Tafuta

Vatican News
Sherehe ya pentekoste imekuwa ni fursa ya kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao! Sherehe ya pentekoste imekuwa ni fursa ya kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao!  (Vatican Media )

Sherehe ya Pentekoste 2019: Roho Mtakatifu awafariji wanaoteswa!

Katika Sala za Waamini, Kanisa amemwomba Mwenyezi Mungu kulipyaisha Kanisa ili liweze kufanana na Kristo Yesu, Mchumba wake mwaminifu, katika utii na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Mwenyezi Mungu apende kumtuma Roho Mtakatifu ili aumbe upya sura ya dunia, watu waishi katika misingi ya haki na amani na kamwe asiwepo mtu anayedharirishwa wala kutelekezwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Sherehe ya Pentekoste, Kanisa limeadhimisha siku ya kuzaliwa kwake, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, wakatoka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ari na moyo mkuu pasi na woga wala makunyanzi. Ni Siku ya Waamini Walei Duniani. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 9 Juni 2019 ameadhimisha Sherehe ya Pentekoste kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Sherehe ya Pentekoste inafunga shamrashamra za Kipindi cha Pasaka kwa kukazia mambo yafuatayo: Roho Mtakatifu, Nafsi ya tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, aliwawezesha wafuasi wa Kristo kuwa na amani na utulivu wa ndani, tayari kujisadaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia!

Amani na utulivu ni zawadi ya Roho Mtakatifu hata katika ulimwengu mamboleo. Amani ya Roho Mtakatifu inabubujika kutoka kwa Kristo Yesu na wala hakuna sababu ya kurejea tena katika hofu, mashaka na woga kama ilivyokuwa kwa Mitume kabla ya kushukiwa na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni chemchemi ya karama, zawadi na mapaji mbali mbali, changamoto na mwaliko wa kuvuka kinzani na mipasuko inayoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, kwa kutenda mema, badala ya kulipiza kwa maovu; kwa kukaa kimya, badala ya kupiga makelele na hatimaye ni kwa njia ya sala na kufunga!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa, familia ya Mungu inalo jukumu la kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayomwilishwa katika huduma ya upendo na mshikamano kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Roho Mtakatifu anaweza kutengeneza makazi yake, mahali ambapo anapendwa na kukaribishwa. Waamini wanahamasishwa kuomba mapaji ya Roho Mtakatifu, ili kuwajengea amani na utulivu; kuwaondolea woga na hofu na hatimaye, ile tabia ya ubinafsi, tayari kujisadaka kwa ajili ya Mungu, Kanisa na jirani. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Kanisa litaendelea kupyaishwa kila siku katika maisha na utume wake! Roho Mtakatifu awawezeshe waamini kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa amani, wema na utume wa matumaini kwa wale waliokata tamaa!

Katika Sala za Waamini, Mama Kanisa amemwomba Mwenyezi Mungu kulipyaisha Kanisa ili liweze kufanana na Kristo Yesu, Mchumba wake mwaminifu, katika utii na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Mwenyezi Mungu apende kumtuma Roho wake Mtakatifu ili aweze kuiumba upya sura ya dunia, ili watu waweze kuishi katika misingi ya haki na amani na kamwe asiwepo mtu anayedharirishwa wala kutelekezwa. Katika lugha ya Kiswahili, lililotolewa Sr. Veronica Silvester Buganga wa Shirika la Wakarmeli, Kanisa limemwomba, Baba mwema, ili aweze kuwafariji kwa Roho Mtakatifu, Wakristo wanaoteswa, kwa kuungana na mateso ya Yesu; waonje furaha ya ushindi dhidi ya chuki na waweze kupokelewa na Mwenyezi Mungu katika muungano kamili!

Roho Mtakatifu asaidie kupyaisha nyoyo za waamini vijana, ili waweze kujenga mahusiano ya dhati na Kristo Yesu, bila ya kuwa na woga wa kujisadaka kwa ajili ya wito na maisha ya Kipadre. Roho Mtakatifu Mfariji agange na kuponya madonda ya waamini wengi, wanaojikuta wakiwa hawana tena matumaini katika Fumbo la Pasaka ya Kristo!

Papa Pentekoste
10 June 2019, 15:49