Tafuta

Vatican News
Serikali ya Ufaransa inasema, ukarabati wa Kanisa kuu la Notre Dame utafanyika kwa kipindi cha miaka mitano kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi wa fedha itakayokusanywa! Serikali ya Ufaransa inasema, ukarabati wa Kanisa kuu la Notre Dame utafanyika kwa kipindi cha miaka mitano kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi wa fedha itakayokusanywa!  (AFP or licensors)

Janga la Moto Kanisa kuu la Notre Dame: Miaka 5 ya Ukarabati!

Rais Emmanuel Macron amesema, Serikali yake inatarajia kwamba, Kanisa kuu la Notre Dame, litaweza kufanyiwa ukarabati kwa muda wa miaka mitano na hivyo kurejea tena katika hali yake yenye mvuto na mguso kwa maisha ya kiroho, kitamaduni na kijamii. Ukarabati huu utazingatia msingi ya ukweli na uwazi katika kupokea na kutumia fedha zitakazochangwa na wadau mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji mkuu wa mpito mjini Vatican amethibitisha kwamba, Jumatano, tarehe 17 Aprili 2019, Baba Mtakatifu Francisko amepokea simu kutoka kwa Rais Donald Trump wa Marekani, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Marekani amependa kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Kanisa Katoliki kutokana na janga la moto lililotokea Jimbo kuu la Paris, Ufaransa na kuteketeza Kanisa kuu la Notre Dame! Ameonesha nia ya Marekani kuchangia katika ukarabati wa Kanisa kuu la Notre Dame.

Papa Francisko anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka kusaidia kuzima moto pamoja na kuokoa mali ya Kanisa. Watu wote hawa wapokee shukrani kutoka kwa Kanisa zima. Kwa njia ya maombezi na tunza ya Bikira Maria, azidi kuwaombea, ili mchakato wa ukarabati wa Kanisa uanze na kusonga mbele kwa haraka kama kielelezo cha shukrani na utukufu kwa Mungu. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema, Serikali yake inatarajia kwamba, Kanisa kuu la Notre Dame, litaweza kufanyiwa ukarabati kwa muda wa miaka mitano na hivyo kurejea tena katika hali yake yenye mvuto na mguso kwa maisha ya kiroho, kitamaduni na kijamii. Ukarabati huu unapaswa kuzingatia msingi ya ukweli na uwazi katika kupokea na kutumia fedha zitakazochangwa na Serikali pamoja na wadau mbali mbali.

Tayari kuna watu wameonesha nia ya kuchangia ukarabati huu, akiwemo Bwana Francois Henri Pinault, Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kering ambaye ameahidi kuchangia zaidi ya Euro milioni moja, sawa na Dola za Kimarekani milioni 110. Kanisa kuu la Notre Dame ni kito cha thamani, utambulisho wa wananchi wa Ufaransa na kivutio kikuu cha majadiliano ya kidini na kiekumene. Bwana Stèphane Bern, mwandishi wa habari anayehamasisha mshikamano katika kuchangia ukarabati wa Kanisa la Notre Dame amesikika akisema, tayari Wasamaria wema wamekwisha kuchangia zaidi ya bilioni moja, tangu kampeni hii ilipoanzishwa, Jumanne.

Wachunguzi wa mambo wanasema, gharama za ukarabari wa Kanisa kuu la Notre Dame zinatakiwa kugharimiwa na Kanisa pamoja na watu binafsi kwa sababu halikuwa limewekewa bima! Serikali ya Ufaransa imezindua kampeni kwa ajili ya waandisi watakaoshughulikia ukarabati wa Kanisa kuu la Notre Dame mintarafu teknolojia na changamoto mamboleo, kadiri ya maelezo yaliyotolewa na Waziri mkuu Edouard Philippe, wakati akizungumza na waandishi wa habari, Jumatano, tarehe 17 Aprili 2019. Ukweli na uwazi ni kati ya mambo ambayo yanafanyiwa kazi kwa sasa kama sehemu ya mchakato wa ukarabati wa Kanisa kuu la Notre Dame.

Papa: Rais Trump
19 April 2019, 11:27