Tafuta

Vatican News
Papa Francisko. Mkesha wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana anawaalika Wakristo kuondoa mawe kwenye makaburi ya nyoyo zao, ili Mwanga wa matumaini uweze kupenya! Papa Francisko. Mkesha wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana anawaalika Wakristo kuondoa mawe kwenye makaburi ya nyoyo zao, ili Mwanga wa matumaini uweze kupenya!  (ANSA)

PASAKA YA BWANA 2019: Papa Francisko: Kesha la Pasaka

Papa Francisko katika mkesha wa Pasaka, amekazia: Ushuhuda wa wanawake katika Fumbo la Ufufuko; Changamoto walizokutana nazo kaburini na hatimaye, Habari Njema kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kutoka kwa wafu! Siku ya kwanza ya juma, wanawake wakiwa na manukato yao walikwenda kaburini, lakini wakiwa na hofu ya jiwe lile kubwa mlangoni pa kaburi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C. PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika “Kesha la Pasaka”, Jumamosi, 20 Aprili 2019 akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameongoza Ibada ya Mkesha wa Pasaka. Kwanza kabisa, amebariki moto wa Pasaka na kuongoza maandamano ya waamini kuingia Kanisani na baadaye ikaimbwa “Mbiu ya Pasaka” inayosimulia “Sifa ya Mshumaa wa Pasaka”, kielelezo cha Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu meongoza Ibada ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ubatizo ambamo amewabatiza wakatekumeni 8 na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara. Kati yao ni Anastazia Clara kutoka Indonesia, aliyezaliwa kunako mwaka 1958. Wakatekumeni wengine wanatoka Italia, Equador, Perù, Albania na Indonesia. Na hatimaye, Liturujia ya Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake kwenye mkesha wa Pasaka, amekazia kwa namna ya pekee mambo makuu matatu: Ushuhuda wa wanawake katika Fumbo la Ufufuko; Changamoto walizokutana nazo kaburini na hatimaye, Habari Njema kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kutoka kwa wafu! Siku ya kwanza ya juma, wanawake wakiwa na manukato yao walikwenda kaburini, lakini wakiwa na hofu ya jiwe lile kubwa mlangoni pa kaburi! Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo safari ya wokovu ambayo waamini wamefanya kumbu kumbu yake katika Mkesha wa Pasaka, kwa kuangalia uzuri wa kazi ya uumbaji dhidi dhambi; ukombozi kutoka utumwani dhidi ya ukosefu wa uaminifu katika kutekeleza Agano na Mwenyezi Mungu! Ahadi za Manabii dhidi uhaba wa imani kutoka kwa watu wa Mungu.

Hivi ndivyo inavyoendelea kujitokeza katika historia ya Kanisa na ya kila mwamini, kiasi cha kuonekana kwamba, safari iliyofanyika haizai matunda yanayokusudiwa, kwa kufikia lengo lake. Matokeo yake ni waamini kuchanganyikiwa na hatimaye, kupoteza matumaini, mwanzo wa giza katika maisha! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, jitihada za wale wanawake si kazi bure, kwani kazi kubwa imetendwa na Mwenyezi Mungu kwa kuwaondolea lile jiwe kubwa, kikwazo cha matumaini yaani: ukosefu wa matumaini, kifo, dhambi, woga pamoja na kumezwa na malimwengu. Historia ya maisha ya mwanadamu ni safari inayomsaidia kugundua “Jiwe hai” yaani Kristo Mfufuka, msingi imara wa Kanisa lake hata kama bado kuna changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza! Kristo Mfufuka anapyaisha yote na kuwainua wale waliokata tamaa.

Waamini wanahamasishwa kumtafuta Kristo Mfufuka kwa kuhakikisha kwamba, kwanza kabisa wanaondoa jiwe, kizingiti ambacho wanapaswa kukipatia jina! Ni mwaliko wa kuondokana na hali ya ukosefu wa imani, kiasi cha kutumbukia katika kifo na kuona kwamba, maisha si mali kitu, hali inayowakatisha watu wengi tamaa! Baba Mtakatifu anawataka waamini kugundua ndani mwao lile “Kaburi la Matumaini” ili kumkaribisha Kristo Mfufuka, kwani Mungu si wa wafu, bali wa walio hai! Kamwe waamini wasikubali kuzika matumaini! Jiwe la dhambi ni kizingiti kwa watu wengi, kwani kinarubuni na kuwapatia ahadi kedekede ambazo ziko tayari; dhambi inawahakikishia watu ustawi na mafanikio katika maisha, lakini matunda yake ni utupu na kifo!

Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaachana na dhambi inayoelemea nyoyo zao na hivyo kuweka uzio kwa mwanga wa Mungu kutoweza kupenya! Uzio huu ndio uchu wa fedha na mali, kiburi na majivuno mambo yanayokwenda kinyume kabisa cha Kristo ambaye ni mwanga wa kweli dhidi ya umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko! Baba Mtakatifu anasema zile changamoto ambazo wanawake walikutana nazo pale kaburi ziliwafadhaisha, wakaingiwa na hofu na hatimaye, kuinama kifudifudi hata nchi, kwani waliishiwa nguvu na kukosa ujasiri wa kuinua vichwa vyao. Huu ndio mwelekeo hata kwa waamini wanapokumbana na udhaifu na mapungufu yao, kiasi hata cha kushikwa na woga na hatimaye, kujifungia katika hofu zao, kiasi cha kusahau kwamba, wao ndio wadau wakuu wa hatima ya maisha yao, wakitaka wanaweza kumfungulia Kristo Yesu, nyoyo zao, ili aweze kuwashika mkono na kuwainua tena!

Waamini wanaweza kusimama tena kwa njia ya Neno na imani kwa kutambua kwamba, wameumbwa kwa mambo mazito katika maisha na wala si kwa ajili ya kifo, changamoto na mwaliko wa kumtafuta na kumwambata Kristo Mfufuka! Baba Mtakatifu anawataka waamini kuangalia maisha kama anavyoangalia Mwenyezi Mungu! Katika dhambi anawaona watoto wake wakijitahidi kuinuka tena; katika kifo, wakifufuka tena; katika hali ya kukata tamaa, wakifarijika. Hakuna sababu ya kuogopa kwani Mwenyezi Mungu anapenda maisha ya kila mja wake na kwamba, Pasaka ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu ambao kwa njia ya Kristo Yesu, unapyaisha yote yaani: kifo katika maisha na maombolezo katika sherehe. Kwa njia ya Kristo, waamini wanaweza kujenga na kudumisha: umoja, faraja, imani, matumaini na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ambao kamwe hauwezi kubadilika! Makaburi iwe ni sehemu ya tafakari nzito ya maisha, tayari kuanza mchakato wa kumtafuta Kristo Mfufuka!

Wanawake walifurahishwa sana na Habari Njema kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini na kumbu kumbu hai. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kwenda tena Galilaya ili kupyaisha imani yao, kuonja tena na tena ule upendo wa kwanza, kwa kurejea katika sakafu ya Moyo wake Mtakatifu, kielelezo cha imani ya Pasaka. Hii ni imani inayomshuhudia Kristo Yesu anayekutana na watu wake katika hija ya maisha yao. Yesu daima amewapigania, akashinda kwa niaba yao dhidi ya usiku wa giza, mapambano na dhambi kwa kuwagusa kwa njia ya Neno lake! Baba Mtakatifu anawataka waamini wasipoteze muda mrefu kwa kukaa kaburini, bali wasimame mara, kwenda kukutana na Kristo Mfufuka.

Kwa bahati mbaya, waamini wakati mwingine wanaelemewa zaidi na matatizo yao ambayo kimsingi ni sehemu ya maisha, lakini wakumbuke kwamba, Kristo Mfufuka ni msaada mkubwa katika maisha yao na wakisha kukutana naye, waanze maisha mapya kwa kutembea katika mwanga pasi na kurejea tena makaburini. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake katika Mkesha wa Pasaka kwa kusema, Kristo Mfufuka awe ni kiini cha maisha na kamwe wasikubali kuburuzwa na mawimbi ya maisha, matatizo wala kujikwaa katika jiwe la dhambi litakalowaondolea imani na kuwajengea hofu na woga katika maisha. Waamini wawe na jeuri ya kumtafuta na kumwambata Kristo Mfufuka na kwa njia hii, wataweza hata wao kufufuka pamoja na Kristo!

Papa: Kesha la Pasaka
21 April 2019, 13:42