Tafuta

Vatican News
Papa Francisko kuhusu ufuasi wa Kristo anakazia mambo makuu matatu: Hija ya Kanisa; Utayari na Maamuzi ya busara ili kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani! Papa Francisko kuhusu ufuasi wa Kristo anakazia mambo makuu matatu: Hija ya Kanisa; Utayari na Maamuzi ya busara ili kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani!  (Vatican Media )

Papa Francisko: Masharti ya Ufuasi: Hija, Utayari & Maamuzi!

Papa Francisko asema, ufuasi wa Kristo Yesu unafumbatwa katika: hija ya Kanisa; Utayari na Maamuzi ya busara. Huu ni uamuzi unaopaswa kuwa huru na unaofahamika katika undani wake; uamuzi ambao unatekelezwa kwa kuzingatia upendo, kama kielelezo cha shukrani kwa neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si katika mchakato wa mtu kujitafuta mwenyewe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wito wa kumfuasa Kristo Yesu una raha, masharti, magumu na changamoto zake zinazopaswa kuvaliwa njuga kwa imani, matumaini na mapendo thabiti; kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake! Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, Mwinjili Luka, kwa umakini mkubwa anamwonesha Kristo Yesu akifunga safari ndefu kwenda Yerusalemu, lakini Wasamaria hawampokei. Hii ni safari inayovuka mipaka ya mahali na kijiografia na kuzama ndani kabisa katika maisha ya kiroho yanayopewa tafsiri yake kitaalimungu, kwani Yesu alikuwa anaelekea kutekeleza na hatimaye, kutimiza utume wake kama Masiha.

Kristo Yesu anafanya maamuzi mazito kabisa katika maisha na utume wake, anawataka wale wote wanaoitikia wito wake, kujipima na uamuzi huu bila kuyumbishwa wala kuteteleka! Haya ni maamuzi yanayojikita katika hija ya Kanisa, utayari na uamuzi makini na wabusara! Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 30 Juni 2019. Mwinjili Luka anawasilisha mbele ya macho ya wasomaji wake wahusika wakuu watatu, kama dira na mwongozo kwa wale wanaotaka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao.

Baba Mtakatifu anasema, Mhusika wa kwanza akasema, nitakufuata kokote utakakokwenda. Lakini Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake. Yesu alikuwa ameacha yote hata uhakika na usalama wa maisha yake, ili kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu kwa kondoo waliopotea. Kwa njia hii, amewaonesha wafuasi wake kwamba, utume wao hapa duniani ni  wa haraka, endelevu na unafumbatwa katika hija na ufukara wa Kiinjili. Kanisa kwa asili, daima liko safarini, wala haliwezi kuridhika kukaa kitako na kujifungia katika nyua zake binafsi.

Kanisa lina mwelekeo mpana zaidi, kwani linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa mataifa, hadi kufikia pembezoni mwa jamii na mambo msingi ya maisha. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mhusika wa pili alipata mwaliko kutoka kwa Yesu ili aweze kumfuata, lakini akamwomba ampatie kwanza ruhusa aende kumzika baba yake! Lakini Yesu akamwambia, waache wafu wazike wafu wao, bali yeye aende akautangaze Ufalme wa Mungu.Ombi hili ni muhimu kisheria kwani linakita uzito wake kwenye Amri ya Mungu ya kumpenda baba na mama, ili kupata heri na miaka mingi duniani. Hata hivyo Yesu anamjibu akimwambia; waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe nenda ukautangaze Ufalme wa Mungu.

Haya ni maneno makali yanayotoa changamoto kubwa katika ufuasi! Lakini, Kristo Yesu anataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ufuasi, utangazaji na ushuhuda wa Ufalme wa Mungu kuliko hata mambo msingi katika maisha kama ilivyo familia. Ole wao wale wanaodhani kwamba wito ni kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi au kwa kutaka kujijengea jina! Kuna haraka ya kutangaza na kushuhudia Injili inayovunjilia mbali mnyororo wa utamaduni wa kifo na kufungua ukurasa mpya wa maisha na uzima wa milele! Kumbe, hapa hakuna “kulala wala kuchelewa”; bali wafuasi wa Kristo wanapaswa kuwa tayari kujitoa na kujisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Mhusika wa tatu, alitamani kumfuasa Kristo Yesu, lakini kwa masharti kwamba apewe ruhusa kwanza akawaage watu wa nyumbani kwake. Lakini Yesu anamkata kauli kwa kumwambia kwamba, mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu. Wito na ufuasi wa Kristo Yesu unafutilia mbali majuto pamoja na kuangalia mambo ya kale na badala yake, wale wanaotaka kumfuasa Kristo lazima wawe na fadhila kuamua kwa busara! Baba Mtakatifu Francisko kwa muhtasari anasema, Kristo Yesu amebainisha mambo makuu matatu yanayopaswa kupewa kipaumbele kwa wale wote wanaotaka kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani.

Kimsingi wanapaswa kukazia: hija ya Kanisa; Utayari na Maamuzi ya busara; haya ni mambo msingi katika maisha, kama njia ya kuwa mfuasi amini wa Kristo Yesu. Huu ni uamuzi unaopaswa kuwa huru na unaofahamika katika undani wake; uamuzi ambao unatekelezwa kwa kuzingatia upendo, kama kielelezo cha shukrani kwa neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si katika mchakato wa mtu kujitafuta mwenyewe. Yesu anapenda kuona waja wake wakionesha upendo wa dhati kabisa mbele yake na kwa ajili ya Injili. Upendo huu unapata tafsiri yake katika huduma kwa Mungu na jirani; kwa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; kwa kuwakaribisha, kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama Kristo Yesu mwenyewe alivyotenda katika maisha na utume wake.

Bikira Maria, kielelezo cha Kanisa linalofanya hija, awasaidie waamini kumfuasa Kristo Yesu kwa furaha na kutangaza, kwa ari, moyo na upendo mkuu Habari Njema ya Wokovu!

Papa: Ufuasi

 

30 June 2019, 14:53