Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2019 Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2019 

UJUMBE WA PAPA FRANCISKO KWA KWARESIMA 2019

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa wokovu wa kazi ya uumbaji; madhara ya nguvu ya dhambi na kifo; pamoja na nguvu ya utakaso inayofumbatwa katika toba na msamaha. Anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Mama Kanisa anawajalia waja wake kujiandaa kwa furaha na utakaso wa roho kuweza kuadhimisha Fumbo la Pasaka kwa mioyo sasfi ili hatimaye, kuifikia Pasaka ya milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu”. (Rej. Rom. 8:19). Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa wokovu wa kazi ya uumbaji; madhara ya nguvu ya dhambi na kifo; pamoja na nguvu ya utakaso inayofumbatwa katika toba na msamaha. Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Mama Kanisa anawajalia waja wake kujiandaa kwa furaha na utakaso wa roho kuweza kuadhimisha Fumbo la Pasaka kwa mioyo sasfi ili hatimaye, kuifikia Pasaka ya milele!

Watu wote wamekombolewa kwa njia ya Fumbo la Pasaka na matumaini katika Kristo Yesu. Hili ni fumbo ambalo linaendelea kutenda kazi katika maisha ya watu hapa duniani, kwani huu ni mchakato unaofumbata historia na kazi nzima ya wokovu “Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu”. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anapenda kutoa dondoo zitakazosaidia toba na wongofu wa ndani katika kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2019.

Wokovu wa kazi ya uumbaji: Maadhimisho ya Juma Kuu ambamo Mama Kanisa anakumbuka kwa namna ya pekee kabisa: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, mwaliko na wito wa kujitambua kwamba, tangu asili wamechaguliwa ili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, yaani Kristo Yesu. Ikiwa kama mwamini anaishi kama mwana wa Mungu, mtu aliyekombolewa na anajiachilia ili kuongozwa na Roho Mtakatifu, atafahamu jinsi ya kumwilisha Amri za Mungu, kwa kuanzia na zile ambazo zimechapwa katika moyo na katika mazingira, kimsingi atajitahidi kutunza mazingira kama njia ya kushiriki ukombozi wake!

Ni kwa njia hii, Mtakatifu Paulo, Mtume, anatamani sana kuona watoto wa Mungu, yaani wale wote ambao wanafaidika kutokana na neema ya Fumbo la Pasaka, wanaishi kikamilifu matunda ya kazi ya wokovu, itakayofikia utimilifu wake katika wokovu wa mwili wa mwanadamu. Pale ambapo upendo wa Kristo unajifunua kwa njia ya maisha ya watakatifu wake katika roho, nafsi na mwili; watakatifu hawa wanamtolea Mwenyezi Mungu sifa, heshima na utukufu; kwa sala na tafakari; na kwa sanaa inayovishirikisha viumbe vyote amana inavyojidhihirisha kwa namna ya pekee katika utenzi wa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Lakini kwa bahati mbaya, utulivu ulioletwa kwa njia ya wokovu unatishiwa na nguvu ya dhambi na kifo.

Madhara ya Nguvu ya Dhambi na Kifo! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, pale ambapo waamini wanashindwa kuishi kama waana wa Mungu, hasa kwa kutenda kinyume na upendo kwa jirani, viumbe vingine  vyote na hata kwa watu wenyewe, wanaathirika kutokana na ubinafsi; kwa kutumia kwa ajili ya mafao binafsi. Hali kama hii, inatisha na hivyo kupelekea mtindo wa maisha ambao unakwenda kinyume na hali halisi ya maisha ya binadamu na mazingira yake, ndiyo maana mwandishi wa Kitabu cha Hekima ya Yoshua Bin Sira anahimiza uchaji wa Mungu katika majaribu, kwa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza kama rejea ya maisha yao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, bila ya kuwa na dira na mwongozo sahihi wa maisha kuelekea katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, ni wazi kwamba, watu wataongozwa na mantiki ya kutaka yote, mara moja na kuendelea kupata zaidi na zaidi. Ikumbukwe kwamba, chanzo cha ubaya wowote ule ni uwepo wa dhambi inayoharibu uhusiano na umoja kati ya Mungu, jirani na mazingira ambayo wanaunganishwa nayo kwa njia ya miili yao. Kuvunjilia mbali uhusiano na Mungu, mwanadamu amejikuta akiharibu uhusiano na jirani zake pamoja na mazingira na matokeo yake ile bustani nzuri kama inavyosimuliwa kwenye Kitabu cha Mwanzo, inageuka kuwa jangwa.

