Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amewapongeza wanakwaya mchanganyiko kutoka Bonheiden, Ubelgiji kwa upendo, mshikamano na faraja kwa wazee! Papa Francisko amewapongeza wanakwaya mchanganyiko kutoka Bonheiden, Ubelgiji kwa upendo, mshikamano na faraja kwa wazee! 

Papa Francisko awataka vijana kuchota utajiri kutoka kwa wazee!

Papa Francisko amepata nafasi ya kusalimiana na Kwaya mchanganyiko kutoka Bonheiden, nchini Ubelgiji inayowatunza wagonjwa wa “Alzheimer”. Papa anamshukuru Mungu kuweza kumpatia nafasi ya kukutana na kundi la watu kama hawa, wanaoimba, huku wakifarijiana na kusindikizana katika mahangaiko ya ugonjwa wao, ili kupeana faraja na kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza Katekesi yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano, tarehe 3 Aprili 2019, amepata nafasi ya kukutana na kusalimiana na Kwaya mchanganyiko kutoka Bonheiden, nchini Ubelgiji inayowatunza wagonjwa wa “Alzheimer”. Baba Mtakatifu anasema, anamshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kumpatia nafasi ya kukutana na kundi la watu kama hawa, wanaoimba, huku wakifarijiana na kusindikizana katika mahangaiko ya ugonjwa wao, ili kupeana faraja na kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, wimbo wao umekuwa na maana kubwa zaidi, hata kuliko mateso na mahangaiko yao, kwani ni wimbo ambao umetolewa kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kutumia hali zao, kielelezo cha upendo na huruma. Hii ni changamoto ya kuwaheshimu na kuwathamini wazee ambao wanahifadhi kumbu kumbu ya maisha. Pengine, kati ya wazee hawa kuna baadhi yao wamepoteza kumbu kumbu, lakini wao wenyewe ni sehemu ya mizizi ya kumbu kumbu na vijana wanapaswa kujifunza kutoka kwenye hazina hii ambayo ni wazee wa sifa. Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume na baadaye kusalimiana na kila mmoja wao, kama baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu!

Papa: Wagonjwa
03 April 2019, 15:51