Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019 anafanya hija ya 28 ya Kitume Kimataifa huko Morocco: Kauli mbiu "Papa Francisko mhudumu wa matumaini". Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019 anafanya hija ya 28 ya Kitume Kimataifa huko Morocco: Kauli mbiu "Papa Francisko mhudumu wa matumaini".  (AFP or licensors)

Hija ya Papa Francisko nchini Morocco: Mhudumu wa matumaini

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019 anafanya hija ya 28 ya kimataifa nchini Morocco kwa kuongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mhudumu wa matumaini Morocco 2019”. Akiwa nchini Morocco atakutana na kuzungumza na viongozi wa serikali na wanadiplomasia; wakleri, watawa na viongozi wa Makanisa na ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II kwa mara ya kwanza katika historia, alitembelea nchini Morocco kunako mwaka 1985 wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Vijana Duniani. Hii ilikuwa ni fursa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kukutana na kuzungumza na vijana wa dini ya Kiislam waliokuwa wameungana na vijana wenzao kutoka Kanisa Katoliki! Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019 anafanya hija ya 28 ya kimataifa nchini Morocco kwa kuongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mhudumu wa matumaini Morocco 2019”.

Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa serikali, vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia. Atatembelea Taasisi ya Kidini ya Mohammed VI inayotoa mafunzo kwa viongozi na wahubiri wa dini ya Kiislam. Hii itakuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na wahamiaji na wakimbizi wanaohudumiwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Rabat, Morocco. Kama kielelezo cha huduma ya upendo na mshikamano, Baba Mtakatifu atatembelea kwa faragha Kituo cha Huduma za Kijamii Vijijini, kilichoanzishwa na Mtakatifu Luisa de Marillac pamoja na Mtakatifu Vincent wa Paulo kunako mwaka 1633.

Kanisa linathamini mchango na huduma inayotolewa na wakleri pamoja na watawa nchini Morocco kama vyombo vya mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hawa nao watapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu ili kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Maaskofu wa Morocco watapata chakula cha mchana na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili na baadaye alasiri, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Mfalme Moulay Abdella. Ibada ya Misa Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa na kwa Ibada hii ya Misa, Baba Mtakatifu atakuwa anakunja vilago vya hija yake ya 28 Kimataifa nchini Morocco! Ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Mfalme Mohammed VI pamoja na Maaskofu Katoliki nchini Morocco, kutembelea nchini mwao kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutembelea mji wa Rabat na Casablanca.

Baba Mtakatifu anatembelea nchini Morocco kama kiongozi wa kiroho, mjumbe wa amani na matumaini yanayowawezesha watu kujenga sanaa na utamaduni wa kukutana katika ukweli na haki, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa Katoliki nchini Morocco lina idadi ndogo sana ya waamini, lakini linaendelea kuwa ni shuhuda wa Habari Njema ya Wokovu na wajenzi wa Ufalme wa Mungu. Hija hii ya kitume inaonesha upendeleo wa pekee wa Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini wanaoishi pembezoni mwa vipaumbele vya jamii na hata wakati mwingine vile vya Kanisa! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna jumla ya wakatoliki 30, 000 nchini Morocco. Kama alivyoamua kwenda Armenia nchi ndogo sana machoni pa watu wa Mataifa, ndivyo pia ameamua kwenda Morocco, nchi ambayo ina waamini wengi wa dini ya Kiislam, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anatembelea nchini Morocco ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo pamoja na kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Wakristo. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Morocco kunako mwaka 1985, kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inalenga kuwapatia watu wa Mungu nchini Morocco baraka; imani na matumaini anasema Askofu mkuu Cristobal Lopez wa Jimbo kuu la Rabat nchini Morocco katika barua yake ya kichungaji kwa familia ya Mungu nchini humo, kama sehemu ya maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Morocco.

Huu ni ujumbe wa matumaini hasa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Morocco ambao, wakati mwingine ni wapita njia kama wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora Barani Ulaya. Baba Mtakatifu anakwenda nchini Morocco kama chombo na shuhuda wa majadiliano ya kidini, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, chachu muhimu sana ya maendeleo endelevu na fungamani; utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo yake vikipewa kipaumbele cha kwanza. Mfalme Mohammed VI wa Morocco naye anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kidini. Itakuwa ni nafasi kwa Baba Mtakatifu Francisko walau kukutana na kuzungumza na familia ya Mungu nchini Morocco, ili kuonja wema na ukarimu wao, kufahamu walau historia ya nchi yao, ili kuwatia shime, kusali pamoja nao na hatimaye, kuwapatia baraka zake za kitume.

Askofu mkuu Cristobal Lopez anakaza kusema, hija ya Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, inapania kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini pamoja na taifa la Mungu nchini humo katika ujumla wake. Kwa mara nyingine tena, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko utasaidia kuimarisha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa njia yake, kuendelea kulidumisha Kanisa: moja, takatifu, katoliki na la mitume. Familia ya Mungu nchini Morocco inapenda kuchukua fursa hii tangu wakati huu kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao, mwezi Machi, 2019. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa kujiandaa kikamilifu, kiroho na kimwili, ili kuweza kumpokea mjumbe wa imani, matumaini na mapendo anayewatembelea nchini mwao. Maandalizi haya pia ni sehemu ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo!

Papa Morocco 2019

 

 

27 March 2019, 10:01