Tafuta

Vatican News
Hotuba ya Papa Francisko kwa viongozi wa Serikali na wanadiplomasia: Majadiliano ya kidini, Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji na mchango wa Kanisa nchini Morocco! Hotuba ya Papa Francisko kwa viongozi wa Serikali na wanadiplomasia: Majadiliano ya kidini, Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji na mchango wa Kanisa nchini Morocco!  (AFP or licensors)

Hija ya Papa Francisko Morocco: Hotuba kwa watu wa Mungu Morocco

Papa Francisko amekazia umuhimu wa majadiliano ya kidini ili kujenga udugu wa kibinadamu; uhuru wa kidini; utunzaji bora wa mazingira pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Amegusia kuhusu mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Morocco! Amewashukuru wananchi wa Morocco kwa ukarimu wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 30 Machi 2019 ameanza hija ya 28 ya kimataifa nchini Morocco inayoongozwa kauli mbiu “Papa Francisko mhudumu wa matumaini Morocco 2019”. Baba Mtakatifu anafanya hija hii kama hujaji wa amani, udugu na mahudumu wa matumaini! Hija hii inajikita katika mambo makuu matatu: majadiliano ya kidini; huduma kwa maskini yaani wakimbizi na wahamiaji pamoja ushuhuda wa imani kutoka kwa waamini nchini Morocco!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa familia ya Mungu nchini Morocco, viongozi wa Serikali, wawakilishi wa vyama kiraia pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchini zao nchini Morocco: amekazia umuhimu wa majadiliano ya kidini ili kujenga udugu wa kibinadamu; uhuru wa kidini; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kumshukuru Mfalme Mohammed VI kwa niaba ya watu wa Mungu nchini Morocco kwa mwaliko wa kutembelea Morocco na kwa hakika ameshuhudia ukarimu wa familia ya Mungu nchini Morocco.

Baba Mtakatifu anasema, hija hii ya kitume ni fursa kwake kugundua utajiri na tamaduni za watu wa Morocco, tayari kusonga mbele katika mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na kuzungumza na Sultan Al Malik Al Kamil. Hili ni tukio linalodhihirisha ujasiri wa watu kukutana, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini, chuki na uhasama vinavyosababisha mipasuko na uharibifu mkubwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, waamini wakiheshimiana na kushirikiana, wataweza kujenga urafiki wa kweli na hatimaye, kujenga mazingira ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kizazi kijacho!

Baba Mtakatifu anasema, Morocco ni daraja kati ya Bara la Afrika na Ulaya, changamoto na mwaliko wa kujenga na kudumisha utandawazi wa mshikamano, unaofumbatwa katika uaminifu na ujasiri mambo msingi katika mchakato wa majadiliano unaoheshimu amana na utajiri wa watu na ule wa mtu mmoja mmoja! Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na wote, na hasa wakati huu ambapo kuna hatari kubwa ya kumezwa na tabia ya kutowajali wala kuwathamini watu wengine, kutokana na uadui na hali ya dunia kuendelea kusambaratika!

Kumbe, kuna haja ya kujenga jamii ambayo iko wazi, yenye mwingiliano na mshikamno; maendeleo na ujenzi wa majadiliano yanayowawezesha watu kufahamiana kwa kutumia mbinu na vigezo hizi. Waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa kuvunjilia mbali tabia ya kinzani, kutoelewana; hali ya kudhaniana vibaya, woga na misigano isiyokuwa na tija wala mashiko, ili kufungua njia mpya inayofumbatwa katika ushirikiano pamoja na kuheshimiana. Kuna haja ya kusimama kidete kupambana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kujenga mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali kwa kufanya rejea kwenye tunu msingi za maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu anasema, ndiyo maana anayo furaha ya kutembelea Taasisi ya Mohammed VI inayotoa mafunzo kwa viongozi na wahubiri wa dini ya Kiislam. Hii ni taasisi ambayo ilianzishwa na Mfalme Mohammed VI, ili kutoa mafunzo muhimu yatakayowasaidisa viongozi wa kidini kuondokana na misimamo mikali ya kiimani, ambayo imekuwa ni chimbuko la vita, ghasia na mashambulizi ya kigaidi; mambo yanayodhalilisha dini na kufanya kufuru dhidi ya Mwenyezi Mungu. Kuna haja ya kuwa na malezi pamoja na majiundo makini kwa viongozi wa kidini, ili kusaidia kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho kwa vijana wa kizazi kipya!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, majadiliano ya kweli yanawawezesha waamini kujenga madaraja yanayowakutanisha, tayari kukabiliana na changamoto ambazo amezitaja hivi punde! Ikiwa kama waamini wataheshimu na kuthamini tofauti zao msingi, imani kwa Mwenyezi Mungu itawawezesha kutambua, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hawa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wenye: haki sawa, dhamana na wajibu; utu na heshima yao na kwamba, wanapaswa kuishi kama ndugu wamoja, ili kueneza tunu: wema, upendo na amani. Ndiyo maana anasema Baba Mtakatifu, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu vinapaswa kuwawezesha waamini wote kuishi kadiri ya imani yao; mambo msingi yanyofumbatwa katika utu na heshima yao kama binadamu!

