Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika ujumbe wake kwa familia ya Mungu nchini Romania anasema, anakwenda nchini mwao kama hujaji na ndugu yao! Papa Francisko katika ujumbe wake kwa familia ya Mungu nchini Romania anasema, anakwenda nchini mwao kama hujaji na ndugu yao!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Hija ya Kitume Romania: Twende pamoja!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya Video kwa familia ya Mungu nchini Romania, anasema, anapenda kuonesha furaha yake kwamba, muda si mrefu atakuwa miongoni mwao! Romania ni nchi nzuri na yenye ukarimu na kwamba, anakwenda kati yao kama hujaji na ndugu yao! Ushuhuda wa imani uliooneshwa nchini humo ni amana na utajiri wa Kanisa zima la Romania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Mei hadi 2 Juni 2019 anatembelea Romania, miaka ishirini tangu, hija kama hii ifanywe na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1999. Kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ndiyo maana, kauli mbiu ya hija hii ya 30 Kimataifa inaongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Hii pia ni changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II, akiwataka Wakristo wote nchini Romania kuwa wamoja, chini ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya Video kwa familia ya Mungu nchini Romania, anasema, anapenda kuonesha furaha yake kwamba, muda si mrefu atakuwa miongoni mwao! Romania ni nchi nzuri na yenye ukarimu na kwamba, anakwenda kati yao kama hujaji na ndugu yao! Anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru viongozi wa Serikali waliomkaribisha pamoja na kumpatia ushirikiano mkubwa. Baba Mtakatifu anasema, akiwa nchini Romania, atapata fursa ya kukutana na Patriaki na Sinodi ya Kudumu ya Kanisa la Kiorthodox nchini Romania pamoja na viongozi na waamini wa Kanisa Katoliki. Wote hawa wanaunganishwa na kifungo cha imani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Mitume wa Yesu, yaani Petro na Andrea nduguye.

Mapokeo yanaonesha kwamba, Mitume hawa ndio waliojisadaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Romania. Ikumbukwe kwamba, hawa ni ndugu wa damu, waliothubutu hata kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kati yao kuna umati mkubwa wa mashuhuda wa imani, kama inavyoonesha kwa miaka ya hivi karibuni, Maaskofu saba wa Kanisa Katoliki lenye asili ya Kigiriki, ambao anatarajia kuwatangaza kuwa Wenyeheri. Hawa ni watu walioteseka kiasi hata cha kusadaka maisha yao, amana na utajiri ambao haupaswi kusahaulika. Huu ni urithi wa wote unaowachangamotisha kujenga na kudumisha umoja na mshikamano.

Baba Mtakatifu anasema, anakwenda ili kutembea pamoja nao, ili kujifunza kulinda mizizi ya imani na tunu msingi za maisha ya familia; kwa kuhudumiana; ili kuvuka hofu, mashaka na hali ya kudhaniana vibaya, ili kubomolea mbali kuta zinazowatenganisha. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, kuna watu hadi sasa wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya hija yake ya kitume nchini Romania. Anapenda kuwashukuru wote hawa kutoka katika sakafu ya moyo wake na kwamba, anawahakikishia pia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Hatimaye, anapenda kuwapatia baraka zake za kitume, akiwaomba kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa sala na sadaka yao!

Papa: Romania

 

 

29 May 2019, 16:25