Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anakazia umuhimu wa Wakristo kunenga na kudumisha uekumene wa huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Papa Francisko anakazia umuhimu wa Wakristo kunenga na kudumisha uekumene wa huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!  (AFP or licensors)

Hija ya Papa Francisko Morocco: Uekumene wa huduma ya upendo!

Papa Francisko anasema, Wakristo wanaitwa na kutumwa ulimwenguni ili kujenga Ufalme wa Mungu pamoja na kuyachachusha malimwengu kwa Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu pamoja na Amri ya upendo wa kidugu. Kwa ufupi, hii ndiyo Injili ya huduma ya upendo, utambulisho na ushuhuda wenye mvuto na mashiko sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Morocco inajikita katika mambo makuu matatu: majadiliano ya kidini; huduma kwa maskini yaani wakimbizi na wahamiaji pamoja ushuhuda wa imani kutoka kwa waamini nchini Morocco! Baba Mtakatifu ameianza Jumapili, tarehe 31 Machi 2019 kwa kukutana na wakleri, watawa pamoja na wajumbe wa Baraza la Makanisa nchini Morocco kama ushuhuda wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika majadiliano ya kiekumene. Wakristo wanaitwa na kutumwa ulimwenguni ili kujenga Ufalme wa Mungu pamoja na kuyachachusha malimwengu kwa Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu pamoja na Amri ya upendo wa kidugu. Kwa ufupi, hii ndiyo Injili ya huduma ya upendo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, utume huu, haujalishi idadi wala ukubwa wa eneo, bali ule uwezo wa kuleta mabadiliko kwa mshangao unaofumbatwa katika furaha na matumaini, uchungu na fadhaa. Huu si utume wa wongofu shuruti, bali unaokita mizizi yake katika mahusiano kati ya wakristo na Yesu pamoja na jirani zao, ili kweli waweze kuwa ni nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia. Ukristo ni sehemu ya mchakato wa watu kukutana katika upendo, kwa kutambua kwamba, wao wamependwa kwanza na Mwenyezi Mungu na kwa jinsi hii nao pia wanapaswa kupenda kama Kristo Yesu alivyowapenda na kwa jinsi hii, wataweza kutambulikana kuwa ni wafuasi wa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kila mmoja kadiri ya wito na utume wake, kuhakikisaha kwamba analisaidia Kanisa kukuza na kudumisha majadiliano, kama sehemu ya ujumbe na utekelezaji wa uaminifu wao kwa Mwenyezi Mungu ambaye katika wema, hekima na upendo wake usio na mipaka anaongea na wanadamu kama na rafiki na hivyo Mwenyezi Mungu anawaalika kushiriki kikamilifu katika urafiki wake. Tangu mwanzo wa Ubatizo wao, Wakristo wanaalikwa kushiriki katika majadiliano ya wokovu na urafiki. Wakristo wanapaswa kuwa ni Sakramenti hai ya majadiliano na watu wanaoishi katika medani mbali mbali za maisha, katika hali ya unyenyekevu na upendo; kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokwenda na kukutana na Sultan Al Malik Al Kamil.

Huu ndio mfano ulioachwa na Mwenyeheri Charles de Foucault, aliyemwabudu Yesu wa Nazareti katika ukimya, changamoto na mwaliko wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Majadiliano ni sehemu ya vinasaba na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Baba wa wote! Majadiliano ya wokovu ni dhamana na wajibu ambao wamekabidhiwa wakleri na watawa, kwa ajili ya watu wa Mungu kwa njia ya sala kwa ajili ya upendo kwa jirani; ni sala inayobeba maisha ya watu wao ili kuyatolea Altareni, ili yaweze kubarikiwa na Roho Mtakatifu na kwa jinsi hii, wanaweza kuendelea kusali kwa pamoja huku wakisema, “Baba Yetu uliye mbinguni”.

Haya ni majadiliano yanayogeuka kuwa ni sala ya udugu wa kibinadamu unaotaka kuvunjilia mbali utengano, sera za ukinzani na chuki pamoja na uchu wa mali. Ni sala inayojiaminisha katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa njia ya upendo na wala si kwa nguvu kiuchumi, kidini na ukabila. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wakristo nchini Morocco wanaoendeleza majadiliano ya kidini, kwa kushirikiana katika urafiki, ili kupandikiza mbegu ya matumaini kwa watu wote. Kwa njia hii, wataweza “kufyekelea mbali” kishawishi cha kutaka kutumia tofauti msingi na ujinga wa watu kwa ajili ya kupandikiza woga, chuki na mipasuko mbali mbali, mambo ambayo yanayoweza kusababisha majanga katika jamii!

Wakristo wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yao, ili wapate kuwa matajiri kwa umaskini wake. Huu ni mwaliko wa kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa njia ya uekumene wa huduma ya upendo; kwa njia ya majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, kama ndugu wamoja. Wakristo wawe mstari wa mbele katika majadiliano kwa kujipambanua katika huduma ya haki na amani; elimu, ustawi na maendeleo ya maskini.

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwasalimia wakleri, watawa na waamini wazee na wagonjwa ambao hawakupata bahati ya kuja kukutana naye mubashara, lakini wanamsindikiza kwa njia ya sala. Daima wakumbuke kwamba, wao ni mashuhuda wa historia inayoendelea kutukuka kutokana na sadala yao, inayopaswa kuendelezwa mbele kwa imani na matumaini makubwa! Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa wakleri, watawa na wajumbe wa Baraza la Makanisa nchini Morocco kwa kusali pamoja Sala ya Malaika wa Bwana!

Papa: Uekumene wa huduma
31 March 2019, 12:53