Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anasema, majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya waamini wa dini mbali mbali. Papa Francisko anasema, majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya waamini wa dini mbali mbali. 

Papa Francisko: Majadiliano ya kidini ni vinasaba vya waamini!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali ni nyenzo msingi ya kupambana na tabia ya ubinafsi, misimamo mikali ya kidini na kiimani ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na maridhiano kati ya watu, kila mtu akipewa nafasi ya kushuhudia imani yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawahimiza Wakristo kwa busara na mapendo, kwa njia ya majadiliano ya kidini, umoja na ushirikiano na waamini wa dini nyingine, kutoa ushuhuda wa imani na wa maisha yao. Waamini watambue, wahifadhi na kukuza mema ya kiroho, kimaadili, pamoja na tunu msingi za kijamii na za kitamaduni ambazo zinapatikana kutoka kwa waamini wa dini nyingine.

Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali ni nyenzo msingi ya kupambana na tabia ya ubinafsi, misimamo mikali ya kidini na kiimani ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na maridhiano kati ya watu, kila mtu akipewa nafasi ya kushuhudia imani yake! Kumbe, katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Wakristo wanapaswa kumuungama Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chanzo cha imani, furaha na matumaini kwa waja wake. Mwenyezi Mungu ni kiini cha majadiliano na watu wake na kamwe hajaacha kuzungumza na wanawadamu katika safari ya maisha yao hapa duniani, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale hata leo hii, Mwenyezi Mungu anazungumza na binadamu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele, aliyetumwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Imegota miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na Sultan Malik Al-Kamil, kunako mwaka 1219 huko nchini Misri. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1986, kwa mara ya kwanza katika historia, akawakutanisha viongozi wa kidini huko Assisi kwa ajili ya kusali na kuombea amani duniani! Mkutano huu, ukawa ni chachu ya kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kudumisha amani duniani. Sala na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku ni nyenzo msingi ya ujenzi wa amani duniani. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Miaka 25 baadaye, aliwataka waamini wa dini mbali mbali kuendeleza roho na moyo wa sala kutoka Assisi kwa kudumisha majadiliano na upatanisho.

Baba Mtakatifu Francisko anasema majadiliano ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya waamini wa dini mbali mbali duniani. Ni majadiliano ambayo yanafumbatwa katika utu na tunu msingi za maisha ya binadamu, ili kujenga na kudumisha leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika amani ya kweli. Jambo la msingi ni waamini kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani kwa njia ya majadiliano katika ukweli, uwazi, haki na usawa! Umoja, udugu na usawa ni nyenzo madhubuti dhidi ya vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kiimani.

Leo hii, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, waamini wa dini mbali mbali wanakabiliwa na changamoto kuu tatu: Mosi, Utambulisho wa dini yao; nani ni Mungu wao na ushuhuda wa maisha mintarafu kile wanacho kiamini katika maisha. Pili ni changamoto pia ya kuheshimu watu wenye imani tofauti kwa kutambua kwamba, hawa si adui bali ni wanandani wa hija ya maisha kuelekea katika ukweli. Tatu ni changamoto ya ukweli katika imani wanayoungama na kuishuhudia. Yote haya yakizingatiwa kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini, hakuna sababu ya vita vya kidini, nyanyaso na dhuluma kwa misingi ya kiimani kama inavyoshuhudiwa kwa sasa sehemu mbali mbali za dunia.

Majadiliano ya kidini ni sehemu muhimu sana inayoweza kuwasaidia waamini kufahamu imani yao kwa dhati, ili kuweza kuitangaza na kuishuhudia, vinginevyo hapa ni shughuli pevu kabisa, kwani badala ya amani na utulivu, watu watakuwa na woga, mashaka na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wasiwe na woga wa kutangaza na kushuhudia imani kwa watu wa Mataifa, huu ni utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho.

Majadiliano ya kidini
02 February 2019, 15:52