Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Papa Francisko: Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. 

Baba Mtakatifu Francisko: Ujumbe kwa Siku ya Maji Duniani 2019

Maadhimisho ya Mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “hakuna kumwacha mtu nyuma katika kupata huduma ya maji ifikapo mwaka 2030” kwa kuzingatia lengo namba 6 la Malengo ya Maendeleo endelevu, ifikapo mwaka 2030. Maji ni hitaji muhimu sana katika maisha ya binadamu na linachangia katika mchakato wa kuweka uwiano sawa katika mazingira na maisha ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 22 Machi 2019 inaadhimisha Siku ya Maji Duniani, huku kukiwa na taarifa kwamba, kuna watu zaidi ya bilioni mbili ambao hawana uhakika wa maji safi na salama. Ukame wa kutisha ni chanzo kinachowapelekea watu kuzikimbia nchi na familia zao. Uchafuzi wa vyanzo vya maji na ukosefu wa uhakika wa maji safi na salama ni changamoto pevu hasa katika nchi changa zaidi duniani. Uhakika wa maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Maadhimisho ya Mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “hakuna kumwacha mtu nyuma katika kupata huduma  ya maji ifikapo mwaka 2030” kwa kuzingatia lengo namba 6 la Malengo ya Maendeleo endelevu, SDGs, ifikapo mwaka 2030.

Maji ni hitaji muhimu sana katika maisha ya binadamu na linachangia katika mchakato wa kuweka uwiano sawa katika mazingira na maisha ya watu katika ujumla wake. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watu wanapata maji safi na salama kwa ajili ya mahitaji yao. Kila kukicha hitaji la maji safi na salama linaendelea kuongezeka maradufu duniani na ikumbukwe kwamba, hii ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Kauli mbiu ya “hakuna kumwacha mtu nyuma katika huduma ya maji” ni muhimu sana kwa sababu inagusa: Uhai, utu na heshima ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kuunganisha nguvu ili kuhakikisha kwamba, hata maskini wanafanikiwa kupata maji safi na salama, kwa kuhakikisha kwamba, haki ya maji, inakuwa ni sehemu ya sera na mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa, ili haki ya watu kupata maji safi na salama iweze kutendeka!

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani kwa Mwaka 2019, aliomwandikia Profesa Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kama sehemu ya maadhimisho haya! Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kauli mbiu hii inatekelezwa kwa dhati katika matendo, kwa kuhifadhi miundo mbinu ya maji pamoja na kuwekeza katika kutafuta maji safi na salama sanjari na kutoa elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya, ili kuhakikisha kwamba, wanatumia maji kwa uangalifu sana. Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema, hii inatokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya watu wanatumia vibaya maji.

Vijana pamoja na wakazi wote wa dunia hii wanaalikwa  kulinda na kutunza amana hii kwa ajili ya wote. Inasikitisha kuona kwamba, kuna uchafuzi mkubwa wa maji sehemu mbali mbali za dunia na matokeo yake ni magonjwa. Kumbe, vijana wafundwe kuhusu matumizi bora ya rasilimali maji. Kila mtu atambue kwamba, anawajibika kulinda na kutunza maji. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika utekelezaji wa miradi ya maji ya muda mrefu, ili kuondokana na kishawishi cha kutaka kugeuza maji kuwa ni bidhaa inayoratibiwa na sheria ya soko duniani! Baba Mtakatifu anakaza kusema, “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanahitaji kuona kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inawasaidia kupata maji safi na salama, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao!

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea wale wote ambao wanateseka kutokana na ukame wa kutisha na wale ambao hawana maji safi na salama. Anakumbusha kwamba, maji ni rasilimali adhimu inapaswa kutumiwa kwa unyenyekevu kwa ajili ya kizazi cha sasa na maendeleo ya kizazi kijacho!

Papa: Maji Duniani 2019
22 March 2019, 17:09