Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumsikiliza Roho Mtakatifu ili wasimezwe na malimwengu! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumsikiliza Roho Mtakatifu ili wasimezwe na malimwengu!  (Vatican Media )

Papa: Msikilizeni Roho Mtakatifu msimezwe na malimwengu!

Kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa ni: kufundisha na kuwakumbusha yale yote walioambiwa. Kristo Yesu ni utimilifu wa ufunuo wa Baba wa mbinguni, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Kwa njia ya uwepo tendaji wa Roho Mtakatifu, Mitume wa Yesu wataweza kuwa na ufahamu wote pamoja na kuyakumbuka yale ambayo Yesu mwenyewe amewafundisha Mitume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu, wakati wa Karamu ya Mwisho, aliwafundisha Mitume wake kumpenda, kuyashika maneno yake pamoja na kumpenda Baba yake wa mbinguni. Akawaahidia Roho Mtakatifu, Msaidizi na zawadi ya Baba kwa njia ya Mwana, atakayewafundisha yote na kuwakumbusha yote waliyoambiwa na Kristo Yesu.  Atakuwa pamoja nao hadi utimilifu wa nyakati kwa njia ya Roho Mtakatifu, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia! Roho Mtakatifu ni msaidizi na mfariji.

Kristo Yesu anakwenda kwa Baba yake wa mbinguni, ataendelea kuwafundisha na kuwahamasisha wafuasi wake kwa njia ya Roho Mtakatifu! Kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa ni: kufundisha na kuwakumbusha yale yote walioambiwa na Kristo Yesu wakati alipokuwa hapa duniani. Kristo Yesu ni utimilifu wa ufunuo wa Baba wa mbinguni, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Kwa njia ya uwepo tendaji wa Roho Mtakatifu, Mitume wa Yesu wataweza kuwa na ufahamu wote pamoja na kuyakumbuka yale ambayo Yesu mwenyewe amewafundisha mitume wake. Hii pia ni dhamana na utume unaoendelezwa na Mama Kanisa kwa kuwa na imani ya dhati kwa Kristo Yesu.

Kanisa linapotekeleza Neno lake pamoja na Wakristo kuwa ni wasikivu kwa Roho Mtakatifu, anayewawezesha kuendelea kuishi na kushuhudia uwepo wa Kristo Mfufuka katika maisha yao; tayari kupokea kwa moyo wa ukarimu amani ambayo wanapaswa kuitangaza na kuishuhudia, kwa kujenga na kudumisha madaraja ya kukutana na wengine! Huu ni muhtasari wa tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili, tarehe 26 Mei 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ili Kanisa liweze kutekeleza yote haya kwa ukamilifu zaidi, kila Mkristo na kila Jumuiya inaitwa kutembea katika mwanga wa Roho Mtakatifu anayetaka kufanya yote mapya.

Hii ni changamoto ya kuondokana na malimwengu, yanayoangaliwa kwa kipimo cha binadamu, mikakati na malengo yake; mambo ambayo wakati mwingine, yanasigana kabisa na hija ya imani pamoja na unyenyekevu wa kusikiliza Neno la Mungu. Roho Mtakatifu anataka kuwaongoza waamini pamoja na kuliongoza Kanisa, ili kuwa na mng’ao halisi, mzuri na angavu kutoka kwa Kristo Yesu. Wakati huo huo, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kumfungulia Roho Mtakatifu malango ya nyoyo zao, ili kupokea zawadi ya Roho Mtakatifu, ili aweze kuwaongoza katika njia za historia. Ni Roho Mtakatifu ambaye siku kwa siku, anawafundisha wafuasi wa Kristo mantiki ya Injili, upendo wenye ukarimu na “kuwafundisha yote” pamoja na “kuwakumbusha yale yote walioambiwa na Kristo Yesu.

Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, Mwezi Mei ni mwezi ambao umetengwa rasmi kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria, Malkia wa mbingu, apende kwa tunza yake ya kimama, kulilinda Kanisa pamoja na kuwalinda watu wote. Bikira Maria ambaye kwa njia ya imani, unyenyekevu na ujasiri, ameshirikiana kikamilifu na Roho Mtakatifu kwa ajili ya kutekeleza Fumbo la Umwilisho wa Mwana wa Mungu, awasaidie hata waamini waweze kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwafundisha na kuwaongoza, ili kulipokea Neno la Mungu, kulitangaza na kulishuhudia kwa njia ya maisha!

Papa: Roho Mtakatifu
27 May 2019, 15:05