Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Fumbo la Pasaka ni ujumbe wa furaha, imani na matumaini kwa watu wa Mungu! Papa Francisko: Fumbo la Pasaka ni ujumbe wa furaha, imani na matumaini kwa watu wa Mungu!  (AFP or licensors)

Hija ya kitume: Bulgaria: Ujumbe wa Furaha ya Pasaka!

Kristo Amefufuka kweli kweli. Huu ni ujumbe wa furaha, matumaini na ushuhuda wa imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kristo Mfufuka anawataka waja wake, kupyaisha maisha yao, kwa kuwa hai kwa sababu yuko ndani mwao na kamwe hatawatelekeza kamwe! Kristo Yesu, daima yuko tayari na anawasubiri waamini waweze kumrudia na kuanza upya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Bulgaria, Jumapili tarehe 5 Mei 2019 ametembelea Kanisa kuu la Kipatriaki na kusali mbele ya kiti cha Watakatifu Cyril na Methodi wanaoheshimiwa sana kutokana na mchango wao katika mchakato mzima wa uinjilishaji, utamadunisho na umwilishaji wa Neno la Mungu katika Liturujia takatifu na katika uhalisia wa maisha! Akiwa mbele ya Kanisa hili, Baba Mtakatifu amewaongoza waamini kusali Sala ya Malkia wa Mbingu. Amewakumbusha salam ambayo Wakristo wamezoea kusalimiana wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani Kristo Amefufuka kweli kweli.

Huu ni ujumbe wa furaha, matumaini na ushuhuda wa imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kristo Mfufuka anawataka waja wake, kupyaisha maisha yao, kwa kuwa hai kwa sababu yuko ndani mwao na kamwe hatawatelekeza kamwe! Kristo Yesu, daima yuko tayari  na anawasubiri waamini waweze kumrudia na kuanza upya, pale wanapojisikia kwamba, wanaanza kuzeeka kwa sababu ya majonzi, hofu, wasi wasi na mashaka. Kristo Mfufuka daima yuko tayari kupyaisha maisha ya waja wake kwa kuwakirimia nguvu na matumaini. Kwa muda wa miaka zaidi ya elfu mbili, imani kwa Kristo Mfufuka imetangazwa ulimwenguni kutokana na juhudi pamoja na ukarimu wa wamisionari na waamini waliojisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili.

Katika maisha na utume wake, Kanisa nchini Bulgaria, limebahatika kupata wachungaji waliojipambanua kwa utakatifu wao, kama ilivyo kwa Mtakatifu Yohane XXIII aliyeishi nchini Bulgaria kuanzia mwaka  1925 hadi mwaka 1934. Akapendwa na waamini wa Kanisa la Mashariki, akajenga urafiki na waamini wa dini mbali mbali na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia. Katika maisha na utume wake, akawa mstari wa mbele kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene, yaliyokuwa na mwangi mkubwa sana wakati wa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ulioitishwa kwa utashi wake. Katika muktadha huu, wananchi wa Bulgaria wakamwita “Yohane Papa mwema”.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika hija yake ya kitume, atapata nafasi pia ya kukutana na kuzungumza na wawakilishi wa madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini Bulgaria. Hali inayoonesha kwamba, Bulgaria ni nchi ya Kiorthodox inayotaka kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana kama sehemu ya mbinu mkakati na kipimo cha kufahamiana. Baba Mtakatifu anasema, ametoa heshima yake kwa watakatifu Cyril na Methodi wanjilishaji mahiri wa Waslav. Amekutana na kuzungumza na Patriaki Neofit pamoja na wajumbe wa Sinodi Takatifu. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu amewaalika waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa Mbingu na Nchi, ili aweze kuwaombea kwa Kristo Mfufuka.

Bulgaria iwe kweli ni mahali pa watu kukutana na kuheshimiana, kwa kuvuka mipaka ya tofauti za kitamaduni, kidini na kikabila, kwa kujisikia kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja. Baba Mtakatifu amesali Sala ya Malkia wa Mbingu mbele ya Sanamu ya “Bikira Maria wa Nessebar” yaani “Bikira Maria Mlango wa Mbingu”. Sanamu hii ilipendwa sana na Mtakatifu Yohane XXIII, akatembea nayo hadi kicho chake!

Papa: Malkia wa Mbingu
05 May 2019, 14:19