Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko kuongoza maziko ya Askofu mkuu Lèon Kalenga Badikebele, Balozi wa Vatican nchini Argentina, aliyefariki dunia tarehe 12 Juni 2019. Baba Mtakatifu Francisko kuongoza maziko ya Askofu mkuu Lèon Kalenga Badikebele, Balozi wa Vatican nchini Argentina, aliyefariki dunia tarehe 12 Juni 2019. 

Papa Francisko kuongoza Ibada ya Mazishi ya Askofu mkuu L. Kalenga

Papa Francisko, Jumamosi tarehe 15 Juni 2019 anaongoza Ibada ya mazishi ya Marehemu Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Argentina ambaye amefariki dunia, tarehe 12 Juni 2019. Ibada hii inahudhuriwa na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Vatican kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao wako mjini Vatican. Tukio la Kihistoria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 15 Juni 2019 majira ya saa 1:30 asubuhi kwa saa za Ulaya ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Argentina ambaye amefariki dunia, tarehe 12 Juni 2019. Ibada hii inahudhuriwa kwa namna ya pekee na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Vatican kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao, kuanzia tarehe 12-15 Juni 2019 wako mjini Vatican kwa ajili ya mkutano maalum.

Hii ni  sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Baba Mtakatifu Francisko katika kuimarisha umoja, mshikamano na mafungamano na wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu alipokutana na Mabalozi pamoja na wawakilishi hawa, Alhamisi, tarehe 13 Juni 2019 amewapatia Mwongozo wa maisha na utume wao unaowakumbusha kwamba: Mabalozi ni watu wa Mungu na Kanisa wenye ari na mwamko wa kitume. Ni wapatanishi na wawakilishi wa Papa; ni watu wanaochakarika kwa ajili ya maendeleo ya watu; maisha yao yanapaswa kusimikwa katika utii, sala, huduma ya upendo na unyenyekevu wa maisha, kama wafuasi wa Kristo Yesu!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko ili kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Vatican, alisema kwamba, wameungana na Mwamba wa imani, ili kutangaza na kushuhudia Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hii ni fursa ya ushuhuda wa umoja na furaha ili kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro “Per videre Petrum” aliyekiri na kuungama kwa mara ya kwanza imani kwa Kristo Yesu, kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai. Mkutano huu ni kama hija ya kitume inayotekelezwa na Maaskofu mahalia kila baada ya miaka mitano, kwa kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini wao, hadi sasa hija hii inayeendelea kuadhimishwa kila baada ya miaka mitatu.

Mabalozi na wawakilishi wa Vatican wanatambua kwamba, ni kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu wameweza kuteuliwa miongoni mwa Wakleri kwa ajili ya kumwakilisha Baba Mtakatifu sehemu mbali mbali za dunia! Wanatambua udhaifu na mapungufu yao kama wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwenye Makanisa mahalia, Serikali na Mashirika ya Kimataifa. Ni kutokana na muktadha huu anasema Kardinali Pietro Parolin, wako mbele ya Baba Mtakatifu anayeendelea kutekeleza dhamana na utume wake kama msingi wa umoja wa Kanisa, ili aweze kuwaimarisha ndugu zake katika imani, hususan wakati huu, Kanisa linapokumbana na mawimbi mazito katika maisha na utume wake.

Kardinali Parolin anasema, ingawa mtumbi huu ambao ni Kanisa hauwezi kuzama kwa sababu nahodha wake ni Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hata katika dhuluma na nyanyaso, Msalaba wa Kristo utaendelea kuwa ni kielelezo cha ushindi na njia inayowaelekeza waamini kwenda kwa Baba wa mbinguni. Mabalozi na wawakilishi hawa wako mbele ya Baba Mtakatifu wakiomba, awaimarishe katika imani na huduma kwa ajili ya watu wa Mungu. Mwishoni mwa hotuba yake, Kardinali Pietro Parolin, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameendelea kuonesha kipaumbele cha pekee kwa Mabalozi na wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, anawatia shime, kuweza kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo. Wanatambua na kuthamini wosia wake katika maisha na utume wao, ili daima waendelee kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; na kwa waamini wanaowahudumia kwa ukarimu na upendo!

Kard. Parolin
14 June 2019, 16:08