Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu: Mapenzi ya Mungu ni wokovu wa watu wake, mema na amani! Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu: Mapenzi ya Mungu ni wokovu wa watu wake, mema na amani!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Mapenzi ya Mungu ni wokovu, amani na mema yote!

Mapenzi ya Mungu bila shaka yoyote ile ni wokovu wa binadamu anayeshirikishwa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Mwenyezi Mungu anataka waja wake wawe huru na kuendelea kutembea katika upendo, kwani anawatakia watoto wake mema na wokovu. Hii ni sala inayowataka waamini kuwa jasiri dhidi ya mambo yanayokwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

 Sala ya Baba Yetu ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Ni Sala ambayo ina maombi saba yanayoelekezwa kwa Mwenyezi Mungu, kama kielelezo cha upendo wa dhati unaowaka kutoka katika undani wa mwamini kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Hili ndilo kundi la kwanza la maombi yanayoelekezwa kwa Mungu yaani: Jina lako litukuzwe, Ufalme wako ufike, Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Mapenzi ya Mungu ni watu wote waokoke, wapate kuyajua yaliyo ya kweli na kupendana wao kwa wao kama Mwenyezi Mungu anavyowapenda.

Kristo Yesu ni kielelezo cha utimilifu wa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni, kwa njia ya utii, mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu! Ili kuweza kuingia mbinguni, mwamini anapaswa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake! Mwenyezi Mungu daima amekuwa “akichakarika usiku na mchana” kama inavyoonesha Injili kumtafuta mwanadamu aliyetopea katika dhambi ili aweze kutubu na kumwongokea kama ilivyokuwa kwa Zakayo, tajiri, mtoza ushuru lakini mfupi wa kimo, aliyetamani sana kumwona Kristo Yesu katika maisha yake, kiasi cha kupanda juu ya mkuyu! Kristo Yesu alipofika mahali pale, akamwambia Zakayo ashuke upesi, kwani alitamani kushinda nyumbani kwake, kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

Kwa maneno mengine, Kristo Yesu, alikuja kuyafanya mapenzi ya Mungu ambayo yamemwilishwa kwenye Sala ya Baba yetu! Waamini wanasali na kuomba, ili mapenzi ya Mungu yafanyike hapa duniani kama sehemu ya utekelezaji wa kazi ya ukombozi. Hii inatokana na ukweli kwamba, daima Mwenyezi Mungu anajitaabisha kuwatafuta watoto wake kama kielelezo cha upendo na huruma yake isiyokuwa na kikomo! Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 20 Machi 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi kuhusu Sala ya Baba Yetu, Sala ya Bwana!

Mwenyezi Mungu hakutaka kujificha bali ameamua kuja ulimwenguni, ili kuwaokoa watu wake. Maandiko Matakatifu yanafafanua kuhusu ushuhuda wa mapenzi ya Mungu, unaojikita katika uaminifu na uvumilivu. (Rejea KKK. N. 2821-2827). Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Timotheo, anakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu anataka watu wote waokolewe na kupata kujua yaliyo kweli. Mapenzi ya Mungu bila shaka yoyote ile ni wokovu wa binadamu anayeshirikishwa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Mwenyezi Mungu anataka waja wake wawe huru na kuendelea kutembea katika upendo, kwani Mwenyezi Mungu anawatakia watoto wake mema na wokovu.

Hii ni sala inayowataka waamini kuwa jasiri dhidi ya mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu. Kwa muhtasari tu, bado duniani kuna vita, upotofu, unyonyaji, dhuluma na maasi, lakini pia wanatambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima anawatakia mema, ndiyo maana kwa imani na matumaini thabiti wanathubutu kusema, “Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni”, ili watu wafue panga zao ziwe majembe na mikuki yao iwe miundu na wala hawatajifunza vita kamwe! Kwa sababu Mwenyezi Mungu anataka amani kwa ajili ya watu wake!

Sala ya Baba Yetu inawasha moto wa mapendo kwa Kristo Yesu, aliyekuja kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni, ni moto unaowasukuma waamini kufanya mageuzi ulimwenguni kwa kujikita katika upendo! Kwa hakika, wokovu wa Mungu utafunuliwa kwa watu wa Mataifa wakati wa utimilifu wa nyakati. Waamini wanasali kumwomba Mwenyezi Mungu ili waweze kushinda ubaya kwa kutenda wema, kiasi hata cha kutii na kujinyenyekesha wakati wa majaribu magumu na mazito katika maisha!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Bustanini Getsemani, Kristo Yesu alionja mateso makali kiasi cha kumwomba Baba yake wa mbinguni akisema, “Ee Baba, ikiwa kama ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke” (Lk. 22:42). Kristo Yesu aliushinda ulimwengu, kwa kujiaminisha na kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa milele, kiasi cha kuteswa, kufa na hatimaye, kufufuka kutoka kwa wafu. Wakati mwingine, Mwenyezi Mungu anaweza kumwachia mwamini kutembea katika magumu ya maisha, kuonja mateso na hata kuchomwa na miiba, lakini daima anatembea bega kwa bega, kati pamoja na waja wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, haya ndiyo matumaini na ukweli wa maisha kwamba, Mwenyezi Mungu yuko pamoja na waja wake, ndiyo maana wanahamasishwa kuwa na sala endelevu katika maisha, kwani iko siku wataweza kuona haki ya Mungu ikitendeka kati yao! Mwishoni, wote wamesali Sala ya Baba Yetu, kila mtu katika lugha yake mwenyewe, ili kweli mapenzi ya Mungu yafanyike duniani kama mbinguni!

Papa: Sala ya Baba Yetu
20 March 2019, 15:51