Tafuta

Papa Francisko anawataka vijana kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo! Papa Francisko anawataka vijana kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo! 

Papa Francisko: Vijana simameni kidete kutetea uhai!

Chama cha Kutetea Maisha Italia katika kipindi cha miaka 43 kimekuwa ni chachu ya kupokea, kuenzi na kuheshimu Injili ya uhai kwa kutambua kwamba, maisha ni matumaini ya siku za mbeleni. Mambo ya kuzingatia: watu wawe wakarimu kupokea zawadi ya uhai. Ujauzito unapaswa kuangaliwa kama mchakato wa mahusiano, umoja na mafungamano ya dhati kati ya mama na mtoto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumapili tarehe 3 Februari 2019 linaadhimisha Siku ya 41 ya Maisha Kitaifa inayoongozwa na kauli mbiu “Maisha ni matumaini kwa siku za mbeleni”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 2 Februari 2019 amekutana na kuzungumza na wanachama wa Chama cha Kutetea Maisha Italia, (MpV). Ametumia fursa hii kuwapongeza kwa utume unaowasukuma kujisadaka kwa ajili ya kutetea Injili ya uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi kutoa kipaumbele cha pekee katika kutunza hadhi ya maisha ya binadamu, dhamana inayopaswa kutekelezwa na jamii nzima, kila mtu kadiri ya utume na nafasi yake katika jamii. Chama cha Kutetea Maisha Italia, (MpV) katika kipindi cha miaka 43 kimekuwa ni chachu ya kupokea, kuenzi na kuheshimu Injili ya uhai kwa kutambua kwamba, maisha ni matumaini ya siku za mbeleni. Jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, watu wanakuwa wakarimu kupokea zawadi ya uhai, tayari kuilinda kama kielelezo cha umama bora.

Ujauzito unapaswa kuangaliwa kama mchakato wa mahusiano, umoja na mafungamano ya dhati kati ya mama na mtoto ambaye bado yuko tumboni! Wazazi wanashiriki kwa namna ya pekee kabisa katika mpango wa kazi ya uumbaji na kwamba, Mungu wa kweli peke yake ndiye anayetangaza na kuleta wokovu kama anavyosema Nabii Isaya, tazama, nitatenda neno jipya! Baba Mtakatifu anakazia uzuri na utakatifu wa maisha unaochipuka kutoka katika Injili ya uhai na kwamba, binadamu hana haki yoyote ile ya kutema zawadi ya uhai, kwa kutoa mimba, kwani kwa kufanya hivi ni kukiuka wito unaowaunganisha ili kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mahali ambapo kuna Injili ya uhai, hapo kuna matumaini! Lakini pale ambapo watu wanachezea zawadi ya maisha kama “mpira wa kona”, hapo, watu wanashindwa kuona zawadi ya Injili ya uhai na hivyo kuigeuza kuwa kama kitu kinachoweza kutumika au kutupiliwa mbali kama taka! Utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba kwa sasa unaonekana kuwa ni haki ya kibinadamu na kusahau mateso na mahangaiko ya watoto wachanga ambao bado hawajazaliwa.Waamini wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha uhai kwa kutambua na kuheshimu nguvu ya Mungu, licha ya udhaifu wao wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu amewapongeza na kuwashuruku vijana ambao wamejiunga na Chama Cha Kutetea Maisha Italia, jambo linalowafanya kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu! Uwepo na ushiriki wa vijana katika Chama hiki ni amana na utajiri mkubwa wa Kanisa na jamii katika ujumla wake, katika mustakabali wa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Vijana ni chachu inayoendelea kupyaisha hata maisha ya watu ambao umri wao unazidi kwenda mbio!

Vijana wanapaswa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa uwazi na ujasiri, daima wakisimama kidete kulinda maisha ambayo ni kito cha thamani kubwa. Chama hiki kinapaswa kutambuliwa na kuheshimiwa na watu wote wenye mapenzi mema kutoka katika medani mbali mbali za maisha. Kwa njia ushuhuda huu, vijana wametangaza imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watoto waliouwawa kwa kutolewa mimba, ni sehemu ya jamii na kwamba, mauaji yao yanatia shaka ujenzi wa misingi ya haki inayogusa undani wa utu wa binadamu na jamii katika ujumla wake!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Uhai Kitaifa nchini Italia anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika wanasiasa wote kutoa kipaumbele cha kwanza katika kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai ambayo ni matumaini ya leo na kesho ya binadamu. Mafanikio na mafao binafsi, kamwe yasiwe ni chanzo cha kuvuruga Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Zawadi ya maisha, iwe ni changamoto kwa watu wote kusimama kidete kuipokea kwa furaha na kwa mikono miwili. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Injili ya uhai!

Injili ya Uhai dhidi ya Utamaduni wa kifo

 

02 February 2019, 14:54