Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika michezo anakazia: Elimu, Malezi na Majiundo makini kwa vijana: Malengo katika maisha; Sadaka na Mshikamano wa kidugu! Papa Francisko katika michezo anakazia: Elimu, Malezi na Majiundo makini kwa vijana: Malengo katika maisha; Sadaka na Mshikamano wa kidugu!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Michezo: Malengo, Sadaka na Mshikamano

Papa Francisko anasema: Wanamichezo wawe ni vyombo vya furaha; mifano bora ya kuigwa; wajenge na kudumisha mafungamano ya kijamii kwa njia ya michezo, kwa kuwaweka mbele ya macho yao, walengwa wakuu wa Shirikisho hili nchini Italia. Moyo wa mshikamano na ushiriki mkamilifu katika michezo ni chachu muhimu sana katika maisha ya kijamii na kitamaduni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Wanamichezo Vijana Kitaifa nchini Italia “Lega Nazionale Dilettanti” linaundwa na timu za wanamichezo vijana zipatazo 12, 000, zenye washabiki waliosajiliwa milioni moja; watu wanaounganishwa na furaha pamoja na ushabiki wa mpira wa miguu; fursa inayowapatia watu burudani, ukuaji wa mwilingiliano wa watu pamoja na ukomavu wa mtu binafsi! Shirikisho hili kwa Mwaka 2019 linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.

Hii ni fursa kwa wajumbe wa Shirikisho hili kuhakikisha kwamba, wanaimarishwa zaidi katika malengo ya Shirikisho hili kwa kumwilisha mafundisho msingi ambayo yamekuwa yakitolewa hadi wakati huu! Shirikisho hili limeweza kuratibu na kuhamasisha mashindano katika ngazi mbali mbali, kiasi cha kuendelea kujipambanua kwa kutoa mchango mkubwa katika mchezo wa mpira wa miguu nchini Italia, hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Michezo kwa vijana ni fursa ya kujipatia elimu, malezi na majiundo makini yanayopaswa kuthaminiwa na kudumishwa.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 15 Aprili 2019 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Wanamichezo Vijana Kitaifa nchini Italia. Baba Mtakatifu anakaza kusema muktadha wa kitamaduni na kijamii pamoja na mabadiliko na changamoto zake zina athari kwa watu wote, lakini waathirika wakuu ni vijana wa kizazi kipya. Ni mabadiliko yanayowataka watu kwenda mchakamchaka ili kuridhika, lakini katika hali na mazingira kama haya, matokeo yake ni kuacha utupu katika nyoyo za watu na muda unakuwa hauna tena malengo maalum!

Baba Mtakatifu anawataka wanamichezo kusimama na kufanya tafakari ya kina na kupambanua malengo na hatimaye, kusimama na kuendelea na mchakamchaka wa maisha, ili kufikia lengo maalum pamoja na kutambua kwamba, kushinda au kushindwa ni sehemu ya mchezo wenyewe! Mchakato wa kuweka bayana malengo ni endelevu kwa kutambua kile kinachotendeka kwa kadiri ya nyenzo zilizopo, ili kuweza kufikia matokeo yanayokusudiwa! Michezo inahitaji: mambo ya kiufundi, mazoezi, hali ya kuthubutu, uvumilivu kwa kukubali kushinda au kushindwa; kwa kujenga na kudumisha ari, sadaka na moyo wa kufanya kazi kwa pamoja na kama timu sanjari na kuwa ni mtu mwenyewe furaha na mwelekeo chanya wa maisha!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mchezaji mahiri anapaswa kuwa na sifa kede kede, si tu kwa kufunga goli, au kuwapiga chenga wapinzani wake. Bali anapaswa kuonesha nidhamu kwa kuzungumza kwa amani na utulivu na mwamuzi wa mchezo au wapinzani wake, kwa kukubali pia adhabu pale anaponawa mpira. Yote haya ni mambo muhimu sana yanayoendelezwa na kukuzwa na Shirikisho la Wanamichezo Vijana Kitaifa nchini Italia. Shirikisho linawataka wanachama wake kuheshimu sheria, taratibu na kanuni za michezo ili kuwa uwiano mzuri katika michezo “fair play”; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu. Haya ni mambo yanayomtaka mwanamichezo kujitawala na kudumisha nidhamu inayopatikana kwa mazoezi ya ndani, kwa kuboresha maisha ya kiroho na kimwili; kwani mwanadamu ameumbwa: mwili na roho; mambo yanayopaswa kushughulikiwa kikamilifu.

Michezo inayo nafasi ya pekee katika ustaarabu wa maisha ya mwanadamu kwa kupima umuhimu wa tukio lenyewe katika uhuru kamili. Mwelekeo huu unafumbatwa katika kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za michezo, uzuri na furaha ya kukutana na wengine, ili kupimana nguvu. Baba Mtakatifu anawataka wanamichezo vijana watakapokuwa maarufu kwa kutandaza kabumbu uwanjani kukumbuka kwamba furaha ndiyo inayonogesha michezo, badala ya kutamani ushindi na kuwabeza wengine. Wamamichezo watakapofikia hatua hii watambue kwamba, wamekuwa na kukomaa! Wanamichezo wawe ni vyombo vya furaha; mifano bora ya kuigwa na vijana wenzao; wajenge na kudumisha mafungamano ya kijamii kwa njia ya michezo na mshikamano, kwa kuwaweka mbele ya macho yao, walengwa wakuu wa Shirikisho la Wanamichezo Vijana Kitaifa nchini Italia.

Moyo wa mshikamano na ushiriki mkamilifu katika michezo ni chachu muhimu sana katika maisha ya kijamii na kitamaduni! Hapa kunamaanisha ni kumsaidia kunyanyuka mwanamichezo mwenzako aliyeanguka, aliyetendewa kosa au ambaye ameumia! Lengo ni kudumisha umoja na mshikamano wa kijamii kwa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kwa dhati kabisa pasi na makunyanzi. Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu anakaza kusema wa mwisho watakuwa wa kwanza na kwanza watakuwa wa mwisho, kwa kukazia upendo na wema kwa watu wote; kwa kujifunza kuona na kufurahia uzuri hata katika mambo madogo madogo; kwa kukubali karama na mapungufu yao katika hali ya utulivu.

Haya ndiyo mambo ambayo wanamichezo wanapaswa kuyakuza na kuyadumisha ndani mwao, chachu ya mabadiliko makubwa kijamii. Hii ni changamoto ya kuendelea kutunza mazingira nyumba ya wote, kuondoa kuta za utengano, kwa kuwashirikisha wote ili kujenga ari na moyo wa kufanya kazi kama timu, kwani haya ndiyo matumaini halisi ya binadamu! Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka wanamichezo kuwa na malengo ili waweze kuwa mahiri katika michezo kwa kuzingatia ukweli wa maisha na kujenga urafiki!

Papa: Wanamichezo
15 April 2019, 14:45