Tafuta

Vatican News
Zakayo mtoza ushuru alipata taabu sana kuutafuta Uso wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake! Akaonana na Yesu, akatubu, akaongoka na kufanya mapilizi! Zakayo mtoza ushuru alipata taabu sana kuutafuta Uso wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake! Akaonana na Yesu, akatubu, akaongoka na kufanya mapilizi! 

Papa: Zakayo mtoza ushuru: Huruma na upendo wa Mungu!

Mkutano wa 42 wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Kitaifa nchini Italia uliofunguliwa kuanzia tarehe 5-7 Aprili 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Leo wokovu umefika nyumbani humu: Yesu ana nguvu ya kuokoa. Mwanadamu anayo furaha ya kuhudumia”. Katika ulimwengu wa utandawazi: mwanadamu amekuwa na mwelekeo wa kudhani kwamba, ameokoka, yuko salama na analindwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. – Vatican.

Zakayo Mtoza ushuru alikuwa akitafuta kumwona Kristo Yesu ni mtu wa namna gani. Kwa bahati mbaya umati wa watu ulimzuia kumwona Yesu, kwa sababu alikuwa mfupi wa kimo. Alitamani kuona Uso wa Kristo, ufunuo wa upendo na huruma ya Baba wa milele. Kristo Yesu ni kielelezo cha utimilifu wa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni, kwa njia ya utii, mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu! Ili kuweza kuingia mbinguni, mwamini anapaswa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake!

Mwenyezi Mungu daima amekuwa “akichakarika usiku na mchana bila kupumzika” kama inavyoonesha Injili, kumtafuta mwanadamu aliyetopea katika dhambi ili aweze kutubu na kumwongokea kama ilivyokuwa kwa Zakayo, tajiri, mtoza ushuru lakini mfupi wa kimo, aliyetamani sana kumwona Kristo Yesu katika maisha yake, kiasi cha kupanda juu ya mkuyu! Kristo Yesu alipofika mahali pale, akamwambia Zakayo ashuke upesi, kwani alitamani kushinda nyumbani kwake, kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

Mkutano wa 42 wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Kitaifa nchini Italia uliofunguliwa kuanzia tarehe 5-7 Aprili 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Leo wokovu umefika nyumbani humu: Yesu ana nguvu ya kuokoa. Mwanadamu anayo furaha ya kuhudumia”. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, mwanadamu amekuwa na mwelekeo wa kudhani kwamba, ameokoka, yuko salama, analindwa pamoja na kuendelea kujiaminisha kwamba, anaweza kujiokoa mwenyewe pasi ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Jumuiya za Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Kitaifa nchini Italia, katika muktadha huu, kimeamua kama ilivyokuwa kwa Zakayo mtoza ushuru kutafuta uso wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake.

Wajumbe hawa wanatambua na kuthamini kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu wa ulimwengu. Ndiye aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni dhamana na wajibu wa Wakristo kutambua kwamba, wanaitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wajumbe hawa wanatafakari kuhusu chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka wa Kristo Yesu na sehemu ya pili wameangalia kero za maisha pasi na uwepo wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Zakayo Mtoza ushuru kabla ya kukutana na ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Zakayo Mtoza ushukuru anatubu na kumwongokea Mungu na macho yake yanafunguliwa, na hivyo kuona dhambi zilizokuwa zinampekenya na akawa tayari kutimiza malipizi kwa kuwasaidia maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanahamasishwa kumtafuta Mungu na kuwahudumia jirani zao, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji. Dr. Salvatore Martinez, Rais wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Kitaifa nchini Italia katika mkutano huu, amewasilisha pia salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anawapongeza kwa kauli mbiu inayoongoza mkutano huu wa sala kwa kukazia kwamba, kwa hakika, Kristo Yesu amepewa mamlaka na nguvu ya kumkomboa mwanadamu na mwanadamu kwa upande wake anapaswa kuhudumia katika furaha ya kweli!

Baba Mtakatifu anapenda kuungana pamoja nao kiroho, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliyejitaabisha kuwalisha watu Chakula cha Neno la Mungu; akawasamehe dhambi zao, akawaganga na kuwaponya; akawalisha na kuwanywesha na hatimaye, akawafungulia mlango wa huruma na upendo wa Baba wa milele wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Baba Mtakatifu anakazia ushuhuda wenye mvuto na mashiko, unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na Tafakari ya kina ya Maandiko Matakatifu!

Kwa upande wake, Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, huu ndio muda uliokubalika kwa watu wa Mungu kutembea pamoja kama Jumuiya za imani zinazotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ili kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya maisha ya kiroho, kanuni maadili na utu wema. Haya ni mambo msingi yanayohimizwa sana na Baba Mtakatifu Francisko! Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni changamoto na mwaliko wa kumkimbilia Kristo Yesu, ili kuonja huruma na upendo wa Baba wa milele anayeangalia undani wa mtu na wala si maumbile na hali yake.

Kardinali Kevin Joseph Farrell  anakaza kusema, ushuhuda wa maisha ya Kikristo unapaswa kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika Injili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hata leo hii, uwepo wa Kristo Yesu: unaongoa, una fariji, unawaweka watu huru, unaganga na kuponya udhaifu na dhambi za binadamu! Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limeanzisha kitengo maalum kijulikanacho kama “CHARIS” katika asili yake, neno hili maana yake ni “neema au zawadi maalum kutoka kwa Roho Mtakatifu”.

Hiki ni kitengo kinachotoa huduma ya kimataifa kwa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki  Wakatoliki na kilizinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2018, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Hii ni siku ambayo Katiba inayosimamia shughuli za kitengo hiki kama dira na mwongozo wa kusimamia na kukuza imani ya Kanisa Katoliki ilizinduliwa. Zote hizi ni kazi za Roho Mtakatifu zinazoendelea kupyaisha maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Farrell anakaza kusema, hata Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Kimataifa kiko chini ya mwongozo wa Katiba hii. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, wanachama wa vyama hivi vya kitume, wataendelea kuonesha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na kukuza umoja, udugu na ushirikiano na vyama vingine. CHARIS ni msaada mkubwa kwa Mabaraza ya Maaskofu pamoja na Wakleri watakaokuwa wanahitaji msaada wake kwa ajili ya huduma kwa vyama na mashirika ya kitume!

Wakati huo huo, Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anasema, Zakayo Mtoza ushuru anaonesha ile shahuku inayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake ya kutaka kukutana na Kristo Yesu, mwanzo wa mchakato wa toba na wongofu wa ndani. Yesu kwa kuingia na kushinda nyumbani mwa Zakayo Mtoza ushuru, anatubu na kumwongokea Mungu. Aliwaka ndani mwake, moto wa kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, huku akiongozwa na Roho Mtakatifu. Waamini wawe na ujasiri wa kuomba nguvu na neema ya Roho Mtakatifu itakayowasindikiza kuuelekea utakatifu wa Mungu!

Zakayo Mtoza Ushuru
06 April 2019, 16:21