujibu sala ya kila mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza yake ya daima.

Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: neema na rehema pamoja na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani! Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, katika madhabahu, kamwe hawatakosekana Wamisionari wa huruma, mashuhuda wa upendo wa Mungu unaokoa na kuponya! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Msaidizi Antoine Hèrouard wa Jimbo Katoliki la Lille kuwa mjumbe wa Kitume wa huduma kwa mahujaji wanaohiji kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, Ufaransa. Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya. Askofu Msaidizi Antoine Hèrouard atawajibika moja kwa moja kwa Vatican katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kisheria.

Uamuzi huu wa Baba Mtakatifu unaendelea kuimarisha maamuzi aliyoyatoa kunako mwaka 2017, anasema Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika makala yake kuhusiana na maamuzi ya Madhabahu ya Bikira Maria wa Medjugorje, kuwa hizi ni sehemu ambazo zinapaswa kuwa ni chemchemi ya sala na shuhuda za Kikristo ili kuzima kiu ya mahitaji ya watu wa Mungu: kiroho na kimwili. Itakumbukwa kwamba, miaka miwili iliyopita, Baba Mtakatifu Francisko alilikabidhi dhamana ya kuratibu shughuli za kichungaji kwenye Madhabahu ya Kimataifa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya.

Baba Mtakatifu katika barua yake kwa Askofu Msaidizi Antoine Hèrouard wa Jimbo Katoliki la Lille anasema, kutokana na uchunguzi wa kina na mapana uliofanywa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, imeonekana kwamba, kuna hitaji la msingi la kuwa na  mwakilishi wa kitume atakayesaidia kuratibu shughuli za kichungaji katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, Ufaransa. Jimbo Katoliki la Tarbes na Lourdes litaendelea kuwa chini ya Askofu Nicolas Jean Renè Brouwet. Lengo ni kuendelea kuboresha huduma ya shughuli za kichungaji na maisha ya kiroho kwa mahujaji wanaotembelea Madhabahuni hapo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, udhibiti wa shughuli za kiuchumi na fedha ni muhimu, lakini kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa ajili ya maisha ya kiroho! Amana na urithi wa imani unapaswa kumwilishwa na kutamadunishwa, ili uweze kusonga mbele. Baba Mtakatifu anahitimisha kwa kusema, utajiri na nguvu ya Roho Mtakatifu inashuhudiwa katika ibada maarufu zinazodumishwa na watu wa kawaida. Hija ya pamoja kuelekea kwenye madhabahu pamoja na ushiriki mkamilifu katika matukio ya kiibada, kwa kuambatana na watoto pamoja kuwakaribisha jirani ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji na ushuhuda nguvu ya kimisionari!

Papa: Lourdes
07 June 2019, 11:19