Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema wafungwa wanapaswa kujengewa imani, matumaini na mapendo, ili kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi! Baba Mtakatifu Francisko anasema wafungwa wanapaswa kujengewa imani, matumaini na mapendo, ili kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi! 

Papa: Barua kwa wafungwa gerezani: Imani, Matumaini & Msamaha!

Baba Mtakatifu Francisko katika katika barua yake kwa wafungwa wa Gereza la Gorgona, anawashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa wafungwa na mahubusu gerezani hapo. Anawasihi wafungwa kuwa na imani na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwani Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, upendo na msamaha wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, magereza yanapaswa kuboreshwa zaidi, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Inasikitisha kusikia na kuona kwamba, magereza yanageuka kuwa ni mahali pa vurugu, uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu; mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa kwa kiasi kikubwa! Wafungwa wanapaswa kujengewa imani na matumaini ya kuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi wanapohitimisha adhabu zao magerezani. Hiki kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza maisha mapya! Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliowaandikia wafungwa wanaotumikia adhabu zao kwenye Gereza la Kisiwa cha Gorgona, huko Livorno, Kaskazini mwa Italia.

Barua hii imepelekwa gerezani hapo na Kardinali Ernst Simoni mwenye umri wa miaka 91 sasa ambaye aliteseka gerezani bila hatia kwa muda wa miaka 25, akafanyishwa kazi ngumu. Huyu ni mtu wa Mungu aliyeonja dhuluma na nyanyaso katika maisha yake; mateso na magumu ya maisha ya gerezani!Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wafungwa hao gerezani hapo kwa kumshirikisha mang’amuzi, changamoto na kero za maisha ya gerezani, kwa kuzingatia ukweli na uwazi! Wafungwa wanapokuwa gerezani hapo, wanaendelea kufanya kazi zinazowapatia utambulisho wao kama binadamu na mwisho wa mwezi wanapewa ujira kidogo kwa ajili ya kugharimia maisha yao binafsi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hali ya magereza si rahisi sana kwani ina changamoto zake, mwaliko kwa Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinaonesha uwepo wake wa kimama miongoni mwa wafungwa, kwani kwa sehemu kubwa magereza ni maeneo ya mateso na ukombozi wa ndani, kwani hakuna binadamu ambaye ni mkamilifu zaidi, wote wanatenda dhambi na kutindikiwa neema ya Mungu. Huu ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha kwa matendo mema, adili na manyofu. Baba Mtakatifu katika barua hii, anawashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo na ukarimu kwa wafungwa na mahubusu gerezani hapo.

Baba Mtakatifu anawataka wafungwa kuwa na imani na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwani Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, upendo na msamaha wa kweli! Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawaweka wafungwa wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa! Kardinali Ernst Simoni, Jumamosi tarehe 22 Juni 2019 kwa niaba ya Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kwa kuonesha mshikamano wake wa huruma na upendo. Amewahimiza wafungwa kuendelea kuwa na imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha! Kardinali Ernst Simoni ametembelea na kukagua kazi zinazofanywa na wafungwa hao kama sehemu ya mafunzo ya uzalishaji na huduma. Kwa hakika uwepo wake gerezani hapo, umekuwa ni ushuhuda wa nguvu kwa wafungwa wengi!

Papa: Wafungwa
24 June 2019, 10:12