Huo ukawa ni mwanzo wa dhambi inayomfanya mwanadamu kujisikia kuwa kama mungu mdogo na mmiliki wa viumbe vingine vyote anayeweza kuvitumia kwa mafao binafsi hata kama ni kinyume cha utashi wa Mungu hali inayopelekea pia kusigina watu na viumbe vingine! Pale ambapo Sheria ya Mungu ambayo ni upendo, inapowekwa “kibindoni” na matokeo yake watu kuanza kutumia “Sera” za “Mwenye nguvu mpishe”, hiki ni kielelezo cha dhambi ambayo imekita mizizi yake katika moyo wa mwanadamu. Matokeo yake anasema Mwinjili Marko ni hila, ufisadi na kijicho; kwa kutoguswa na mahangaiko, ustawi na mafao ya watu wengine na hata wakati mwingine mafao yake binafsi.

Baba Mtakatifu anaendelea kupembua hali hii kwa kusema, huu ndio mwanzo wa matumizi mabaya kazi ya kazi ya uumbaji, watu na mazingira kutokana na tamaa mbaya inayodhani kwamba, kila “kipendacho roho” ni haki, na matokeo yake ndiyo uharibifu hata kwa maisha ya binadamu anayepaswa kutawala viumbe hivi! Nguvu ya utakaso inayofumbatwa katika toba na msamaha anasema Baba Mtakatifu, ni ushuhuda unaopaswa kutolewa na watoto wa Mungu, ambao wamekuwa ni viumbe vipya katika Kristo Yesu na kwamba, ya kale yamekwisha pita na kwa njia yao, viumbe pia vinaweza kusherehekea Pasaka.

Hija ya Kipindi cha Kwaresima iwasaidie Wakristo kupyaisha sura na roho zao kama waamini, kwa njia ya toba, wongofu wa ndani na msamaha wa dhambi, ili kuweza kufaidika na neema zinazobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka! Uvumilivu huu utapata utimilifu wake pale ambapo watoto wa Mungu wataanza kufumbata wongofu wa ndani, kwa kujikwamua kutoka katika utumwa wa dhambi, rushwa na ufisadi ili kuingia katika utukufu wa waana wa Mungu. Kipindi cha Kwaresima ni Kisakramenti cha toba na wongofu wa ndani, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kukita zaidi maisha yao katika Fumbo la Pasaka kwa njia ya maisha binafsi, kifamilia, na kijamii, kwa njia ya kufunga, kusali pamoja na matendo ya huruma!

Kufunga anasema Baba Mtakatifu ni kubadili mtindo na mtazamo kwa jirani pamoja na mazingira, ili kuondokana na kishawishi cha kutaka “kukumbatia yote” ili kutosheleza tamaa, kiasi hata cha kufifisha upendo unaoweza kuzima utupu wa moyo wa mtu! Kusali ni kutoa nafasi ya kwanza kwa Mwenyezi Mungu kwa kuondokana na tabia ya kupenda kuabudu miungu wa uwongo, kwa kudhani kwamba, binadamu anaweza kujitosheleza mwenyewe bila ya kumtegemea Mwenyezi Mungu. Kusali ni kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, binadamu daima ana kiu ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake.

Matendo ya huruma yawawezeshe waamini kuondokana na tamaa ya kutaka kujilimbikiza mali na utajiri, kwa lengo la kuwa na uhakika wa kesho iliyo bora zaidi na kusahau kwamba, hapa duniani, binadamu ni mpita njia tu! Waamini wajibidishe kutafuta furaha ya kweli katika mpango wa Mungu kwenye kazi ya uumbaji ambayo ni upendo kwa Mungu na jirani; upendo kwa kazi ya uumbaji na mazingira, hiki ni kielelezo cha furaha ya kweli katika maisha ya binadamu! Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake wa Kwaresima kwa kusema, Kwaresima ya Mwana wa Mungu ni mchakato wa kuingia katika Jangwa la Kazi ya Uumbaji, ili kurejesha tena mazingira kuwa ni Bustani ya umoja na Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kabla ya dhambi ya asili.

Kwaresima kiwe ni kipindi cha kupandikiza matumaini ya Kristo hata katika kazi ya uumbaji kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru na utukufu wa watoto wa Mungu. Kwaresima ni kipindi kilichokubalika, waamini wakitumie kikamilifu, kwa kutubu na kumwongokea Mungu. Ni wakati muafaka wa kuachana na ubinafsi, uchoyo na kuanza kujielekeza zaidi kwa ajili ya huduma, ustawi na maendeleo ya jirani wanaoteseka, ili kushirikishana tunu za maisha ya kiroho na kimwili. Kwa njia hii, waamini wataweza kuupokea ushindi wa Kristo Mfufuka katika maisha yao kwa kushinda dhambi na kifo na kuanza mchakato wa kutumia nguvu hii kuleta mabadiliko katika kazi ya uumbaji.

Papa: Kwaresima 2019
05 March 2019, 06:40