Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anatembelea Romania kuanzia tarehe 31 Mei hadi tarehe 2 Juni 2019 anafanya hija ya kitume nchini Romania inayoongozwa na kauli mbiu "Twende pamoja". Papa Francisko anatembelea Romania kuanzia tarehe 31 Mei hadi tarehe 2 Juni 2019 anafanya hija ya kitume nchini Romania inayoongozwa na kauli mbiu "Twende pamoja". 

Hija ya Papa Francisko Romania: Wananchi wako tayari kwa ugeni!

Baba Mtakatifu Francisko atatembelea mji mkuu wa Bucharest, mji wa Ias ulioko Kaskazini wa Romania pamoja na mji wa Blaj, Kituo kikuu cha utamaduni nchini Romania. Hii itakuwa ni hija ya 30 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Romania kunako mwaka 1999., tukio la kihistoria tangu mwaka 1054.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Mei, Siku kuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti hadi tarehe 2 Juni 2019, Kanisa, sehemu mbali mbali za dunia, linapoadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni atakuwa abafanya hija ya kitume nchini Romania. Baba Mtakatifu atatembelea mji mkuu wa Bucharest, mji wa Ias ulioko Kaskazini wa Romania pamoja na mji wa Blaj, Kituo kikuu cha utamaduni nchini Romania. Hii itakuwa ni hija ya 30 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Romania kunako mwaka 1999.

Hili lilikuwa ni tukio la kihistoria tangu Kanisa lilipotengana kunako mwaka 1054 na huo ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo! Takwimu zinaonesha kwamba, Romania ina idadi ya watu wapatao milioni 20 na asilimia 86% ni waamini wa Kanisa la Kiorthodox na asilimia 7.3% ni waamini wa Kanisa Katoliki. Hija hii ya kitume inaongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja”, mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembea kwa pamoja chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwa kukataa kishawishi cha uchoyo na ubinafsi, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anatembelea Romania ili kuimarisha imani miongoni mwa ndugu zake katika Kristo sanjari na kukazia umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Romania. Askofu mkuu Ion Robu wa Jimbo kuu la Bucarest katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, kwa sasa familia ya Mungu nchini Romania, iko tayari kumpokea na kumkarimu, Baba Mtakatifu anayetarajiwa kuwatembelea hivi karibuni. Hii ni fursa na upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, uwepo wake kwao ni alama ya sherehe na furaha kubwa.

Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Romania, miaka ishirini tangu, hija kama hii ifanywe na Mtakatifu Yohane Paulo II. Kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ndiyo maana, kauli mbiu ya hija hii ni “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Hii pia ni changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II, akiwataka Wakristo wote nchini Romania kuwa wamoja, chini ya Kristo Yesu. Romania inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira na kazi na matokeo vijana wengi wanakimbilia kwenda nje ya nchi ili kutafuta fursa hizi. Matokeo yake ni kuyumba kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Papa: Romania

 

28 May 2019, 16:02