Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amekutana na kuzungumza na kijana Greta Thunberg na kumpongeza kwa kusimama kidete kutetea mazingira nyumba ya wote! Papa Francisko amekutana na kuzungumza na kijana Greta Thunberg na kumpongeza kwa kusimama kidete kutetea mazingira nyumba ya wote!  (Vatican Media)

Papa Francisko ampongeza Kijana Greta kwa ujasiri wake!

Baba Mtakatifu Francisko amemtia shime Kijana Greta Thunberg kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu bila kukata tamaa. Na Greta kwa upande wake, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujipambanua katika kulinda, kutetea na kudumisha mazingira bora kwa wote! Kijana Greta anaendelea kujipambanua kuwa ni kijana mkereketwa wa utunzaji bora wa mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anasema hii ni dira na mwongozo wa maisha kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Ni mwaliko wa kufanya toba na wongofu wa kiekolojia ili kukuza na kudumkisha ekolojia fungamani, inayowataka watu kuishi kwa furaha na katika ukweli, kwa kutambua kwamba, kuna uhusiano wa karibu sana kati ya mazingira, haki kwa maskini, amani na utulivu wa ndani, kiasi kwamba, kilio cha Dunia Mama ni sawa na kilio cha maskini duniani!

Baba Mtakatifu katika Waraka huu anagusia kuhusu haki kati ya vizazi na hatima ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira kwa vizazi vijavyo. Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee umuhimu: mshikamano kati ya vizazi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; dira, maana na tunu msingi zinazopaswa kuzingatiwa. Lengo la maisha, kikomo cha kazi! Je, vijana wa kizazi kipya wataachiwa kitu gani kwa siku za usoni? Kifusi, mahame na takataka? Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutafakari wajibu wake ili kukabiliana na athari hizi kwa siku za usoni!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, tarehe 17 Aprili 2019 alikutana na kuzungumza na Kijana Greta Thunberg, mwenye umri wa miaka 16 kutoka Sweden, ambaye alianza na mgomo kwa kusimama mbele ya Bunge la Sweden na hatimaye, akaweza kupata fursa ya kusikilizwa na wakuu mbali mbali wa nchi pamoja na Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu amemtia shime Kijana Greta kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu bila kukata tamaa. Na Greta kwa upande wake, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujipambanua katika kulinda, kutetea na kudumisha mazingira bora kwa wote!

Baba Mtakatifu anawachangamotisha walimwengu kushikamana kwa dhati ili kuweza kuzikabili changamoto hizi kwa umoja, kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo vya Mwenyezi Mungu katika utunzaji bora wa mazingira na kwamba, hii ni sehemu ya Injili ya Kazi ya Uumbaji, kielelezo makini cha umoja na mafungamano ya kijamii kati ya binadamu ambayo yamekita mizizi yake katika: Uhusiano na Mwenyezi Mungu; Uhusiano na Jirani na hatimaye, Uhusiano na dunia yenyewe. Mwanadamu amejeruhiwa kwa dhambi ya asili na matokeo yake yanayojionesha ardhini, majini, hewani na katika aina mbali mbali za mifumo ya maisha sanjari na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Changamoto hizi zinahitaji kwa namna ya pekee kabisa mageuzi kuhusu mtazamo wa maendeleo endelevu ya binadamu, uratibu wa shughuli za kiuchumi pamoja na mitindo ya maisha. Mafundisho ya Kanisa kuhusu kazi ya uumbaji yanakazia kwamba, kama ulivyo uumbaji hata maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini kwa bahati mbaya, mwanadamu anaelemewa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kazi ya uumbaji ni hatua ya kwanza katika wito wa mwanadamu yaani: Uumbaji, Umwilisho na Ukombozi.

Papa: Greta Thurnberg
19 April 2019, 11:43