Tafuta

Vatican News
Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Papa Francisko awataka waamini kujenga na kudumisha moyo wa ibada na uchaji wa Mungu wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Papa Francisko awataka waamini kujenga na kudumisha moyo wa ibada na uchaji wa Mungu wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.  (ANSA)

Papa: Sherehe za Ekaristi Takatifu: Moyo wa Ibada & Uchaji wa Mungu

Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni mwaliko wa kufurahia uwepo endelevu wa Kristo Yesu, ambaye ni Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumpokea Kristo kwa moyo wa shukrani, kwa kuondokana na ukakasi wa moyo na mazoea, ili kupyaisha ile “Amina” yao wanapopokea Ekaristi kwa sababu ni kiini cha: umoja, upendo, sadaka, utakatifu na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 23 Juni 2019 amesema kwamba, Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, ameadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu yaani: Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu, maarufu kama “Corpus Domini” kwa lugha ya Kilatini! Mwinjili Luka, katika Sherehe ya Ekaristi Takatifu anaweka mbele ya macho ya waamini ule muujiza uliotendwa na Kristo Yesu, kwa kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili. Kabla ya muujiza huu, Mitume walimwendea Yesu na kumwomba auage mkutano ili waende katika vijiji na mashamba ya kando kando wapate mahali pa kulala na vyakula!

Lakini, Yesu akawaambia “Wapeni ninyi chakula”. Hata Mitume walikuwa wamechoka na kwa majibu haya walionekana pengine kukasirika kutokana na umati mkubwa uliokuwa mbele yao! Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, huu ni mwaliko kwa Mitume wa Yesu kuanza mchakato wa wongofu wa ndani, kutokana katika tabia ya kujifirikia binafsi na kuanza kutembelea katika hija ya mshikamano wa upendo, kwa kugawana na kushirikishana hata kile kidogo ambacho Mwenyezi Mungu anawawekea mbele yao! Na hapo Yesu ndipo anapotenda muujiza kwa kuitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie makutano; wote wakala, wakashiba na kusaza vikapu kumi na viwili.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, muujiza huu ni muhimu sana, kiasi kwamba, umesimuliwa na Wainjili wote kuonesha na kushuhudia nguvu ya Masiha, huruma na upendo wake kwa watu wanaoteseka! Muujiza huu ni kati ya miujiza mikubwa iliyotendwa na Kristo Yesu, ambao pia ni Kumbu kumbu endelevu ya Sadaka yake, yaani Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu! Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa maisha na utume wa Kristo Yesu, kielelezo makini cha upendo kwa Mungu na ndugu zake. Kama ilivyokuwa wakati alipokuwa anaweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, alimtolea Baba yake wa mbinguni Sala ya Baraka, akaumega mkate na kuwapatia wafuasi wake; vivyo hivyo akafanya pia kwa Divai.

Yote haya yalitendeka siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, akataka kuwaachia wafuasi wake Kumbu kumbu la Agano Jipya na la milele; Kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Sherehe ya  Fumbo la Ekaristi Takatifu inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka, ni mwaliko wa kufurahia uwepo endelevu wa Kristo Yesu, ambaye ni Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumpokea Kristo kwa moyo wa shukrani, kwa kuondokana na ukakasi wa moyo na mazoea, ili kupyaisha ile “Amina” yao wanapopokea Mwili wa Kristo, kwa sababu ni kiini cha upendo wake unaogeuza maisha ya mwamini kuwa sadaka safi na takatifu kwa Mwenyezi Mungu na mafao kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao hapa duniani!

Baba Mtakatifu anasema amina hii inapaswa kububujika kutoka katika undani wa maisha yao, kwani Kristo Yesu anawakirimia nguvu ya kuendelea kuishi kwani Kristo Yesu anaishi. Waamini wajenge moyo wa ibada na uchaji wa Mungu wanapokwenda kupokea Ekaristi Takatifu, iwe kana kwamba, hii ni mara yao ya kwanza kupokea Ekaristi! Maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanafuatiwa mara nyingi kwa maandamano makubwa, ambayo waamini wote wanahamasishwa kushiriki: kiroho na kimwili, kwa kutumia njia mbali mbali za mawasiliano. Bikira Maria awasaidie waamini kumfuasa Kristo Yesu kwa imani na upendo mkuu, ili hatimaye, waweze kumwabudu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu!

Corpus Domini

 

23 June 2019, 16:41