Kumbe, waamini wa dini mbali mbali wakuze na kudumisha maridhiano; kwa kutajirishana, kushirikiana na kushikamana, ili kujenga madaraja ya majadiliano ya kidini katika misingi ya utulivu, urafiki na udugu. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, mwezi Januari 2016 mjini Marrakesh, nchini Morocco kulifanyika mkutano wa kimataifa kuhusu haki za waamini wenye idadi ndogo katika ulimwengu wa dini ya Kiislam. Wajumbe wa mkutano huu, kwa nguvu zote walilaani vitendo vinavyodhalilisha dini, vinavyosababisha ubaguzi na utengano, ghasia na vurugu. Viongozi hao wakakazia umuhimu wa kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, haya ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika masuala ya kisheria.

Ujenzi wa Taasisi ya Kiekumene ya Al Mowafaqa mjini Rabat, kunako mwaka 2012 ni alama ya kinabii, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na kidini na utamaduni wa dini ya Kiislam. Ni alama ya ushuhuda wa huduma ya udugu wa kibinadamu! Hizi zote ni jitihada za makusdi kabisa katika kupambana na vitendo vya chuki na uhasama; vita na ghasia pamoja na misimamo mikali ya kidini na kiimani; vitendo vya kigaidi na dhuluma kwa kisingizio cha udini. Baba Mtakatifu anakaza kusema, majadiliano ya kidini yanayovaliwa njuga kwa wakati huu pamoja na mambo mengine, yanalenga kukuza na kudumisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Itakumbukwa kwamba, Mkutano wa kimataifa kuhusu mazingira COP22 mwaka 2016 ulifanyika nchini Morocco. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inalinda na kutunza mazingira, kwa kujikita katika wongofu wa kiekolojia kwa ajili ya mchakato wa maendeleo fungamani. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumshukuru Mungu kwa hatua mbali mbali ambazo zimefikiwa, kwa kukazia mshikamano kati ya Mataifa, ili hatimaye, kupata suluhu ya haki na inayodumu, dhidi ya majanga yanayoendelea kumwandama mwanadamu, kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa pamoja na kupambana na umaskini duniani

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inang’oa mambo yote yanayopelekea watu kulazimika kuzikimbia nchi na familia zao, na hivyo kujikuta wakiwa ni wakimbizi, ambao wakati mwingine, hawapokelewi! Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018 “Global Compact 2018” uliotiwa mkwaju huko Marrakesh, Morocco unapania kuwa hati rejea kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ni wakati wa kusonga mbele kutoka katika ngazi ya dhamana ya kimaadili na kuanza utekelezaji wake kwa vitendo.

Kuna haja ya kuwaheshimu na kuwathamini wakimbizi na wahamiaji katika sera na maamuzi mbali mbali yanayotekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa, wanaolazimika kutafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Morocco iliyokuwa mwenyeji wa mkutano ule, itaendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa ajili ya huduma na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji, ili waweze kupokelewa, kulindwa, kuendelezwa na hatimaye, kushirikishwa katika maisha ya nchi wahisani, kwa kuheshimu na kuthamini utu wao, ili kwamba, hali na mazingira yatakapoboreka, waweze tena kurejea katika nchi zao wenyewe!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuta za utengano, kutotoa msaada kwa familia husika, kamwe haitaweza kuwa ni suluhu katika mchakato wa kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Jibu makini linafumbatwa katika haki jamii, itakayoweza kukuza na kudumisha amani; kwa kuweka uwiano wa kiuchumi ili kudhibiti mipasuko ya kisiasa ambayo imekuwa inatishia maisha ya binadamu! Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wa Serikali ya Morocco kwa kutambua na kuthamini mchango wa Wakristo nchini humo na kwamba, wanapenda kushiriki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo. Kanisa Katoliki nchini Morocco litaendelea kuchangia katika huduma za kijami, hasa katika sekta ya elimu kama jukwaa la majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa wanafunzi.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza Wakristo walioko nchini Morocco kuendelea kujipambanua kama wahudumu, wahamasishaji na walinzi wa udugu wa kibinadamu!

Kipindi Maalum 2019
30 March 2019, 17:32