Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawashukuru wale wote waliojisadaka kufanikisha hija yake ya kitume nchini Morocco! Papa Francisko anawashukuru wale wote waliojisadaka kufanikisha hija yake ya kitume nchini Morocco!  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko Morocco: Shukrani za dhati kabisa!

Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kufanya hija hii ya kitume nchini Morocco kwa kuwa pamoja na kati yao kama mhudumu wa matumaini! Baba Mtakatifu anamshukuru Mfalme Mohammed VI kwa mwaliko wake pamoja na kuwashukuru wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza, ili kuhakikisha kwamba, hija hii ya kitume inafanikiwa kikamilifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima, wakati wa hija yake ya kitume nchini Morocco, Jumapili tarehe 31 Machi 2019, ametumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kufanya hija hii ya kitume nchini Morocco kwa kuwa pamoja na kati yao kama mhudumu wa matumaini! Baba Mtakatifu anamshukuru Mfalme Mohammed VI kwa mwaliko wake pamoja na kuwashukuru wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza, ili kuhakikisha kwamba, hija hii ya kitume inafanikiwa kikamilifu!

Baba Mtakatifu amewashukuru wakleri, watawa na waamini walei nchini Morocco wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa nchini Morocco. Anawashukuru wale wote waliomsindikiza kwa sala na sadaka zao katika hija hii ya kitume nchini Morocco, kiasi cha kumwezesha kushirikishana na watu wa familia ya Mungu nchini Morocco: imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wakristo nchini Morocco wawe ni vyombo, mashuhuda na wahudumu wa matumaini ambayo, kimsingi ndiyo kiu ya walimwengu kwa wakati huu!

Papa: shukrani
31 March 2019, 17:49