Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye katika sala kwa ajili ya kuwaombea waamini wa dini ya Kiislam walioshambuliwa! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye katika sala kwa ajili ya kuwaombea waamini wa dini ya Kiislam walioshambuliwa!  (AFP or licensors)

Papa: Mshikamano na waamini wa dini ya Kiislam New Zealand

Baba Mtakatifu Francisko anasema, licha ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inayoendelea kurindima sehemu mbali mbali za dunia dhidi ya binadamu, hivi karibuni tena, kumetokea shambulizi la kigaidi dhidi ya waamini wa dini ya Kiislam waliokuwa wanaswali huko Christchurch, New Zealand. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka na kuwaombea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 17 Machi 2019, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye kwa ajili ya kusali na kuwaombea waamini wa dini ya Kiislam 50 waliouwawa, Ijumaa, tarehe 15 Machi 2019 mjini Christchurch, nchini New Zealand kutokana na vitendo vya kigaidi na ubaguzi wa rangi. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu alikwisha tuma salam za rambi rambi katika ujumbe uliotiwa sahihi na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, akionesha majonzi yake makubwa kutokana na vitendo hivi vinavyodhalilisha: maisha, utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, licha ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inayoendelea kurindima sehemu mbali mbali za dunia dhidi ya binadamu, hivi karibuni tena, kumetokea shambulizi la kigaidi dhidi ya waamini wa dini ya Kiislam waliokuwa wanaswali huko Christchurch, New Zealand. Baba Mtakatifu anawaombea wale wote waliofariki dunia katika shambulizi hili pamoja na familia zao. Amechukua fursa hii, kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Jumuiya ya waamini wa dini ya Kiislam. Amewaomba kwa mara nyingine tena, kuungana pamoja naye katika sala ili kuimarisha amani na maridhiano kati ya watu, dhidi ya chuki na uhasama!

Taarifa zinaonesha kwamba, shambulizi hili limefanywa na Brenton Harrison Tarrant, mwananchi kutoka Australia, mwenye umri wa miaka 28. Huyu ni kijana mwenye msimamo mkali anayejihusisha na sera pamoja na itikadi kali za ubaguzi wa rangi, zilizompelekea hata kufanya mashambulizi huko New Zealand. Bado kuna watu 36 ambao wamelazwa hospitalini na hali zao zinasemekana kuwa mbaya. Brenton Harrison Tarrant kwa mara ya kwanza amefikishwa Mahakani tarehe 16 Machi 2019 na anatarajiwa kurejeshwa tena Mahakamani tarehe 5 Aprili 2019 ili kusomewa mashitaka ya mauajia ya kukusudia.

Taarifa kwa vyombo vya habari kutoka katika Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, inaonesha masikitiko makubwa kwa mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, waliokuwa wanasali. Kitendo hiki ni kufuru dhidi ya utakatifu wa nyumba ya Sala na Ibada. Haya ni matokeo ya mahubiri ya chuki na uhasama yanayofanywa na baadhi ya waamini. Kumbe, huu ni mwaliko kwa waamini wa dini mb, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Kwa upande wake, Serikali ya Marekani imeonesha kusikitishwa sana na mashambulizi haya ya kigaidi na inaungana na wananchi wa New Zealand katika kipindi hiki cha maombolezo makubwa kwa watu wake waliopoteza maisha! Salam za rambi rambi zimetolewa pia na viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa akiwemo Rais Vladimr Puttin wa Urussi, Bwana Claude Junker, Rais wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya pamoja na Rais Sergio Mattarella wa Italia.

Papa: New Zealand
17 March 2019, 12:30