Tafuta

Vatican News
Papa Francisko. Heri za Mlimani ni chemchemi ya uongozi bora! Papa Francisko. Heri za Mlimani ni chemchemi ya uongozi bora!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Heri za Mlimani: Ni chemchemi ya uongozi bora!

Kristo Yesu anawaonesha wafuasi wake Heri za Mlimani kama: hekima na njia salama wanayopaswa kuifuata kama dira ya uongozi. Upole, unyenyekevu na huruma, mambo msingii kwa kiongozi kuwa mkweli, mnyenyekevu na mtu wa haki. Viongozi wanapaswa kuondokana na unafiki pamoja na hali ya kujikweza, ili kuona boriti machoni pao, ili kuwasaidia wengine kuwa watu bora zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili VIII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa na kwa namna ya pekee kabisa, Injili inayosimulia mifano mitatu iliyotolewa na Kristo Yesu ni mwaliko wa kutafuta na kufumbata hekima, kama dira na mwongozo wa watu wa Mungu, vinginevyo, watakaiona cha mtema kuni. Kwani kipofu hawezi kumwongoza kipofu mwenzake. Walengwa wakuu wa sehemu hii ya Injili ni wale wahusika wakuu katika malezi na makuzi; viongozi wa maisha ya kiroho, viongozi wa Serikali na jamii; watunga sera na sheria; walimu na wazazi; makundi ambayo yanapaswa kuwa makini katika kutekeleza dhamana na wajibu wake pamoja na kuwa na mang’amuzi ya kufuata njia sahihi ya kuwaongoza watu waliokabidhiwa kwao!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 3 Machi 2019. Kristo Yesu anawaonesha wafuasi wake Heri za Mlimani kama: hekima na njia salama wanayopaswa kuifuata kama dira ya uongozi. Upole, unyenyekevu na huruma, mambo msingi yanayomwezesha kiongozi kuwa mkweli, mnyenyekevu na mtu wa haki. Viongozi wanapaswa kuondokana na unafiki pamoja na hali ya kujikweza, ili kuona boriti machoni pao, tayari kuwasaidia jirani zao kuondoa vibanzi vilivyomo machoni pao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni ukweli usiofumbiwa macho kwamba, watu wengi wanapenda kuwalaani wengine kutokana na makosa pamoja na dhambi zao, kiasi hata cha kushindwa kuona makosa na dhambi zake mwenyewe. Ni watu wanaojihurumia sana wenyewe, lakini kwa wengine, wanakuwa ni wakali na wakatili sana. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanashauriwa kuwasaidia jirani zao kwa ushauri mzuri, wakati huo huo, wakitambua kwamba, hata wao wana mapungufu na wawe tayari kukosolewa, kwani kukosoa na kukosoana ni kujengana katika fadhila ya udugu!

Kwa njia hii, waamini wataweza kuwa kweli watu wanaoaminika, watu wenye unyenyekevu na mashuhuda wa upendo! Watu wanaweza kutambulikana kuwa ni wema au wabaya kutokana na ushuhuda wa maneno na matendo yao. Kile kilicho chema, kizuri na kitakatifu kinabubujika kutoka katika moyo wa mtu mwema na kushuhudiwa kwa njia ya maneno! Kwa mtu wenye moyo mbaya na roho ya kwa nini? Huyo ataonekana na kusikika hata kwa maneno yake! Hawa ndio wale “wanaopika majungu”  usiku na mchana; watu wasioridhika hata kidogo na matokeo yake ni watu wenye “litania za manung’uniko” kila kukicha! Ni watu wanaowateta jirani zao na kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa!

Tabia ya namna hii anasema Baba Mtakatifu Francisko ni hatari sana, kwani inasambaratisha familia, shule, maeneo ya kazi na makazi ya watu. Mara nyingi vita inaanza kwa maneno! Kumbe, hii ni nafasi kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu mafundisho ya Kristo Yesu, kwa kujiuliza, Je, mimi ninawateta wengine? Ninataka kuwaharibia sifa zao njema? Je, niko mwepesi kuona makosa ya wengine kuliko makosa yangu mwenyewe? Mtu akishagundua udhaifu na mapungufu yake mwenyewe aanze kujitakasa na hali hii itakuwa ni msaada kwa watu wengi zaidi! Maombezi ya Bikira Maria yawe ni msaada katika kufuata nyayo za Kristo Yesu katika mafundisho yake!

Papa: Sala Malaika Bwana

 

03 March 2019, 09:55