Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani 2019 unaongozwa na kaui mbiu " Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu" Ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani 2019 unaongozwa na kaui mbiu " Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu"  (Vatican Media)

UJUMBE WA PAPA FRANCISKO SIKU YA 56 YA KUOMBEA MIITO

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani anapenda kutafakari na vijana ili kuona jinsi ambavyo Mungu anawawezesha watu kuwa ni vyombo vya ahadi zake, lakini akiwataka kuwa na ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi zake kama ilivyojionesha kwa wito wa Mitume wa kwanza wa Yesu waliokuwa wakivua samaki kwenye Ziwa Galilaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu”. Siku hii inaadhimishwa Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema na kwa mwaka huu inaadhimishwa tarehe 12 Mei 2019. Ujumbe huu ni matunda ya tafakari ya kina kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyoadhimishwa, Oktoba 2018 mjini Vatican na kufuatiwa na Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani iliyoadhimishwa huko Panama.

Matukio yote haya anasema Baba Mtakatifu yameliwezesha Kanisa kusikiliza kwa makini sauti ya Roho Mtakatifu na kilio cha maisha ya vijana, wanaoendelea kujiuliza maswali mengi, vijana ambao wanaelemewa na changamoto za maisha bila kusahau matumaini yanayofumbatwa katika maisha yao! Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anapenda kutafakari na vijana ili kuangalia jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anawawezesha watu kuwa ni vyombo vya ahadi zake, lakini akiwataka kuwa na ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi za Mungu kama ilivyojionesha kwa wito wa Mitume wa kwanza wa Yesu waliokuwa wakivua samaki kwenye Ziwa Galilaya.

Mitume hawa ni Simoni, Yohane na Andrea nduguye, waliokuwa wanaendelea na kazi yao ya kuvua samaki. Hii ni kazi ngumu, iliyowawezesha kujifunza sheria asilia na wakati mwingine walipambana na changamoto za maisha ya Ziwani. Kuna wakati walikabiliwa na upepo mkali, siku nyingine waliambulia patupu; wakiwa wamechoka na kujikatia tamaa. Haya ni matukio ya maisha ya kawaida yanayodhihirisha, ari na mwamko wa ndani pamoja na matumaini yaliyoko moyoni. Ni watu waliokuwa “wanaogelea katika bahati nasibu ya maisha”, ili siku moja waweze kupata furaha ya ndani.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuna siku Mitume walikuwa wana bahatika kupata samaki wengi, lakini wakati mwingine, iliwabidi kuwa na ujasiri wa kuongoza mtumbwi uliokuwa unaelemewa na mawimbi mazito pamoja na kuchanganyikiwa kwa kuona kwamba, walikuwa wameambulia patupu baada ya kazi ya usiku kucha! Katika mazingira kama haya, kweli yataka moyo! Hii ndiyo hali inayojitokeza katika miito mbali mbali ya maisha ndani ya Kanisa. Yesu akiwa anatembea, akawaona wavuvi na kuwakaribia. Hivi ndivyo waamini walivyoamua kufanya: kwa wale walioamua kufunga ndoa au kujiungia katika maisha ya kipadre na kitawa kwa sababu wamepata mang’amuzi yamshangao kwa kukutana na Kristo Yesu. Na tangu wakati huo, wakaanza kuonjea furaha ya ajabu ndani mwao, furaha inayozima kiu ya maisha!

Kristo Yesu akiwa kandoni mwa Ziwa Galilaya, akakutana na wavuvi ambao waliamua kuvunjilia mbali mazoea yao na kuonesha ujasiri wa kuthubutu kuambata ahadi ya Kristo kwamba, “Nitawafanya kuwa wavuvi wa watu”. Mwenyezi Mungu anapomwita mja wake, si kwamba, anaingilia uhuru wake na “kumtwisha zigo zito” la hasha! Bali huu ni mwaliko wa upendo unaotolewa na Mwenyezi Mungu, ili kuweza kuingia na kushiriki katika mradi wake mpana zaidi, kwa kuondokana na mazoea, ili kupata maana kamili ya maisha kwa kuwa na dira pamoja na mwelekeo mpya wa maisha. Kila mtu ameitwa kwa jinsi ya ajabu na kwamba, maisha Nni ya maana sana.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani anasema, wito maana yake ni mwaliko wa kumfuasa Kristo Yesu katika njia ambayo amewaandalia waja wake, ili kuweza kuwakirimia furaha ya kweli pamoja na kuwapatia ustawi na mafao, wale wanaowazunguka. Ili kuweza kupokea ahadi hii kuna haja ya kuwa na ujasiri wa kuthubutu, kuacha yote na kuanza kumfuasa Kristo Yesu kama walivyofanya wale Mitume wa kwanza, ili kutekeleza ndoto kubwa zaidi katika maisha yao. Kuitikia wito ni kuthubutu kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza, badala ya kuendelea “kuogelea” katika mazoea.

Hii ni nguvu inayomsukuma mwamini kugundua mpango wa Mungu katika maisha yake, badala ya kuendelea “kutengeneza nyavu” ili kuwa na uhakika wa maisha, na badala yake, waamini wanapaswa kujiaminisha katika ahadi ya Mungu. Wito wa kwanza anasema Baba Mtakatifu ni maisha ya Kikristo yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo; matunda ya upendo wa Mungu unaowaunganisha na kuwafanya kuwa ni familia kubwa ya Kanisa. Maisha ya Kikristo yanapata chimbuko lake ndani ya Kanisa, yanakua na kusonga mbele kwa kurutubishwa na usikilizaji wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Sala na matendo ya huruma, kama kielelezo cha imani tendaji, umoja na udugu.

