Tafuta

Vatican News
Wosia wa Kitume, Sinodi ya Vijana 2018: "Vive Cristo, esperanza nuestra" yaani "Muishi Kristo, Tumaini letu" ni Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana wa kizazi kipya! Wosia wa Kitume, Sinodi ya Vijana 2018: "Vive Cristo, esperanza nuestra" yaani "Muishi Kristo, Tumaini letu" ni Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana wa kizazi kipya!  (AFP or licensors)

Wosia wa Kitume: Sinodi ya Vijana 2018: Loreto kumekucha!

Tarehe 25 Machi 2019 kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, Baba Mtakatifu Francisko atatia mkwaju kwenye Wosia wa Kitume baada ya Sinodi ya Maaskofu unaoongozwa na kauli mbiu “Vive Cristo, esperanza nuestra” yaani “Muishi Kristo, Tumaini letu” ambao kwa mara ya kwanza umeandikwa kwa lugha ya Kihispania. Wosia huu wa kitume ni safari ndefu iliyoanza 2017.

Na Padre richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 25 Machi 2019, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Hapa Kanisa linatafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu na kukaa kwake Bikira Maria ambaye amekuwa kweli ni Tabernakulo ya kwanza. Yesu mwenyewe katika maisha na utume wake, alitoa kipaumbele cha pekee kwa watoto wadogo, maskini na wagonjwa. Mkristo anaalikwa kwa namna ya pekee kulitafakari Fumbo la Umwilisho kwa kumwangalia mwanadamu anayepewa upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu pamoja na kukombolewa na Yesu Kristo kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu!

Tarehe 25 Machi 2019 kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, Baba Mtakatifu Francisko atatia mkwaju kwenye Wosia wa Kitume baada ya Sinodi ya Maaskofu unaoongozwa na kauli mbiu “Vive Cristo, esperanza nuestra” yaani “Muishi Kristo, Tumaini letu” ambao kwa mara ya kwanza umeandikwa kwa lugha ya Kihispania. Wosia huu wa kitume ni safari ndefu iliyoanza kunako mwaka 2017 Baba Mtakatifu alipowaandikia vijana barua, kukafuatia semina ya kimataifa kuhusu hali ya vijana duniani; Mwezi Machi 2018 vijana waakaadhimisha utangulizi wa Sinodi uliohitimishwa katika maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, Siku ya Vijana Kijimbo. Mwezi Juni, 2018 kukachapishwa hati ya kutendea kazi na Mwezi Oktoba, 2018 maadhimisho na hatimaye, Mababa wa Sinodi wakatoa hati baada ya Sinodi. Januari, 2019, Kanisa likaadhimisha Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani na Machi 2019, Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Vive Cristo, esperanza nuestra” yaani “Muishi Kristo, Tumaini letu”.

Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake anasema, kuna uhusiano wa karibu kati ya Fumbo la Umwilisho na utume wa familia. Kadiri ya mpango wa Mungu, Yesu Kristo alizaliwa na kukulia katika familia ya binadamu iliyoundwa na Yosefu pamoja na Bikira Maria. Kanisa linapoadhimisha Siku ya Uhai, linapenda kukazia umuhimu wa: maisha, utu na heshima ya kila binadamu tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, tangu mwanzo, Mwenyezi Mungu alipenda kuibariki familia na kuipatia dhamana ya kuendeleza kazi ya uumbaji; ili kweli iweze kuwa ni Jumuiya ya maisha na kitalu cha upendo katika moyo wa jamii.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuna uhusiano wa pekee kabisa kati ya Kanisa na Familia. Mama Kanisa anayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, anazisindikiza na kuziunga mkono familia, hasa zile zinazokabiliwa na matatizo na changamoto mbali mbali za maisha.  Familia ni kwa ajili ya mafao ya wengi, changamoto kwa waamini kukuza dhamana hii ndani ya: Familia, Kanisa na Jamii katika ujumla wake pamoja na kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali kwa ari na moyo mkuu. Bikira Maria, Mama wa Mkombozi awe ni chemchemi ya furaha na faraja kwa wanafamilia wote.

Kuna uchungu mkubwa kwa mama anapompoteza mtoto wake. Kwa wanawake wanaotoa mimba, madhara yake ni makubwa katika maisha yao. Haiwezekani sheria kuhalilisha vifo vya watoto wachanga kwa njia ya utoaji mimba, kwani kufanya hivi ni kwenda kinyume cha haki msingi za binadamu. Kuna haja kwa Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujenga na kuendeleza utamaduni wa Injili ya Uhai kwa kuwasaidia wanawake kutambua sura na mfano wa Mungu unaojionesha katika maisha ya watoto wao, hata kabla ya kuzaliwa. Ni changamoto ya kukataa katu katu kukumbatia utamaduni wa kifo, bali wanawake wawe mstari wa mbele kutangaza Injili ya Uhai kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao ya kila siku.

Wosia wa kitume

 

23 March 2019, 16:00