Cerca

Vatican News
Muswada wa Katiba Mpya "Predicate evangelium" unaendelea kuboreshwa zaidi mintarafu "Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa" Muswada wa Katiba Mpya "Predicate evangelium" unaendelea kuboreshwa zaidi mintarafu "Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa"  (ANSA)

Muswada wa Katiba Mpya ya Kitume unaendelea kuboreshwa!

Muswada wa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili uliowasilishwa kwa mara ya kwanza katika mkutano uliopita. Makardinali washauri wameangalia vipengele vya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Makardinali wametoa pia mwongozo unaopaswa kutumiwa kwa ajili ya kutoa ushauri na maoni kwa kuzingatia “dhana ya Sinodi".

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo ndani ya Kanisa uliofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019, lilikuwa ni tukio la kihistoria ambalo licha ya kuwashirikisha Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakuu wa Makanisa, Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, lakini pia walishiriki Makatibu wakuu pamoja na Makatibu wambata kutoka Mabaraza mbali mbali ya Kipapa. Ikumbukwe kwamba, Makatibu, mara nyingi ndio watekelezaji wakuu wa maamuzi yanayofikiwa kwenye vikao na mikutano mbali mbali.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji mkuu wa muda wa Vatican, alipokuwa anatoa kwa muhtasari marejesho ya Mkutano wa 28 Makardinali washauri uliofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019 kwa ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko. Mkutano huu kwa namna ya pekee kabisa, umeendelea kuchambua Muswada wa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” uliowasilishwa kwa mara ya kwanza katika mkutano uliopita. Makardinali washauri wameangalia vipengele vya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa.

Makardinali wametoa pia mwongozo unaopaswa kutumiwa kwa ajili ya kutoa ushauri na maoni kwa kuzingatia “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”, changamoto ambayo kwa sasa inavaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa kama inavyoshuhudiwa katika mchakato wa kushughulikia changamoto za Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Imeamriwa kwamba, Muswada huu utapelekwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Sinodi za Maaskofu wa Makanisa ya Mashariki, Mabaraza ya Kipapa, Mashirikisho ya Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na baadhi ya Vyuo Vikuu vya Kipapa.

Baraza la Makardinali lilipata pia nafasi ya kumsikiliza Padre Federico Lombardi, SJ., Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger/Benedikto XVI, ambaye alikuwa ni Mratibu wa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo ndani ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, uamuzi wa kuitisha mkutano huu ni maamuzi yaliyotolewa na Baraza la Makardinali Washauri katika Kikao chake cha XXVI, kilichofanyika kuanzia tarehe 10- 12 Septemba 2018.

Makardinali wamekiri kwamba, tukio hili ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu mchakato wa ulinzi na usalama wa watoto wadogo. Kanisa linataka kuhakikisha kwamba, linajenga mazingira bora na salama kwa malezi na makuzi ya watoto wadogo. Makardinali wametafakari kwa kina na mapana kuhusu uamuzi wa Kanisa wa kumvua mamlaka na haki ya kuishi kama Padre, aliyekuwa Kardinali Theodore McCarrick, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Washington DC., nchini Marekani. Baraza la Makardinali litakuwa na mkutano wake wa XX1X kuanzia tarehe 8-10 Aprili 2019.

Baraza la Makardinali Washauri
01 March 2019, 13:44