Sakramenti ya Ubatizo inawakirimia waamini maisha mapya yanayowaelekeza kwa Kristo Yesu na kwamba, Kanisa ni Mama mpendelevu, ambaye anapaswa kupendwa na kuheshimiwa na watoto wake, hata pale, watoto wanapogundua “makunyanzi yaliyojaa usoni pake” kutokana na udhaifu wa watoto wake na dhambi zinazowaandama. Watoto wanayo dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, Mama Kanisa anazidi kupendeza, kuchanua na kung’ara, ili aweze kuwa ni shuhuda wa upendo wa Mungu ulimwenguni!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila mwamini kadiri ya wito na dhamana yake katika maisha na utume wa Kanisa anashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anawakumbuka wale wote walioamua kufunga ndoa katika Kristo Yesu, ili kuunda familia na kama ilivyo kwa miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Mfano ni: wafanyakazi, wataalamu, mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo na mshikamano; viongozi wa kijamii na wanasiasa. Wote hawa wanawezeshwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni vyombo vinavyobeba: ahadi ya wema, upendo na haki jamii; tunu msingi zinazohitaji Wakristo wenye ujasiri na mashuhuda amini wa Ufalme wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukufanua kwamba, katika safari ya maisha, kuna baadhi ya watu wanakutana na Kristo Yesu na hivyo kuamua kufuata wito wa kuwekwa wakfu na upadre, wakiwa na furaha kubwa, ari na moyo mkuu, lakini pia woga na wasi wasi wa kuwa ni wavuvi wa watu! Hii ni sadaka inayowataka kujitosa bila ya kujibakiza ili kutekeleza huduma ya kutangaza na kushuhudia Injili kwa ndugu zao, katika hali ya uaminifu mkuu! Katika hali na mazingira kama haya, yataka moyo kuweza kuisikiliza sauti ya Mungu anayeita, kwani mazingira ya sasa si rafiki sana, kwani yanaonekana kutaka kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kiasi hata cha kutumbukia katika “mchoko wa kukosa matumaini.”

Baba Mtakatifu anasema, hakuna furaha kubwa zaidi kama mwamini kuthubutu kusadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa Mwenyezi Mungu pamoja na jirani. Anawataka vijana, kusikiliza na kutikia wito kutoka kwa Mungu, kwa kujiaminisha kwake na kamwe wasiogope wala kukatishwa tamaa na woga usiokuwa na mashiko wala mvuto! Kwani kwa wale wote walioacha nyavu zao na kuanza kumfuasa Kristo Yesu, wameahidiwa furaha tele na maisha mapya yanayozima kiu ya moyo!

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si rahisi sana kufanya mang’amuzi ya wito na kuyaelekeza maisha katika haki, ndiyo maana Kanisa zima halina budi kupyaisha tena dhamana na wajibu wake katika utume kwa vijana. Huu ni wajibu unaopaswa kutekelezwa kwa dhati kabisa na; wakleri, watawa, wahamasishaji wa shughuli za kichungaji, walimu na walezi, ili, vijana waweze kupata fursa ya kusikiliza na kufanya mang’amuzi katika maisha yao. Kuna haja ya kuwa na sera na mikakati ya shughuli za kichungaji na miito, itakayowawezesha vijana kugundua mpango wa Mungu katika maisha yao. Kumbe, maisha ya Sala, tafakari ya Neno la Mungu, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na maongozi ya maisha ya kiroho ni muhimu sana katika maisha ya vijana wa kizazi kipya!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuangalia historia na maisha ya Bikira Maria mambo yanayofumbata kwa namna ya pekee: wito, ahadi na hatari katika maisha, lakini kwa Bikira Maria, hakumezwa na woga, bali alikuwa tayari kuitikia kwa ari na moyo mkuu kwa kusema, “Ndiyo”. Huu ni mfano hai kwa mtu anayetaka kuzama kabisa katika mpango wa Mungu kwa kuthubutu na kujiaminisha mbele ya Mungu kwamba, iko siku ahadi ya Mungu itaweza kumwilishwa katika maisha yake. Baba Mtakatifu anawauliza vijana ikiwa kama wanajisikia ndani mwao kuwa ni vyombo vya ahadi ya Mungu katika maisha yao?

Je, ndani ya sakafu ya nyoyo zao, wamebeba ahadi gani? Bikira Maria alibaini hali ngumu iliyokuwa mbele yake, lakini akashinda woga na hofu na kukubali kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake! Hata vijana wanapoona “ukungu katika maisha” wawe na ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye kwa sala. Wamwombe Mwenyezi Mungu ili aweze kuwapatia neema na nguvu, ili kila mmoja wao, aweze kugundua mradi wa upendo wa Mungu katika maisha yake na hatimaye, aweze kuwakirimia ujasiri wa kuthubutu kufuata njia ile ambayo, Mwenyezi Mungu amewaandalia waja wake, tangu milele yote!

Papa: Ujumbe 56 Miito 2019
09 May 2019, 16:39