Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anampongeza Askofu mkuu Giancarlo Maria Bregantini kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya kuwekwa wakfu kama Askofu Papa Francisko anampongeza Askofu mkuu Giancarlo Maria Bregantini kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya kuwekwa wakfu kama Askofu  (Vatican Media)

Papa Francisko: Jubilei ya Miaka 25 ya Ukaskofu: Bregantini

Askofu mkuu Giovani Bregantini, alipewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1978, akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Locri-Gerace na kwa sasa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Campobasso-Bojano. Alitoa wakati wa Njia ya Msalaba, Ijumaa kuu ya Mwaka 2014. Familia ya Mungu inajivunia kuwa na kiongozi kama yeye, anayethubutu kuyatafakari Madonda ya Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu ni alama ya utimilifu wa Daraja Takatifu ambamo anapewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni dhamana inayofumbatwa katika unyenyekevu na upendo. Askofu anao wajibu wa kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha Ibada na Uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Utume huu, umwezeshe Askofu kuwa kiongozi mkarimu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu ili kuendeleza kazi ya ukombozi. Askofu anapaswa kuratibu maisha na utume wa Kanisa, daima akimwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kumwongoza na kumsimamia. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Mtaguso Mkuu wa kwanza wa Yerusalemu, ulioweka mambo sawa na Injili ya Kristo ikasonga mbele na kuenea sehemu mbali mbali za dunia! Hii ndiyo dhamana inayopaswa kutekelezwa hata na Maaskofu wa sasa katika ulimwengu mamboleo!

Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe wa pongezi na matashi mema, Askofu mkuu Giovani Carlo Maria Bregantini, C.S.S., ambaye hapo tarehe 7 Aprili 2019 amekumbukia Jubilei ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Anamshukuru na kumpongeza kutokana na ari na mwamko wake wa shughuli za kichungaji. Amekuwa chombo na shuhuda wa huduma makini kwa maskini; akajifunga kibwebwe kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, na kwa hakika amekuwa ni chemchemi ya udugu na alama ya neema ya Mungu.

Baba Mtakatifu anayaangalia maisha ya Askofu mkuu Giovani Carlo Maria Bregantini, tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1978, akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Locri-Gerace na hatimaye kwa sasa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Campobasso-Bojano. Anamkumbuka kwa tafakari ya kina, aliyoitoa wakati wa Njia ya Msalaba, Ijumaa kuu ya Mwaka 2014 kuzunguka Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma. Baba Mtakatifu anakaza kusema, familia ya Mungu inajivunia kuwa na kiongozi kama yeye, anayethubutu kuyatafakari Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu yanayoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo; kwa kusikiliza kilio cha maskini na kukipatia majibu muafaka kwa wakati wake!

Huu ni ushuhuda wa maisha yanayosimikwa katika upendo wa udugu wa Kikristo! Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kusema, wakati huu anapompongeza kwa matendo makuu yaliyojitokeza katika maisha na utume wake, anazidi kumwombea ili Mwenyezi Mungu, aendelee kumtunza Askofu mkuu Bregantini, Kondoo walioko chini yake pamoja na kazi njema anazotenda na kwamba, aendelee daima kuwa na ari na moyo mkuu katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anatoa baraka zake za kitume kwa Askofu mkuu Bregantini, wakleri pamoja na watu wote wa Mungu Jimbo kuu la Campobasso-Bojano.

Askofu Mkuu Bregantini
08 April 2019, 09:07